Na Ismail Ngayonga, MAELEZO Morogoro
SERIKALI Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya nchini wametakiwa kutangaza mafanikio ya miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongoozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Hayo yamesemwa leo Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa Habari na Maafisa TEHAMA katika mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa na Halmashauri yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Mikoa na Halmashauri zake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa zinazowekwa katika tovuti hizo zinaonyesha mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Ipo miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya umeme vijiji, ambapo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji wa miradi inawafikia wananchi” alisema Dkt. Abbas.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano inayooongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magaufuli ni kuleta matokeo ya haraka kwa wananchi wake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha taarifa mbalimbali za mafaniko katika maeneo yao ya kazi zinatangazwa kwa kuzingatia muda na wakati.
Dkt. Abbas alisema kuwa Serikali ipo mbioni kuanza utaratibu wa kupima utendaji kazi wa Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya ili kuangalia ni kiasi gani wameweza kutangaza mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema utaratibu huo wa upimaji utaweza kuainisha Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Mikoa na Wilaya zinatoa na zisizotoa taarifa zake kwa umma, ambapo taarifa hiyo itaweza kuwasilishwa katika Mamlaka za juu Serikalini kwa ajili ya utekelezaji.
Aidha alisema kwa sasa suala la utoaji wa taarifa kwa umma si suala la utashi badala yake ni matakwa ya kisheria, hivyo Serikali inaandaa barua zitazoelezwa kwa Watendaji wakuu katika mamlaka za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu umuhimu wa utoaji wa taarifa kwa umma.
“Kwa sasa tuna sheria ya huduma za habari na sheria ya haki ya kupata taarifa, ambazo zote zinasisitiza na kutoa maelekezo kwa taasisi zote za umma kutoa taarifa kwa wananchi” alisema Dkt Abbas.
Alisema kuwa ili kutekeleza vyema majukumu yao msingi ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuhakikisha kuwa wanatumia vyema mitandao ya kijamii katika utoaji wa taarifa za Serikali, kwani kwa sasa ulimwengu upo katika mabadiliko makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Wananchi kwa sasa hawasubiri tena kusoma gazeti linalotoka siku ya pili asubuhi au taarifa ya habari katika redio na televisheni, badala yake wengi wao wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kupata taarifa za matukio ya moja kwa moja yanatokea katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni wajibu wetu kutumia mitandao hiyo” alisem Dkt. Abbas.
Mafunzo hayo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yamehusisha Mikoa 5 na halmashauri 33 zilizopo katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Simiyu, Kilimanjaro na Arusha.
No comments:
Post a Comment