Thursday, February 9, 2017

SERIKALI YA UHOLANZI YAAGIZA AINA 14 ZA MBEGU ZA VIAZI NCHINI

SERIKALI ya Uholanzi imeingiza nchini aina 14 ya mbegu za viazi kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuboresha maisha ya wakulima kupitia mradi wa kuboresha zao la viazi nchini.

Akizungumza katika kikao cha ufunguzi wa mradi huo kilichofanyika mkoani Morogoro katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) jana, Mshauri wa Kilimo wa Ubalozi kwa nchi za Kenya na Tanzania, Bw. Bert Rikken alisema nchi yake imeona Tanzania ina nafasi kubwa ya kuongoza uzalishaji wa viazi kutokana na ukubwa wa ardhi na hali ya hewa.

Bw. Rikken alibainisha wameamua kuingiza mbegu hizo ili kuongeza uzalishaji kwa sababu wakulima wanazalisha chini ya tani nane hadi 10 kwa hekta, hivyo ujio wa mbegu hizi utasaidia kuongeza uzalishaji na kufikia tani 40 kwa hekta.

“Mbegu hizi ni nzuri kwa matumizi mengi, viazi vyake vina ladha nzuri na vinaweza kutumika kutengeneza chips au bidhaa nyingine zitokanazo na viazi ambazo zinaweza kusafirishwa nje ya nchi. Mradi huu ulianza kwa kutiliana saini mawaziri wa kilimo kutoka Tanzania na Uholanzi mwaka 2016 ili kuruhusu mbegu kuingia nchini ili kupata ithibati,” alisema Rikken.

Mradi huo wa miaka mitatu utakaogharimu kiasi cha Euro 388,000 sawa na Sh milioni 700, utahakikisha Tanzania inapata mbegu mpya za zao hilo na kutoa mafunzo kwa taasisi zinazojihusisha na kilimo nchini ili kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake Kaimu Mthibiti Mkuu wa Mbegu kutoka Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), Dkt. George Swella kazi yao kubwa ni kuhakikisha mradi unafanikiwa kwa kusimamia mchakato wa kupima mbegu zilizoingizwa nchini kutoka Uholanzi ili kujua kama zinaendana na mazingira ya Tanzania.

“Awali tulipokea mbegu tatu ambazo zilipitia mchakato mzima wa maabara hadi shambani, majibu ni mazuri na sasa zimeshasambazwa kwa wakulima tunasubiri uzalishaji. Mbegu hizo majina yake ni Jelly, Rumba na Sagitta. Baada ya matokeo hayo tumeletewa mbegu nyingine 11 ambazo bado zipo kwenye mchakato, jumla inakua mbegu 14 kutoka Uholanzi,” alisema Dkt. Swella.
Akizungumzia faida za ujio wa mbegu hizo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Twahir Nzallawahe alisema kwa sasa Tanzania imekua na matumizi makubwa ya viazi hasa kwa Chips, hivyo haja ya kuongeza uzalishaji ni wazo muafaka kwa kipindi hiki.

“Viazi mviringo ni zao muhimu kwa uchumi na mustakabali wa usalama wa chakula nchini, mchango wa viazi mviringo kwa Watanzania wa Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini ni mkubwa hasa katika mnyororo wa kuongeza thamani kwa sababu mahitaji ya zao hili ni makubwa kutokana na ongezeko la walaji wa chips mayai na chips kuku.

“Tumeona ipo haja ya kuwekeza kwenye ulimaji na utayarishaji wa zao hilo ili kuongeza wingi na ubora, mwanzo wa zao lolote ili uongeze wingi na ubora kwa haraka tunaanza na mbegu. Kwa hiyo huu mradi mzima ambao leo tunauzindua unaangalia uwezekano wa kuingiza mbegu kutoka Uholanzi, wenzetu wamepiga hatua katika kilimo cha vaizi mviringo na hasa ni wasafirishaji wakubwa wa mbegu za viazi duniani,” alisema Nzallawahe na kuongeza:

“Uzalishaji ukiwa mkubwa maana yake tunakaribisha wawekezaji zaidi kutoka nje, mfano mdogo mgahawa wa Mc Donald hauwezi kuwekeza katika nchi isiyokuwa na uhakika wa upatikanaji wa viazi bora, hivyo hatuna sababu ya hoteli kubwa kuendelea kuagiza viazi kutoka nje ikiwa uwezo wa kuzalisha zao hilo kwa wingi na ubora wa hali ya juu tunao.”

Kwa upande wake Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Jennifer Baarn aliwahakikisha wajumbe waliohudhuria mkutano huo wanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha mradi unafanikiwa.

“Tumevutiwa na mradi huu na upo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha unafanikiwa, bila kuchelewa tutaitisha kikao cha wadau wa kilimo kujadiliana kuhusiana na viazi lakini pia tutawasiliana na taasisi za kifedha ili kutafuta namna ya kuwawezesha wakulima wadogo kupata mitaji ya kulima viazi,” alisema Jennifer.

Kwa muda mrefu wakulima wa viazi nchini wamekuwa wakitegemea mbegu zilizoandaliwa kienyeji hadi ilipofika mwaka 2013 Serikali ya Finland ilipofanikiwa kuingiza aina nne ya mbegu ambazo ni Asante, Sherehekea, Tengeru na Meru.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Bw.Geoffrey Kirenga  akisisitiza  jambo wakati wa warsha ya siku moja juu ya zao la viazi nchini na namna ya kuliongezea thamani. Kushoto ni Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Bi. Jennifer Baarn, wapili kushoto ni Mshauri Mwandamizi wa Kimataifa  wa maswala ya Mbegu toka Uholanzi,Bw.Jos van Meggelen na kulia ni Kaimu Mthibiti Mkuu wa Mbegu toka Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu nchini(TOSCI),Dr.George Swella. Warsha hiyo iliwakutanisha wadau wa kilimo cha viazi toka Tanzania na Serikali ya Uholanzi.
 Baadhi ya washiriki waWarsha  iliyowakutanisha wadau wa kilimo cha viazi toka Tanzania na Serikali ya Uholanzi wakifurahi kwa kushikana mikono kuashiria ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika kukuza na kuliongezea thamani zao la viazi nchini. Warsha hiyo ilifanyika Mkoani Morogoro katika ukumbi wa Taasisi ya Uthibiti wa Mbegu Nchini(TOSCI).
 Afisa kilimo toka ubalozi wa Uholanzi Nchini,Bi.Theresia Mcha(kulia) akijadiliana jambo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Bw.Geoffrey Kirenga mara baada ya kumaliza warsha ya siku moja juu ya zao la viazi nchini na namna ya kuliongezea thamani. Kushoto ni Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Bi.Jennifer Baarn na wapili kushoto ni Mkuu wa maendeleo ya kongani toka SAGCOT, Bi. Maria Ijumba. Warsha hiyo iliwakutanisha wadau wa kilimo cha viazi toka Tanzania na Serikali ya Uholanzi.

Baadhi ya washiriki wa Warsha iliyowakutanisha wadau wa kilimo cha viazi toka Tanzania na Serikali ya Uholanzi wakiwa katika picha ya pamoja. Walijadili pia namna ya kukuza na kuliongezea thamani zao la viazi nchini. Warsha hiyo ilifanyika Mkoani Morogoro katika ukumbi wa Taasisi ya Uthibiti wa Mbegu Nchini(TOSCI).

No comments: