Thursday, February 16, 2017

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KUIMARISHA SEKTA YA UVUVI

 Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uvuvi kutoka Nchini China Bwana Lan Ping Yong kushoto akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi azma ya Kampuni hiyo kutaka kuwekeza mradi wa Uuvi Visiwani Zanzibar. Viongozi hao walikutana katika Ofisi ya Balozi Seif iliyomo ndani ya jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana J.C Barupal kwenye Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni. 



Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuimarisha Sekta ya Uvuvi katika azma yake ya kujenga uchumi imara unaojitegemea utakaostawisha maisha ya Wananchi wake.

Alisema uimarishaji huo utaelekezwa zaidi katika ujenzi wa Viwanda Vidogo vidogovya usindikaji wa mazao ya Baharini utakaotoa fursa ya kukaribisha Makampuni na Taasisi za Kimataifa kuwekeza miradi yao Visiwani Zanzibar. 

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya Uvuvi ya Hong Dong kutoka Nchini China ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Bwana Lan Ping Yong hapo Ofisini kwake Majengo ya Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. 

Alisema Sekta ya Uvuvi bado ina rasilmali ya kutosha inayoweza kusaidia uchumi wa Taifa unaokwenda sambamba na fursa za upatikanaji wa ajira zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya Wananchi walio wengi Nchini. 

“ Hii ni njia bora na mwafaka ya upatikanaji wa ajira hasa kwa Vijana ”. Alisema Balozi Seif Ali Iddi. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza ujumbe wa Viongozi wa Kampuni hiyo ya Hong Dong ambao amewahi kukutana nao wakati wa ziara yake ya Kiserikali ya hivi karibuni Nchini China kwamba juhudi zitafanywa na Serikali katika kuona azma ya Kampuni hiyo ya kutaka kuwekeza Zanzibar inafanikiwa. 

Balozi Seif alimuahidi Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Hong Dong na Ujumbe wake kuwa pande zinazohusika nchini zitakutana na kuangalia wazo la Kampuni hiyo la uwekezaji kwa lengo la kuchukuliwa hatua za muelekeo wa uanzishwaji wa uwekezaji huo. 

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uvuvi ya Hong Dong ya Nchini China Bwana Lan Ping Yong alisema mradi wa Uvuvi unaotaka kuwekezwa Visiwani Zanzibar utakuwa na uwezo wa kutoa fursa za ajira zisizopungua elfu 1,700. 

Bwana Ping alisema licha ya nafasi za ajira zikilengwa kwa Wazalendo lakini pia utaambatana na wataalamu wa Kampuni ya Hong Dong kutoa mafunzo ya Uvuvi kwa Wavuvi wa Kienyeji ili waendeshe miradi yao katika Mfumo wa Kisasa unaokubalika Kimataifa. 

Bwana Ping alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyokwisha patikana katika Nchi ya Mauritania iliyoko Magharibi ya Bara la Afrika baada ya Kampuni hiyo kuwekeza Mradi wa Uvuvi Nchini humo. 

Alisema mapato ya Wavuvi wadogo wadogo wa Nchi hiyo waliobahatika kuwemo kwenye mradi huo kwa sasa yameongezeka na kuleta ustawi wa familia zao na Taifa lao kwa ujumla. 

Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Hong Dong alisema Taasisi hiyo imetenga nafasi Tatu kwa ajili ya Watendaji wa Sekta ya Uvuvi Zanzibar kwenda Nchini Mauritania kujifunza hatua iliyofikia ya Uwekezaji wa Kampuni hiyo katika Nyanja ya Uvuvi. 

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana J. C. Barupal Ofisini kwake katika Majengo ya Baraza la Wawakilishi Mbweni Wilaya ya Magharibi “B”. 

Katika mazungumzo yao Balozi Seif alisema Nchi ya India iliyopo Bara ya Asia imeshapiga hatua kubwa katika masuala ya Teknolojia ya kisasa ambayo Zanzibar kama Nchi inayoendelea inaweza kujifunza kwa kina Taaluma hiyo kutoka kwa Walaalamu wa India. 

Balozi Seif alimueleza Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar kwamba Makampuni ya India yana uwezo wa kuanzisha miradi yao katika sekta za Kilimo, Biashara na Viwanda Visiwani Zanzibar ili kuitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukaribisha Vitega uchumi vya miradi tofauti Nchini. 

Naye kwa upande wake Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Bwana J.C. Barupal alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba India itaendelea kuunga mkono harakati za maendeleo ya Zanzibar. 

Bwana Barupal alisema uungaji mkono huo umekuja kufuatia mafungamano ya muda mrefu yaliyopo ya Ushirikiano wa Kihistoaria kati ya pande hizo mbili hasa katika masuala ya Kibiashara yaliyotoa fursa kwa wafanyabaishara wa India kuingiza bidhaa zao Visiwani Zanzibar karne nyingi zilizopita nyuma. 


Othman Khamis Ame 

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

No comments: