Thursday, February 9, 2017

BAADA YA KUSOTA NDANI SIKU 7 WEMA ATOKA KWA DHAMANA

Wema Sepetu akishuka katika gari ya Polisi huku pembeni Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lisu akipunga mkono akitokea katika gari hiyo kwa mbele.

Na Karama Kenyunko,Globu ya Jamii.

Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu imewaachia kwa dhamana msanii maarufu nchini Wema Sepetu na wenzake wawili baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambaye kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni tano.

Baada ya kutimiza masharti hayo, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Thomas Simba aliwataka washitakiwa kuhakikisha hawaruki dhamana waliyotakiwa na kuhakikisha wanafika mahakamani hapo kila wanapohitajika.

Hata hivyo, aliwataka mawakili wa serikali kukamilisha upelelezi haraka ili kesi hiyo ifike mwisho. Mbali na wema washtakiwa wengine ni Angelina Msigwa ambaye ni mfanyakazi wa ndani na Matrida selemani Abas ambaye ni Mkulima.

Wote watatu wanashtakiwa na kosa la kukutwa na kiasi kidogo cha madawa ya kulevya chini ya kifungu cha sheria namba 17 (1)(b) cha sheria inayodhibiti matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, iwapo Wema na wenzake watapatikana na hatia basi watatakiwa kulipa faini isiyozidi sh.laki tano au kwenda jela.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa serikali Nassoro Katuga aliyekuwa akisaidiana na Wakili Pamela Shinyambala walidai kuwa Wema na wenzake watatu walitenda kosa hilo tarehe 4 February mwaka huu, huko nyumbani kwao Kunduchi Ununio.

Ilidaiwa kuwa, siku hiyo walikutwa wakiwa na msokoto mmoja pamoja na vipisi viwili vya banfi vyenye gramu 1.80. Hata hivyo washtakiwa wote wamekana mashtaka.

Akielezea hali ya upelelezi wakili Katuga alidai "mheshimiwa Hakimu, upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika tunasubiri taarifa kutoka kwa Mkemia Mkuu ambayo tunategemea kuipata hivi karibuni".

Hakimu Simba aliwapa washtakiwa masharti ya dhamana ambapo mahakama ilimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakao weka dhamana na milioni tano. Mshtakiwa Wema na Wenzake walitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo February 22 mwaka huu.

Nje ya Mahakama Umati wa watu na wasanii mbali mbali walijaa nje kumlaki Wema akitoka mahakamani baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Wema Sepetu akitolewa kutoka mahabusu ya Hakimu Mkazi Kisutu
Wema Sepetu akishuka katika ngazi za Mahakama ya Hakimu mkazi kisutu mara baada ya kuamuriwa apte dhamana ya mahakama.
Weme sepetu akipanda kwenda kusaini hati ya Dhamana kwa hakimu mkazi wa Mahakama ya Kisutu
Wema akishuka katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu 
Wema Sepetu akiwa nje na kwa dhama akiwa ameongozana na wakili 
Wema akirudi mahabusu ya hakimu mkazi kisutu akiwa chini ya ulinzi
Meneja wa Wema, Martin Kadinda  akitoka mahakamani
Baadhi ya wasanii waliofika mahakamani hapo
Mama wema akiwa naingia mahakamani

No comments: