Friday, April 28, 2017

Akana kujihusisha na kusafirisha wasichana nchini Kenya kwa ajili ya biashara ya Ngono.


Na Karama Kenyunko

Mshtakiwa Mary Amokowa, ameiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imuachie huru kwani hakuhusika na tuhuma za kusafirisha wasichana 10 kutoka Tanzania Kwenda Kenya kwa ajili ya biashara ya ngono.

Mshtakiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya ameiomba mahakama imuachie huru kwa kuwa madai ya kesi hiyo ni ya uongo na ya kutengenezwa.

Ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godifrey Mwambapa wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi hiyo inayomkabili yeye,Jackline Milinga na Simon Alex Mgawe.

Akiongozwa na wakili wake Nehemia Nkoko,Mary amedai kuwa yeye ni mfanyakazi wa kampuni ya simu ya safari Com iliyopo Nairobi Kenya. Amedai kuwa, Septemba 4,2015 akiwa na rafiki yake Jackline walisafiri kwa kutumia basi la Mordem Coast kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi.

Ameongeza kuwa walikuwa na tiketi na pasi za kusafiria lakini walipofika Namanga mpakani mwa Kenya na Tanzania, akiwa tayari amekwisha gongewa mhuri wa kutoka Tanzania na akiwa katika foreni ya kusubiri kugongewa muhuri wa kuingia Kenya, askari wawili wa Uhamiaji wa Tanzania walimkamata Jackline.

Amedai walipomkamata walimwambia wana wasiwasi na hati yake ya kusafaria kwa sababu alikuwa na hati ya kusafiria ya kidiplomasia na baadaye walibaini haijaghushiwa ni halali.

Amedai kuwa, baada ya pasi ya rafiki yake kuonekana kuwa ni halali na wote wakati huo walikuwa chini ya ulinzi aliomba waachiwe huru, baada ya kutuchukua maelezo lakini hawakutuachia. Badala yake wakatuweka sehemu moja na hao wasichana 10, ambao tulikaa nao siku nne Uhamiaji Makao Makuu na kwamba walipohamishiwa uhamiaji mkoa hawakuwa na hao wasichana.

Ameileza mahakama kuwa hawajui wasichana anaotuhumiwa kuwasafirisha na wala hakuwahi kuwaona hadi siku Zulfa, Lea, Angelina na Amina walipopelekwa mahakamani kutoa ushahidi kwa upande wa mashtaka. “Shtaka hili ni la uongo na la kutengenezwa , sijawahi kusafirisha binadamu yoyote, mimi ni mfanyakazi wa Safari Com naomba mahakama iniachie huru kwa sababu tuhuma ni za uongo.”Mary alisema.

Kwa upande wa mshtakiwa Simon Alex Mgawe alidai kuwa tuhuma hizo si za kweli yeye hajawahi kusafiri nje ya Tanzania wala kukusanya binadamu kwa lengo la kuwasafirisha hivyo aliomba mahakama imuachie huru. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 11, mwaka huu itakapokujwa kwa ajili ya kuwasilisha hoja zao za majumuisho za kuishawishi mahakama iwaone washtakiwa wana hatia ama la.

Awali ilidiwa kuwa,Septemba 4 mwaka 2015, huko Magomeni, washtakiwa waliwaajiri wasichana 10 wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 22 na kuwasafirisha nchini Kenya kwa ajili ya biashara ya Ngono. Wasichana hao ni Najma Suleiman, Leah Mussa, Zulfa Ally, Rahma Mohammed, Salima Komba, Angelina Banzi, Leila Chorobi, Elizabeth Nalimu, Amina Abdi na Sada Hussein.

No comments: