Teresia Mhagama na Zuena Msuya,
Arusha
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na
Mbunge wa Simanjiro, James Millya wametembelea Kituo cha Jimolojia Arusha,
unapofanyika Mnada wa Pili wa Kimataifa kwa madini ya Tanzanite ili kujionea
jinsi mnada husika unavyoendeshwa.
Mnada huo wa kimataifa
unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 9 hadi 12, Februari, 2017 unahudhuriwa
na wanunuzi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na wauzaji kutoka ndani ya
nchi.
Akitoa maelezo kuhusu mnada huo, Mkurugenzi wa Kitengo cha
Uthaminishaji Madini katika Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard
Kalugendo, alisema kuwa lengo la mnada huo ni kuhakikisha kuwa madini ya
Tanzanite yanapata soko rasmi na Serikali kupata mapato yake stahiki.
Alisema kuwa minada ya madini
inayofanyika ndani ya nchi inasaidia pia kudhibiti utoroshaji wa madini hayo
nje ya nchi kwani wauzaji wa madini hayo wanakuwa na uhakika wa kupata wanunuzi
wa Tanzanite wanaohudhuria minada hiyo.
“Hapa tumekaribisha wanunuzi kutoka sehemu mbalimbali duniani na
sisi kama Serikali tunasaidia kutathmini madini yaliyoletwa na wauzaji wa ndani
ya nchi kwa kuangalia bei katika masoko mengine nje ya nchi na kutoa muongozo
wa bei za madini husika ambayo itamsaidia mchimbaji katika kufanya mauzo,”
alisema Kalugendo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, baada ya kukagua mnada huo, aliishukuru Wizara ya Nishati na Madini kwa
kuendesha mnada husika jijini Arusha na kusema kuwa hii itasaidia kuitangazia
dunia kuwa madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee na Serikali itaongeza
mapato kupitia madini hayo.
Alitoa wito kwa
wafanyabiasharawa madini ya Tanzanite kuweza kupeleka madini mengi zaidi katika
mnada huo ili kuweza kuwa na wadau wengi zaidi na madini hayo yatanunuliwa kwa uwazi ambao utaleta
faida kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.
Wajumbe wa Kamati, Mkuu wa Mkoa
na Mbunge wa Simanjiro pia walipata fursa ya kuona shughuli mbalimbali
zinazofanyika katika Kituo cha Jimolojia ikiwemo za kuchonga vinyago
vinavyotokana na miamba mbalimbali na kuweka katika maumbo mbalimbali na pia
kukata madini ya vito na kuyaweka katika maumbo ya kuvutia.
Mnada wa kwanza wa madini ya
Tanzanite ulifanyika mwezi Agosti mwaka 2016 ambapo jumla ya gramu 318,033.17
na karati 3,274.70 za Tanzanite ziliuzwa na jumla ya kampuni 43 kutoka mataifa
mbalimbali duniani zilihudhuria.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini waliotembelea mnada huo ni pamoja na Mhe. John Heche,
Mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA), Mhe. Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum
(CCM), Mhe. Mwantakaje Juma Mbunge wa Bububu (CCM) na Mhe. Dunstan Kitandula Mbunge wa Mkinga (CCM).
No comments:
Post a Comment