Friday, April 28, 2017

RAS TABORA AWATAKA WANAWAKE WASHIRIKIANE KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Na Tiganya Vincent-RS-Tabora

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara ametoa wito kwa wanawake mkoani hapa kuungana na kushirikiana pamoja katika shughili za mbalimbali za ujasiriamali ili iwe rahisi kwao kunafaika na fursa mbalimbali mikopo ikiwemo asilimia tano inapaswa kutolewa na Halmashauri zao.

Dkt. Ntara alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora wakati akizindua Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi la Mkoa huo.Alisema kuwa wanawake wakiendelea kufanyakazi kwa ubinafsi hawataweza kuendelea bali wataendelea kubaki nyuma.

Katibu Tawala huyo wa Mkoa alisema kuwa wanawake wakiungana na wakaunda vikiundi vinavyoaminika watapata fursa ya kukopeshwa na Taasisi za fedha zilizopo mkoani Tabora na hivyo kukuza mitaji yao ambapo hatimaye wanaweza kuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda vyao.

Dkt. Ntara aliongeza kuwa wakiungana watapata fursa ya wao kuwa kichocheo cha kuleta maendeleo kuanzia ngazi za familia hadi taifa kutokana na wao kuwa wataalam wazuri wa matumizi ya fedha kidogo wanazopata.

Alisema kuwa mwanamke licha ya baadhi yao kutokwenda shule au kutopata fursa ya kusoma lakini bado Mungu amewajalia maarifa ambayo yanasaidia jamii kama vile kufahamu kuwa mtoto wake anaumwa wakati hajasomea udaktari, kufahamu umuhimu wa kilimo cha mboga mboga kuzungumza nyumba yake licha ya kutosomea ubwana au ubibi shamba, kuwa mtunza fedha mzuri licha ya kutosomea uhasibu.

Dkt. Ntara aliwasisitiza wanawake hao kuwa ni vema wakatumia tunu hiyo waliojaliwa katika kuunda vikundi mbalimbali katika maeneo yao na kuanzisha mradi ambapo utawasaidia wao na familia zao na hivyo kuonyesha kuwa wanawake wanaweza.

Alisema kuwa wakifanikiwa kuunda vikundi katika maeneo yao na vikaonekana havina matatizo atahakikisha kuwa anawabana Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zote za Mkoa huu kuhakikisha kuwa wanawapatia ile asilimia tano kama ilivyoagizwa.

Dkt. Ntara aliwakubusha wanawake hao kuwa ni vema wanapouungana wakakumbuka kuwa mtaji sio fedha pekee bali ni pamoja na kuwa na elimu ya mradi unataka kuunzisha , kuwa na watu ambao unawalenga katika mradi wao na watakaoshiriki katika mradi huo.

Aidha, Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliwaasa wanawake hao kuunda mtandao wa mawasiliaono kwa Halmashauri zote ili iwe kwao fursa ya kubadilishana uzoefu na kuwa rahisi kupata masoko.

Uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi mkoani Tabora unalenga kusaidia kuongeza uelewa wa wanawake kiuchumi, kibiashara na upatikanaji wa mitaji.

No comments: