WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia Machi mosi, 2017 Serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.
“Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza Pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika. “Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Februari 16, 2017) wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.
Amesema agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji wa Mererani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.
“Tutawakamata wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mererani kuna bangi, kuna mirungi, cocaine na heroine. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa za kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wale waliolegealegea, kisha tuwapime,” alisisitiza.
Akifafanua suala la uwekezaji kwenye eneo la Shambalai kutokana na ujumbe ulioandikwa kwenye mabango, Waziri Mkuu alisema katika eneo hilo zimetengwa ekari 500 kwa ajili ya EPZA ili kujenga miundombinu mbalimbali.
“Hilo eneo ni la uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, masoko na maduka makubwa (malls). Sote tunafahamu kuwa Tanzania hivi sasa inaweka msisitizo juu ya ujenzi wa viwanda. Pale tunataka tuwe na viwanda vya nyama, vya kushona nguo na kuchakata madini ya Tanzanite ili kjongeza thamani,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema kama kuna mtu ana uhakika kuwa nyumba yake bado haijalipwa fidia katika eneo lile, aende akaonane na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Joel Bendera lakini taarifa alizopewa ni kwamba hakuna mtu ambaye hajalipwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaita wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One ili wampatie taarifa juu ya malalamiko yanayotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ikimilikiwa na wazungu kuliko hivi sasa.
“Nikimaliza ziara ya mkoa huu, nataka tarehe 27 Februari, Wakuu wa hii kampuni waje ofisini kwangu na taarifa kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini. Nitawashirikisha na wabunge wenu ili waje waseme kwa nini mzungu ni bora kuliko Mtanzania,” alisema.
“Serikali hii inatarajia kuona Watanzania wakinufaika na rasilmali zao. Haiwezekani tukahimiza uwekezaji wa ndani halafu leo anasifiwa mzungu kuliko mzawa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, FEBRUARI 17, 2017.
No comments:
Post a Comment