Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alifanya ziara ya kikazi jijini Seoul, Jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko kutoka kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Yun Byung-se ambapo Waziri
Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kumpatia mwaliko wa
kutembelea taifa hilo hususan wakati huu inapoadhimishwa jubilee ya
miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa
kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati katika uwekezaji kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.
Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275 pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600 imejengwa
na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi
teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine
maalum kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake.
Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto Chanika yenye uwezo
wa kulaza wagonjwa 160 inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha,
Watanzania zaidi ya 1000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma
katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya Korea.
Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea ambapo
alitumia fursa hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania
mathalani ujenzi wa Reli ya Kati katika viwango vya kimataifa;
uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; ujenzi wa maeneo ya
viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika miradi mikubwa.
Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia wawakilishi wa makampuni
ya Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na
biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma mbalimbali katika
sekta hiyo.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kukutana na Balozi Sul Kyung-hoon Makamu
wa Rais wa KOICA ambapo aliishukuru Taasisi hiyo kwa kuipatia zaidi
misaada Tanzania kwa uwazi na bila ya masharti yeyote. Pia aliipongeza
KOICA kwa kushirikisha jamii kuanzia wakati wa ubunifu wa mradi hadi
kufikia utekelezaji pamoja na usimamizi.
KOICA
wameombwa kuongeza maeneo ya misaada na kujumuisha maeneo ya ujenzi wa
miundombinu ya maji na nishati ya umeme wa jua, upepo na maji kwa ajili
ya kusaidia maeneo ya vijijini. Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alishauri
KOICA kuangalia uwezekeno wa kuanzisha vituo vya kilimo cha kisasa,
vituo vya kufugia na vituo vya kufundisha ujasiriamali ili jamii kubwa
ya Watanzania iweze kunufaika.
Katika
jitihada za kutafuta washirika kwa ajili ya kusaidia kuboresha Chuo cha
Diplomasia, Mhe. Waziri akiwa Seoul alitembelea Chuo cha Taifa cha
Diplomasia cha Jamhuri ya Korea na kufanya mazungumzo na Balozi
Paik Ji-ah, Kaimu Mkuu wa Chuo. Lengo kuu lilikuwa kujifunza uendeshaji
wa Chuo, mitaala iliyoandaliwa kutoa masomo, walengwa wa masomo hayo,
aina ya wakufunzi, lugha zinazotumika kufundishia, utaratibu wa kuandaa
wanadiplomasia na mifumo ya chuo hicho.
Vilevile
kabla ya kuhitimisha ziara yake, Mhe. Waziri alikutana na Jumuiya ya
Watanzania waishio Jamhuri ya Korea ambapo aliwahimiza kuheshimu Sheria
na Taratibu za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kuleta utaalam utakaosaidia
kuiendeleza Tanzania.
Aidha, akizungumza na
Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, Mhe. Waziri aliwasihi
kuzingatia masomo ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta faida kwa
familia zao na taifa kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri
aliwahakikishia Wanajumuiya hao kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho
za kufungua Ubalozi wa Tanzania jijini Seoul na kuwaomba kutoa
ushirikiano kwa Balozi wa kwanza wa Tanzania katika nchi hiyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 28 Aprili, 2017.
No comments:
Post a Comment