Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema nia ya Uongozi wa Shirikisho la Viwanda Nchini India wa kuonyesha muelekeo wa kutaka kuwekeza miradi yao katika sekta ya Kilimo utaleta matumaini makubwa ya kuimarika kwa Uchumi Visiwani Zanzibar.
Alisema hatua hiyo itafungua milango ya Uwekezaji kwa Taasisi na Makampuni ya Uwekezaji ya Jimbo la Kerala Nchini India kuanzisha miradi yao Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba Utamaduni pamoja na mazingira ya pande hizo mbili yanafanana.
Balozi Seif Ali Iddi akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wawili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mwanzo wa ziara yake ya Wiki Moja Nchini India alitoa Kauli hiyo wakati wa Kikao cha pamoja kati ya ujumbe wake na Uongozi wa Shirikisho la Viwanda Nchini India {CII} hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Crowne Plaza Mjini Kochi katika Jimbo la Kerala.
Aliuomba Uongozi wa Jimbo la Kerala kupitia Shirikisho hilo la Viwanda Nchini India kuanzisha ushirikiano wa pamoja kati yake na Zanzibar hasa kwenye kilimo cha Viungo kwa vile Zanzibar tayari imeshabarikiwa kuwa na rasilmali kubwa ya Mazao yanayotokana na viungo.
Alisema Zanzibar bado inakabiliwa na ukosefu wa Utaalamu wa kutosha katika kuendesha miradi inayotokana na kilimo cha Viungo kiasi kwamba mapato yanayopatikana katika Kilimo hicho hayendi sambamba na nguvu zinazotumika.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Nd. Juma Ali Juma aliueleza Ujumbe huo wa Shirikisho la Viwnada Nchini India kwamba Kilimo badokinategemewa kuwa muhimili wa Uchumi wa Zanzibar kilichoundiwa Sera katika kuona kinamkomboa Mwananchi hasa Mkulima.
Hata hivyo Nd. Juma alisema uzalishaji katika sekta ya kilimo licha ya kwamba ndio tegemezi la kundi kubwa la Wananchi wa Zanzibar unaonekana kupungua kutokana na mabadiliko ya kimazingira. Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na mipango ya kuimarisha Sekta ya Uvuvi katika bahari Kuu ambayo bado haijatumia ipasavyo ili iweze kutoa ajira nyingi zaidi kwa Wazalendo.
Nd. Juma alifafanua kwamba bidhaa zitakazotokana na mazao ya Baharini zinaweza kutoa mchango mkubwa wa chakula katika Sekta ya Utalii na kuipunguzia mzigo Serikali Kuu bidhaa hizo kuagizwa nje ya Nchi jambo ambalo huhitaji gharama kubwa ya Fedha.
Alisisitiza umuhimu wa kutumika kwa Teknolojia ya Kisasa katika uwekezaji unaoendelea kwa sasa utakaokidhi mahitaji halisi kwa vile Zanzibar ina eneo dogo la ardhi. Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ambae pia ni Waziri asiye na Wizara Maalum Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mamboya alisema kundi kubwa la Wanawake na Vijana wanaomaliza masomo yao ya Sekondari bado wanahitaji kuungwa mkono.
Dr. Sira alisema kipato wanachokipata makundi hayo kwa sasa katika baadhi ya kazi wanazizifanya hakijaweza kukidhi mahitaji yao halisi ya kuendesha maisha yao ya kila siku. Alisema uanzishwaji wa Viwanda Vidogo vidogo kwa mchango wa Taasisi na Makampuni ya ndani na nje ya Nchi ndio suluhu pekee itakayoliibuwa na kadhia hiyo kundi hilo ambalo ndilo kubwa katika Jamii.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Ujumbe wa Shirikisho la Viwanda Nchini India {CII} Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Bwana George Paul aliueleza Ujumbe wa Zanzibar kwamba Taasisi zilizo chini ya mwamvuli wa Shirikisho hilo zimepata shauku ya kuangalia namna zinavyoweza kuelekeza nguvu zao za Uwekezaji Visiwani Zanzibar.
Bwana Paul alisema wapo wawakilishi wa kampuni za uwekezaji katika Sekta ya Biashara zinazotarajiwa kushiriki maonyesho ya Biashara Dar es salaam Tanzania ambao wameamua kupanga utaratibu wa kiufika Zanzibar kuangalia mazingira yaliyopo katika sekta ya Uwekezaji Vitega Uchumi.
Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Nchini India wa Pili kutoka Kulia Bwana George Paul akiuelezea Ujumbe wa Zanzibar shauku ya Wawekezaji wa Shirikisho hilo kushawishika kutaka kuangalia fursa za Uwekezaji zilizopo Zanzibar.
Balozi Seif Kushoto akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Nchini India { CII }Bwana George Paul mara baada ya mazungumzo yao ya ushirikiano hapo Hoteli ya Crowne Plaza.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kulia akiuongoza Ujumbe wa Zanzibar katika Mkutano na Uongozi wa Shirikisho la Viwanda Nchini India. Wa kwanza kulia ni Kaimu Balozi wa Tanzania Nchini India Balozi Mohamed Hija, Kulia ya Balozi Seif ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiye na Wizara Maalum Dr. Sira Ubwa Mamboya na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.
Picha na – OMPR – ZNZ.
No comments:
Post a Comment