Mkoa wa Kigoma umenufaika na nyumba mpya 30 za watumishi wa Afya pamoja na vitendea kazi (baiskeli 200, mabegi 225, mabuti 25 na makoti ya mvua 25) kwa ajili ya wahudumu wa Afya ngazi ya jamii vikiwa na ujumla wa thamani ya Shs 1,806,985,822 billioni kutoka kwa Taasisi ya Benjamin W. Mkapa.
Akizungumza wakati wa ukabidhiwaji wa nyumba na vitendea kazi hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Brigedia Jenerali (Mstaafu) Emmanuel Maganga, alisema ya kuwa mkoa wa Kigoma unakabiliwa na upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia 65 ya mahitaji kamili na moja wapo ya sababu zinazopelekea upungufu huo ni ukosefu wa mahali pazuri pa kuishi.
Hivyo nyumba hizi zilizojengwa na Serikali kwa usimamizi wa Taasisi ya Mkapa zitasaidia kupunguza makali ya uhaba wa watumishi kwa mkoa wa Kigoma na nchi nzima kwa ujumla.
Mkuu wa mkoa aliwasisitizia Wananchi pamoja na watumishi wa afya wanaotumia nyumba hizo kuzitunza na kuzithamini kwani zimejengwa kwa faida yao. Hivyo hivyo kwa upande wa vitendea kazi aliwasisi wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa ambalo ni kuwafikia wana jamii ndani ya jamii zao na kuweza kuwapa huduma bora za afya.
“Napenda kutoa wito kwa mashirika yanayojenga nyumba kama vile shirika la nyumba la Taifa, Mifuko ya hifadhi ya jamii, watumishi ujenzi n.k wafirikie zaidi kujenga kwenye vituo vyetu vya Afya na Zahanati ambapo Serikali inaweza kuwapangishiwa watumishi wake” alisisitiza, Mh. Maganga
Nae mkurugenzi wa halmashuri ya kigoma Bi. Hanji Yusuph alisema, halmashauri ya wilaya ya kigoma pekee ina uhitaji wa nyumba 166 na kufikia siku ya makabidhiano halmashauri ya wilaya ya kigoma ilikuwa na nyumba 56, hivyo kupatiwa nyumba 10 inaongeza na kuwa 66. Bado kuna uhitaji wa nyumba 100.
Nae Dr. Ellen Mkondya-Senkoro, alifafanua kuwa nyumba hizo mpya 30 za wahudumu wa afya na vitendea kazi vya watumishi wa Afya ngazi ya jamii vimetolewa kupitia miradi miwili ya Taasisi ya Benjamin Mkapa ambayo wa kwanza ni mradi wa Uimarishwaji wa Mifumo ya Afya ambao ulifadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) umetekelezwa kwa miaka mitano 2011 hadi 2016.
Mradi huu umekuwa unalenga katika kuimarisha masuala ya raslimali watu wa sekta ya afya. Moja wapo ya majukumu ya Taasisi ya Mkapa tuliyopewa na Wizara ya Afya, ni ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya ambapo jumla ya nyumba 480 zimekuwa zinajengwa katika Halmashauri 51 nchini tokea mwaka 2011.Miongoni mwa nyumba hizo 480, 30 zipo katika Mkoa wa Kigoma kwa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Kasulu na Kibondo.
Mradi wa pili ni wa Kifua Kikuu na Ukimwi unaotekelezwa kwa kushirikiana ya Wizara ya Afya kupitia – Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma pamoja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi inatekeleza mradi wa Ukimwi na Kifua Kikuu chini ya Shirika la Save the Children kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.
Mradi huu unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 3 katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma unalenga kuisaidia Serikali kupunguza maambukizi ya Kifua kikuu kwa 25% na kupunguza vifo vitokanavyo na Kifua Kikuu kwa 50% mpaka kufikia 2020. Pamoja na hayo mradi unalenga kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi, Kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi, kutokomeza unyanyapaaji na kuongeza upatikanaji wa urahisi wa huduma za Ukimwi hasa upimaji wa VVU.
Mfano wa moja kati ya nyumba mpya 30 zilizojengwa na kukabidhiwa kwa mkoa wa kigoma na Taasisi ya Mkapa.
Kikundi cha kina mama wa mkoa wa kigoma wakiimba kwa furaha mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Brigedia Jenerali (Mstaafu) Emmanuel Maganga wakati wa hafla ya kukabidhiwa nyumba mpya 30 za watumishi wa afya zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa mkoani Kigoma.
Watu waliohudhiria hafla ya ukabidhiwaji wa vitendea kazi vitendea kazi (baiskeli 200, mabegi 225, mabuti 25 na makoti ya mvua 25) kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii
Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mkapa akitoa ufafanuzi wa jiwe la ufunguzi kwa Mhe. Brigedia Jenerali (Mstaafu) Emmanuel Maganga, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wakati wa halfa ya ukabidhishwaji wa nyumba mpya 30 za watumishi wa Afya iliyofanyika katika zahanati ya Kalinzi mkoani kigoma.
No comments:
Post a Comment