Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba akiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mambo Nje, Ulinzi na Usalama walipowasili NIDA kutembelea na kukagua maendelea ya mradi wa Vitambulisho vya Taifa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Ndg. Andrew W. Massawe akimpokea Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba(Mb) mara baada ya kuwasili katika ofisi za NIDA makao makuu.
wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mh. Adad Rajab (Mb) wakiwasili katika makao makuu ya ofisi za NIDA.
Kamati ya Kudumu ya Bunge Mambo Nje, Ulinzi na Usalama leo imefanya ziara ya kukagua mradi wa Vitambulisho vya Taifa; ambapo mbali na kupokea taarifa ya utekelezaji pia walitembelea na kukagua kituo kikuu cha Kuhifadhi, kuchakata na kuzalisha Vitambulisho vya Taifa -Data Centre.
Akizungumza wakati wa kukaribisha Kamati hiyo; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema mpaka sasa NIDA imefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kikubwa pamoja na changamoto kubwa ya fedha iliyopo.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo; Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Adad Rajab (Mb) amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na NIDA na kwamba Kamati imeridhishwa na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na NIDA na kwamba Kamati yake itaendelea kuishauri Serikali kuongeza bajeti ya fedha kwa NIDA ili kuwezesha kukamilisha zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa, kwani manufaa ya kuwa na mradi huu kwa Taifa ni makubwa katika Nyanja zote.
Wakitoa maoni yao wajumbe wa Kamati hiyo wameitaka Wizara kuiwezesha NIDA na kuharakisha matumizi ya Vitambulisho vya Taifa kielektroniki kwani tayari idadi kubwa ya wananchi wameshatambuliwa na taarifa zao kuingizwa kwenye mfumo.
“Kutokana na manufaa makubwa ya mradi huu kwa Taifa, Serikali ihakikishe inatumia kila mbinu kuhakikisha matumizi yaliyokusudiwa ya kuwa na Vitambulisho vya Taifa”
Akisoma taarifa yake kwa Kamati hiyo; Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Andrew W. Massawe ameieleza Kamati hiyo mpaka sasa NIDA imekamilisha Usajili wa Watumishi wa Umma nchi nzima ambapo watumishi 500,605 wamesajiliwa, NIDA imeanza kuwasajili wageni wanaoishi kihalali nchini, kufungua ofisi katika Wilaya zote nchini pamoja na kuanza zoezi la kuwasajiliwa wananchi katika mikoa mbalimbali nchini akiitaja baadhi; Lindi, Iringa, Geita, Singida, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Manyara n.k.
No comments:
Post a Comment