Tuesday, March 28, 2017

SERIKALI KUTENGENEZA MWONGOZO WA KUWARUDISHA SHULE WALIOPATA MIMBA


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Serikali imejipanga kutengeneza mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata mimba wakiwa masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi kufikia ngazi za juu.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori alipokuwa akifungua warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia jinsia katika elimu kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Prof. Joyce Ndalichako.

Manori amesema Serikali ya Tanzania inajitahidi kuzingatia jinsia katika utoaji wa elimu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya Msingi na Sekondari uwiano wake ni moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana hupungua kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba hivyo lengo la warsha hiyo ni kuwasaidia wadau kuweka mipango ya elimu inayozingatia usawa wa kijinsia.

“Serikali yetu imejipanga kuhakikisha wasichana wanapata elimu hadi ngazi za juu lakini mpango huo unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba na ndoa za utotoni hivyo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ngazi za juu za elimu tuko kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo kwa ajili ya wanafunzi waliopata mimba wakiwa bado wanasoma kupata nafasi ya kuendelea na masomo,”alisema Manori.

Mkurugenzi Msaidizi amezitaja changamoto zingine zinazowapelekea wanafunzi wa kike kuacha shule zikiwemo za umaskini, mazingira rafiki ya kusomea, mila na desturi zinazomkataza msichana kupata nafasi ya kusoma pamoja na kukosa muda wa kujisomea kwa sababu ya kufanya kazi nyingi wanaporudi majumbani.

Manori ametoa rai kwa Watanzania kuelewa kuwa kila mtoto ana haki na wajibu wa kupata elimu bila kujali jinsia pia ameiasa jamii kuacha kuwaozesha wasichana wenye umri chini ya miaka 18 ili waweze kufikia malengo yao waliyojipangia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha mipango ya elimu nchini inaangalia usawa wa kijinsia kwa kuwa ni njia moja wapo itakayochochea maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.

“Warsha hii imeandaliwa kwa ajili ya wadau wote kutoa mawazo yao juu ya changamoto za usawa wa kijinsia zinazoikumba sekta ya elimu pamoja na kuwapa fursa wadau hao kushauriana kuhusu mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo ili kuinua sekta ya elimu sio tu kwa Tanzania bali kwa Afrika nzima,”alisema Haldorsen.

Haldorsen ameongeza kuwa mfumo wa elimu umetambua uhusiano uliopo kati ya elimu na usawa wa kijinsia ndio maana wadau wa masuala ya elimu wa Serikali kutoka katika baadhi ya nchi za Afrika wameamua kuungana kwa pamoja kujadili juu ya tathmini, mpangilio na ufuatiliaji wa elimu unayozingatia jinsia.

Tanzania imekua nchi ya kwanza kuendesha warsha hiyo ya siku tatu iliyoshirikisha maafisa waandamizi wa Serikali wanaoshughulikia mipango ya elimu kutoka nchi za Mozambique, Zambia, Malawi, Uganda, Zanzibar na Tanzania Bara.

Imeandaliwa kwa ushirikiano wa shirika la Plan International- Tanzania, Global Partnership for Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations Girls’ Education Initiative (UNGEI).
Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori akiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu kutoka shirika la Plan International- Tanzania, Global Partnership for Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations Girls’ Education Initiative (UNGEI) mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen akitoa neno fupi kwa ajili ya kuwakaribisha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha kutengeneza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu. Ufunguzi wa warsha hiyo ulifanyika jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Serikali wanaohusika na elimu kutoka nchi sita za Afrika wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (hayupo pichani), Venance Manori wakati wa ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha maafisa hao katika kutengeneza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu.Warsha hiyo ya siku tatu imefunguliwa jana jijini Dar es Salaam.

…………………

No comments: