Na Frank Shija –
MAELEZO, Dar es Salaam.
WAFANYABIASHARA
ndogondogo katika Soko la Machinga Complex Jijini Dar es Salaam wameshauriwa
kubadilika na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria badala ya kufanya
biashara zao kimazoea.
Wito huo umetolewa
leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) George Simbachawene alipofanyaa ziara ya kikazi katika Soko hilo ili
kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa soko hilo.
“Nawapa pole sana
ndugu zangu wafanyabiashara wa Machinga Complex mnaendesha biashara zenu bila
kuzingatia sheria jambo linalo wagharimu hivi sasa katika biashara zenu leo
nimekuja kuwarejesha kwenye mstari,” alisema Simbachawene.
Aidha Waziri
Simbachawene amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuwachukulia hatua
baadhi ya viongozi wa menejimenti ya Machinga Complex kwa kile kinachodaiwa
utendaji wao mbovu na kujaza nadfasi zote zilizo wazi.
Wakati huohuo
amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuteua Wajumbe wa Bodi ya
Machinga Complex ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Soko hilo.
Pia Waziri
Simbachawene ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kulipa kodi zao kwa wakati
huku hakitishia kuwaondoa katika vizimba (eneo la mraba la mauzo) wale wote
watakao kaidi amri hiyo halali ya kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na mikataba
yao.
Awali akimkaribisha
Waziri Simbachawene, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema kuwa
ujio wa Waziri huyo mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa imekuja wakati muafaka
kwani ni takribani kipindi cha karibu mwaka mmoja tangu alipompa maagizo ya
kushughulikia changamoto zinazokabili jengo la Machinga Complex kazi ambayo
waliikamilisha na kukabidhi taarifa katika ofisi ya Waziri Simbachawene.
“Nidhahiri kuwa ziara
yako Mhe. Waziri itatoa majawabu yatakayopelekea kutatua changamoto kadhaa
zinazolikabili soko hili la Machinga Complex na ni imani yangu kwamba utatoa
maagizo na kufanya maamuzi nasi hatuna budi ya kuyapokea na kutekeleza”
alisisitiza Makonda.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Bibi. Sipora Liana amesema kuwa changamoto
kubwa inayokabili Soko hilo ni pamoja na deni linalokadiriwa kufikia zaidi ya
shilingi bilioni 38 zianzodaiwa na Shirika la hifsdhi za Jamii (NSSF) ambao
ndiyo waliojengwa majengo ya soko hilo linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la
Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa
changamoto nyingine inayokabili Soko hilo ni kutokuwapo kwa chombo cha maamuzi
(Bodi) ambayo kazi yake kubwa ingekuwa kushughulikia changamoto zote za mradi
huo.
Soko la Machinga
Complex limejengwa kwa lengo la kutatua changamoto ya ukosekanaji wa soko la
uhakika kwa wafanyabiashara wadogowadogo katika Jiji la Dar es Salaam ambapo
ujenzi wake ulifanyika chini ya udhamini wa NSSF na kumilikiwa na Halmashauri ya
Jiji la Dar es Salaam likiwa na uwezo wa kuchukua takribani wafanyabiashara 4206.
No comments:
Post a Comment