Pikiniki
zinazofanywa na watu mbalimbali katika fukwe zilizoko kwenye ukanda
wa utalii visiwani Zanzibar, zimeelezwa kuwa zinachangia uharibifu mkubwa wa mazingira
unaotishia kuwakimbiza watalii.
Shughuli ya kusafisha mazingira
iliyofanywa juzi katika eneo dogo kwenye ufukwe wa Muyuni ulioko Matemwe mkoa
wa Kaskazini Unguja, ilikusanya karibu tani moja ya takataka zikiwemo chupa za
plastiki.
Operesheni hiyo iliyochukua saa moja,
ilijumuisha wafanyakazi wa Amber Resort na Best of Zanzibar, na kusafisha eneo
linaoandaliwa kwa ajili ya mradi mkubwa wa kitalii utakaofanywa na kampuni ya
Pennyroyal.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo,
Meneja Mradi wa Amber Resort Murtaza Hassanali, alisema vijana wanaotembeza watalii
(mapapasi) pamoja na wageni wanaofika hapo, huondoka wakiacha vitu vingi
visivyofaa ambavyo hugeuka kuwa taka na sumu kwa viumbe wa baharini.
Aidha alieleza kuwa, pikiniki zinazofanywa
na watu kutoka mjini na maeneo mengine hasa vijana, ni chanzo kikuu cha
uharibifu wa fukwe hizo.
"Angalia ufukwe wote umejaa chupa za
plastiki, karatasi za foili, mifuko na viatu visivyofaa na hakuna mtu anayejali
kusafisha. Hii ni hatari sana kwa ustawi wa mazingira ya baharini,"
alisema.
Hata hivyo, alisema kampuni yake
inakusudia kuubadilisha ufukwe huo kwa kusambaza vifaa vya kuwekea taka na
kutoa elimu kwa wakaazi wa kijiji hicho juu ya umuhimu wa usafi wa mazingira.
Aidha alisema kwa kushirikiana na serikali
ya wilaya kupitia ofisi ya halmashauri, wataandaa mabango ya matangazo yanayohimiza
wananchi kuhifadhi fukwe na maeneo yote ya kijiji hicho na kuyaweka katika
sehemu tafauti.
Kwa upande wake, Nahya Khamis Nassor,
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) anayesomea elimu ya afya na
mazingira, alisema inasikitisha kuona fukwe zinazotegemewa kuwa kivutio kwa
watalii, zimekithiri uchafu bila uangalizi.
Alifahamisha kuwa, Kamisheni ya Utalii
Zanzibar inafanya kazi kubwa ya kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini kwa kusambaza
vipeperushi vinavyoonesha uzuri wa mandhari pamoja na taarifa mbalimbali ili
kuwashawishi watalii kuendelea kuja visiwani humu.
Hata hivyo, alisema pale watakapokuja na
kukuta hali ni tafauti, watalii hao watahisi wamedanganywa na huenda wakafikiria
mara mbili kabla hawajaamua kuja tena au hata kuvitangaza visiwa hivi kwa
wananchi wenzao.
"Uchafu huu unaozagaa ufukweni
unaishia baharini kwa kusombwa na maji yanapojaa. Plastiki haziozi na samaki
wanaweza kuzila bila kukusudia na hii ni hatari kwa rasilimali za baharini
kutoweka," alieleza Nahya.
Pamoja na kuwaomba wakaazi wa kijiji hicho
kuzilinda na kuzihifadhi fukwe zao, aliishauri serikali ya wilaya kuunda kanuni
maalumu zitakazosaidia kudhibiti uchafu unaotishia kuwakimbiza watalii.
Alisema itakuwa vyema, kanuni hizo ziweke
adhabu ikiwemo faini kwa mtu yeyote atakaepatikana akichafua mazingira kwa
makusudi kama inavyofanyika katika nchi na miji mingine.
Ofisa mratibu wa kampuni ya Amber Resort
Mohammed Issa Khatib, alisema mpango huo utakuwa endelevu ili kuhakikisha elimu
ya usafi wa mazingira inawafikia wananchi wote kijijini hapo na watu wengine
wanaokitembelea ambao alisema ndio wanaoacha athari kubwa ya uchafu.
Aliwaomba wavuvi na vijana wanaofanya
biashara za kitalii ufukweni waache kutupa taka ovyo, kwani kufanya hivyo
kunachafua mandhari na taswira ya Zanzibar nzima mbele ya macho ya watalii.
No comments:
Post a Comment