Tuesday, February 28, 2017

WAZIRI MKUU ANUSA MADUDU MINADA YA MADINI

 Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akisisitiza jambo katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo ,kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam jana  Februari 27, 2017. 
 Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao alichokiitisha kuhusu masuala ya madini kati yake na viongozi wa Serikali, viongozi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One na baadhi ya wachimbaji wadogo,kwenye makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam jana  Februari 27, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akifafanua jambo katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu kwenye Makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam Februari 27, 2017, kwa ajili ya kujadili masuala ya madini. Watatu kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na  ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Bendera.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Amuagiza Kamishna wa Madini aende Mererani
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema anafuatilia kwa makini minada ya madini inayofanyika nchini kwa sababu anazo taarifa za kukiukwa utaratibu kwenye minada hiyo.

Amesema ukiukwaji huo unachangia kutobadilika kwa mapato ya mauzo yatokanayo na mnada hata kama kuna vito viliyokakatwa au havijakatwa.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Februari 27, 2017) wakati akihitimisha kikao alichokiitisha kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam kilichojumuisha Mawaziri wa Fedha pamoja na Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara na watendaji wake, Mbunge wa Simanjiro, wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One, watumishi waliofukuzwa kazi na wachimbaji wadogo. 

Alisema licha ya kuwa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT) kinasifiwa kwa kuongeza mapato ya madini, bado kuna kazi ya ziada inabidi ifanyike kwenye minada hiyo ili Serikali iweze kunufainika na madini hayo.

“Uzoefu wa kwenye minada ya korosho unaonyesha kuwa wanaushirika ndiyo wanaiba fedha za wakulima. Nimekuwa ninafuatilia kwa muda sasa uendeshaji wa hii minada na sijaridhishwa na uendeshaji wake. Hakuna tofauti ya bei madini ya Tanzanite yanapokuwa yamekatwa au la,” alisema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa madini na vito, inapotokea kuna madini yamekatwa bei inapaswa kuwa juu ikilinganishwa na madini ghafi yanapouzwa moja kwa moja.

Amemuagiza Kaimu Kamishna wa Madini, Bw. Benjamini Mchwampaka (ambaye alihudhuria kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Madini) aende Mererani na kufuatilia utendaji kazi wa mgodi wa Tanzanite One na suala zima la teknolojia zinazotumika kiwandani hapo.

Waziri mkuu aliitisha kikao hicho kufuatia ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mererani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara Februari 16, 2017 kwamba akimaliza ziara ya mkoa huo ataitisha kikao na wawekezaji wa Tanzanite One baada ya kupokea malalamiko kwamba hali ya watumishi ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ilipokuwa inamilikiwa na wazungu kuliko ilivyo hivi sasa.

Ili kuhakikisha ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini unaongezeka, Waziri Mkuu amemwagiza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aimarishe ukaguzi kwenye viwanja wa ndege vya Arusha na Kilimanjaro (KIA),

“Kamishna wa TRA na watu wako inabidi mjipange kwa sababu kuna njia nyingi za ukwepaji kodi zinafanyika kwenye sekta ya madini wakiwemo hata hawa wachimbaji wadogo. Simamieni utaratibu wa kufuatilia kodi, nendeni kule walipo, msisubiri waje kuwaletea malipo ofisini. Wasipokuja je? Au wakija wakakuta mmetoka ofisini je?” Alihoji Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu uelewa wa sheria miongoni mwa wachimbaji wadogo, Waziri Mkuu alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa Kamishna wa Madini wanapaswa kutoa elimu na uelewa wa kisheria kwa wachimbaji hao ili kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza kwenye maeneo mengi nchini.

“STAMICO na Kamishna wa Madini fanyeni kazi pamoja, waelewesheni wachimbaji wadogo kuwa uwepo wa vitalu maana yake kuna mipaka ambayo pia inajumisha utoaji wa leseni kwa wenye vitalu hivyo. Kwa hiyo, waelimisheni kuwa mtu hapaswi kwenda upande wa pili wa mtu mwenye leseni, akifanya hivyo atakuwa anavunja sheria.” 

“Ninyi ni wadau wakubwa wa sekta hii kwa hiyo mnapaswa kushiriki katika zoezi la kutoa elimu. Mnayo maeneo mengi ya uchimbaji lakini yana migogoro, mfano ni kule Ngaka na Kiwira. Maeneo yote haya yanahitaji usimamizi mzuri. Mnayo Bodi, Mwenyekiti yupo kwa hiyo mnatosha kuifanya kazi hii,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One waboreshe mahusiano yao na vijiji vilivyo jirani na mgodi huo. “Kuweni karibu na wananchi ili wajue umuhimu wenu na uwepo wenu na waweze kusaidia kulinda mali zenu. Shirikianeni na Halmashauri na Baraza la Madiwani, tangazeni kazi zenu za CSR ili wananchi wajue mmechangia nini katika kusaidia maendeleo yao,” alisema.

Kuhusu suala la watumishi waliofukuzwa kazi kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu (OWM-Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Erick Shitindi asimamie suala lao na kuwapatia majibu kuhusu hatma ya suala hilo.



Watumishi hao walikuwa wanawakilisha wenzao 201 ambao walifukuzwa kazi Februari 8, 2016 kwa sababu ya kufuatilia maslahi yao vikiwemo malipo ya saa za kazi za ziada (overtime), mishahara ya miezi miwili, malipo ya NSSF, vitendea kazi na usalama wa kazi migodini.

No comments: