Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akitoa taarifa fupi ya utendaji kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.ambayo imeitembelea hospitali hiyo leo. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kingwangallah na Mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Serukamba.
Baadhi ya Wajumbe wa kamati hiyo wakifuatilia ripoti ya utendaji iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Museru.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kingwangallah (kushoto), Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba na Mkurugemzi Mtendaji wa MNH, Profesa Museru wakisiliza maoni ya wajumbe wa kamati hiyo leo.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Dk Faustin Ndugulile akitoa maoni yake baada ya mkurugenzi wa hospitali hiyo kuwasilisha taarifa ya utendaji ya hospitali hiyo kwa wajumbe.
Baadhi ya wakurugenzi, wakuu wa idara wa hospitali hiyo wakifuatilia taarifa ya utendaji ya MNH iliyotolewa leo kwa wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe wa kamati hiyo wakikagua jengo ambalo litatumika kutoa tiba kwa wagonjwa wa figo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Juma Mfinanga akiieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jinsi huduma ya telemedicine inavyofanya kazi baada ya kuunganishwa na hospitali nyingine za mikoa. Kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Serukamba, Mjumbe Joseph Mbilinyi (katikati), Mjumbe Mussa Hassan Zungu na Zitto Kabwe.
………………
Na John Stephen, MNH
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na ubunifu wa kufanya mageuzi makubwa ya kuboresha huduma za afya.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Lucia Mlowe wakati akichangia taarifa ya utendaji iliyowasilishwa kwa kamati hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru.
“Napenda kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa MNH kutokana na ubunifu wenu mkubwa mnaofanya katika kuleta maendeleo ambayo yamelenga kutoa huduma bora. Kutokana na juhudi hizi Serikali inapaswa kutoa fedha ilizoziahidi kwa MNH.
“Nchi nzima inaitegemea MNH, Serikali ione huruma kwa MNH iwapelekee fedha, isiwaache pekee yao,” amesema Mlowe.
Mjumbe wa kamati hiyo msheshimiwa Faustin Mdugulile ameipongeza MNH kutokana na mageuzi makubwa ya kuboresha huduma za afya na ameahidi kuisema MNH bungeni ili serikali kushughulikia changamoto zinazoikabili hospitali hiyo.
Naye Mwekiti wa Kamati hiyo Peter Serukamba ameitaka MNH kuwashirikisha wadau wa afya katika kutoa huduma za afya ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Naishauri serikali iwaachie wadau wa afya kusimamia vifaa tiba zikiwamo mashine za CT-Scan, MRI na vikiwamo vifaa vingine ili kupunguza gharama za uendeshaji. Nchi nyingine za ulaya wanatumia njia hii kuendesha hospitali na lengo ni kupunguza gharama,” amesema Serukamba.
Awali kabla ya wajumbe wa kamati hiyo kuzungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Profesa Museru amesema MHN imeanza ukarabati wa majengo ya kutolea huduma za upasuaji kwa kina mama.
Amesema kutokana na ukarabati huo, vyumba vya upasuaji vimeongezeka kutoka vyumba viwili hadi wanne, kwenye jengo la upasuaji vyumba vimeongezeka kutoka saba hadi vinane na jengo la watoto vyumba viwili hadi hadi vinne.
Profesa Museru amesema katika mwaka wa fedha 2016/17, hospitali inaendelea na mkakati wa kuongeza vitanda vya wagonjwa mahututi kutoka vitanda 17 hadi kufikia vitanda 77.
Amesema kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2016, hospitali imetumia Sh. 59.650 bilioni na kwamba Sh. 24.512 bilioni zilitumika kwa matumizi ya kawaida wakati Sh.29.888 bilioni 29.888 zilitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi.
“Sh. 5.250 bilioni zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikilinganishwa na sh. 51.017 bilioni ambazo zilizotumika katika kipindi cha Julai mpaka Disemba 2015 ambapo sh. 19.222 bilioni zilitumika katika matumizi ya kawaida, sh. 30.703 bilioni zilitumika kulipa mishahara ya wafanyakazi na sh. 1.092 bilioni zilitumika katika shughuli za miradi ya maendeleo,” amesema Profesa Museru.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
No comments:
Post a Comment