Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watumishi 9932 waliogushi vyeti, kuondoka maeneo yao ya kazi haraka iwezekanavyo kabla hawajadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akikabidhiwa taarifa ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma sambamba na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka kumi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Watumishi 9932 wenye vyeti vya kugushi na feki mishahara yao ya mwezi huu ikatwe na waondoke kazini mara moja na hizo nafasi zitangwazwe ili wasomi waweze kuziomba na majina yao yawekwe kwenye magazeti ili wajulikane” amesema Rais Magufuli
Aidha amesema kuwa hadi kufika tarehe 15 Mei, 2017 kila mkuu wa Idara mahali pake pa kazi ahakikishe watumishi hao wameondoka na watakao kaidi agizo hilo amevitaka vyombo vya usalama kuwashughulikia.
Hata hivyo Rais Magufuli ameongeza kuwa watumisi 1538 wanaotumia cheti zaidi ya mtu mmoja kutopewa mshahara hadi pale itakapojulikana nani mwenye cheti halali na kuwataka watumishi 11,769 kuwasilisha vyeti vilivyopungua.
Mbali na hayo Rais Magufuli amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kuachana na masuala ya siasa kwa lengo la kujenga nchi kwani watanzania wanahitaji maendeleo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Angela Kairuki amesema kuwa mpaka sasa vyeti vilivyohakikiwa ni 435,000 ambapo imefanyika kwa awamu tatu iliyojumuisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali pamoja na Serikali Kuu.
“Leo tunakabidhi taarifa ya awamu mbili iliyohusisha Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma, Tume na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi na Wakala wa Serikali ambapo imejumuisha uhakiki wa vyeti vya Kidato cha Nne, Sita, vyeti vya ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada” amesema Waziri Kairuki.
Amesema kuwa matokeo ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma yapo ya aina nne ambapo watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.23 wanavyeti halali, watumishi 9932 asilimia 2.4 wanavyeti vya kugushi, watumishi 1538 asilimia 0.3 vyeti vyao vinatumika kwa zaidi ya mtu mmoja na watumishi 11,769 asilimia 2.8 wanavyeti pungufu.
Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisema wizara yake inakumbana na changamoto ya watumishi wa umma kugushi vyeti hivyo aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwani serikali imeziba njia zote za mkato za kuajiriwa na Serikali.
“Leo tunaandika historia ya kipekee kwani suala la uhakiki wa yveti limefanyika kwa mara ya kwanza nchini ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndio yenye jukumu la kuhakiki uhalali wa vyeti hivyo” amesema Prof. Ndalichako.
Zoezi la uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma limeendeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia Mwezi Oktoba, 2016 likiwa na lengo la kubaini uhalali wa vyeti kwa watumishi wake.
1 comment:
Nampongeza sana rais Dr.John pombe Magufuli,kwa kazi zuri ya kupigiwa mfano ya kuwaondoa watumishi hewa,pia nazipongeza taasisisi na vyombo kama Necta,wizara ya elimu na utumishi kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hili adhimu na la kihistoria,katika nchi hiyo rais anania njema na nchi hii na kwa kufanya hivyo anataka watanzania tujifunze kuishi kwa uhalisia tuache maisha ya kuigiza,ajira hizo elfu tisa zitachukuliwa na watu halisi waliosota kwa muda mrefu bila kupata ajira.
pia napenda kushauri kuwa suala hili liwe endelevu ili kuondoa mfumo mbaya wa watumishi waliokuwa wanalisababishia hasara taifa hili.Mtumishi yeyote ambaye unakosa uhalali wa kutumikia taifa hili na bado unaendelea kuchukua pesa ambyo ni kodi ya watanzania yapaswa usutwe na dhamira yako mwenyewe na ujiondoe mapema.
by Dickson kawovela
mwanachi mzalendo
Post a Comment