KAMPUNI za ujenzi nchini zimeshauriwa kuungana na kushirikiana na kampuni za ujenzi kutoka China ili kujifunza namna wanavyofanya kazi kwa ufanisi.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Asasi ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China, Bwana Joseph Kahama alibainisha kuwa kampuni za ujenzi nchini bado zina safari ndefu ya kuongeza ujuzi na mbinu za kibiashara.
“Wachina ndio wanaoongoza katika ujenzi duniani, mataifa mengi yaliyoendelea majengo yao yanasimamiwa na kampuni za kichina, hivyo hakuna namna kwa kampuni za Kitanzania kushindana nazo wakitaka kufanikiwa wajipenyeze na kuomba ushirikiano hapo watajifunza mengi.
“Kujifunza kuna njia nyingi, ni utaratibu mzuri katika biashara kujipanga,” alisisitiza Bw. Kahama na kuongeza: “zaidi ya asilimia 80 ya kampuni kubwa za ujenzi duniani zinatoka China, na hapa nchini zipo nyingi kwa sasa huu ndio wakati wetu wa kuchota ujuzi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC East Africa Limited), Bwana Yigao Jiang alisema kampuni yake imekuwepo nchini tangu miaka ya 1960 na wapo tayari kuwasaidia Watanzania katika nyanja zote ikiwemo masuala ya kijamii.
“Mbali ya kushiriki ujenzi wa magorofa na miundombinu mbalimbali kampuni yetu inaguswa na matatizo ya kijamii kwa sababu Watanzania ni ndugu zetu sasa, tumeshiriki ujenzi wa reli ya Tazara, tumejenga jengo la Ushirika (Mnazi Mmoja), tumejenga jengo la Nasaco (Dar es Salaam).
“Vilevile jengo la ukumbi mpya Ikulu jijini Dar es Salaam tumeshiriki kuujenga na sasa tunajenga makutano ya barabara za juu Ubungo,” alisema.Alibainisha kuwa “Hili linatufanya kuwa sehemu ya jamii, hadi sasa tumeshiriki kutoa misaada mbalimbali ya kuchimba visima vya maji, kugawa vitanda vya wagonjwa katika wilaya mbalimbali za vijijini na hivi karibuni tumegawa jumla ya madawati 150 katika Wilaya ya Chato mkoani Geita na Ruangwa mkoani Lindi yenye jumla ya thamani ya Sh milioni 10, ambapo kila dawati wanakaa wanafunzi watatu.”
Aidha kampuni hii pia ilishiriki kutoa misaada ya blanketi na vyakula kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera yenye thamani ya Sh mil 10.Kuhusu fursa zinazopatikana kutokana na kampuni za ujenzi kutoka China anaeleza Bw. Kahama: “Watanzania wanapata ajira kwa sababu wasimamizi ni Wachina lakini wafanyakazi wanatoka hapahapa, vilevile wananunua mchanga, saruji, kokoto, nondo na vifaa vingine vya ujenzi kutoka nchini.
“Kampuni hii ya CCECC East African Limited ni ya tatu kwa ukubwa duniani, hivyo nasisitiza tusiache kunufaika kutoka kwao wana mengi ya kutufunza kuhusu sekta ya ujenzi.”
Mkuu wa wilaya ya Chato, Bw Elias Makory akimkabidhi cheti Mkurugenzi wa Operesheni wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Bw.An Yi kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo kwa jamii mara baada ya kupokea madawati 50 kwa matumizi ya wanafunzi 150. Kampuni hiyo imeshatoa jumla ya madawati 150 yenye thamani ya milioni 30 na itaendelea kuchangia huduma mbalimbali za kijamiii.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Bw Elias Makory (wapili kushoto) akipokea rasmi madawati 50 toka kwa Mkurugenzi wa Operesheni wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Bw.An Yi (watatu kushoto). Kampuni hiyo imeshatoa jumla ya madawati 150 yenye thamani ya milioni 30 na itaendelea kuchangia huduma mbalimbali za kijamiii.
No comments:
Post a Comment