MBUNGE
wa Simanjiro, Mheshimiwa James Ole Millya ametoa pongezi kwa viongozi
wa serikali ya awamu ya tano kwa jinsi wanavyojali na kuwahudumia
wananchi.
Ametoa
pongezi hizo jana (Alhamisi, Februari 16, 2017) kwenye mikutano miwili
ya hadhara iliyofanyika Orkesumet na Mererani wilayani Simanjiro,
Manyara, baada ya kupewa nafasi asalimie wananchi kabla Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa hajazungumza na wakazi wa maeneo hayo.
“Serikali
hii ina viongozi wachapakazi akiwemo Waziri Mkuu. Kwa mara ya kwanza
katika jimbo hili, wananchi watapata maji safi kupitia mradi wa maji
kutoka mto Ruvu unaoendelea kujengwa hivi sasa,” alisema kwenye mkutano
wa hadhara wa Orkesumet.
Alitumia
fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu afuatilie suala la ujenzi wa hospitali
ya wilaya kwani sasa hivi wanategemeakituo cha afya na hali ikibadlika
inabidi mgonjwa apeekewe Arusha mjini ambako ni umbali wa km. 150 kutoka
Orkesumet yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.
Pia aliomba ijengwe barabara ya lami ya kuunganisha wilaya hiyo pamoja wilaya jirani za Hai na Kiteto.
Akiwa
Mererani, Bw. Ole Millya aliipongeza Serikali kwa kujenga barabra ya
lami kutoka uwanaja wa ndege wa KIA hadi Mererani. Hata hivyo, aliiomba
serikali iongeze juhudi ili barabara hiyo iweze Mererani na Orkesumet.
Akihibu
hoja hizo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza mbunge huyo kwa
uungwana wake wa kutambua juhudi ambazo Serikali imezifanya kwa wananchi
wa jimbo lake.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara,
aliwaambia wakazi hao kwamba Serikali itaendelea kufanya nao kazi bila
kumbagua mtu yeyote kwa sababu ya itikadi za kisiasa.
“Mmempa
yeye dhamana ya kuwawakilisha kama mbunge wenu lakini dhamana ya
kuongoza nchi mmempa Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa
kuwapigia kura. Kwa hiyo, kazi yetu ni kuwatumikia ili tutatue kero
zinazowakabili wana-Simanjiro,” alisema.
Akizungumzia
sekta ya afya, Waziri Mkuu alisema kituo cha afya cha Orkesumet
kimepokea sh. milioni 49 kati ya sh. milioni 57 zilizoombwa ili
kukiimarisha katika utoaji wa huduma za tiba.
“Tumeshatuma
fedha nyingine sh. milioni 163 kati ya sh. milioni 190 zilizoombwa ili
kununulia dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Pia kun ash, milioni 483
zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya vijijini,” alisema.
“Nia
yetu ni kujenga hospitali kubwa ya wilaya lakini ni lazima tuimarishe
miundombinu ya utoaji tiba ili wananchi wapate huduma stahiki.Ombi la hospitali ya wilaya nimelipokea na nitafuatilia kujua limefikia hatua gani,” alisema.
Kuhusu
ujenzi wa barabara za kuunganisha wilaya, Waziri Mkuu alisema Serikali
itaanza kufanya upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa
barabara ya kutoka Arusha – Kiteto – Kongwa ili ijengwe kwa kiwango cha
lami.
Kuhusu
migogoro ya ardhi iliyotajwa na wananchi kwenye mabango yao, Waziri
Mkuu alimwagiza Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula aende
na mbunge huyo kwenye maeneo yanayolalamikiwa na wananchi ili akabaini
chanzo cha migogoro na aitafutie ufumbuzi.
Kuhusu
umeme, Waziri Mkuu alisema vijiji 18 katika ya 57 vya wilaya
vimeshapatiwa umeme na vilivyoakia vimeshaingizwa kwenye mpango wa
serikali wa kuvipatia umeme vijiji 8,000.
Aliwaonya
wakazi wa Mererani wachukue tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kwani takwimu zinaonyesha kuwa kasi ya maambukizi katika mji huo
iko asilimia 18 kiwango alichosema ni kikubwa kuliko kiwango cha
kitaifa.
No comments:
Post a Comment