Thursday, February 16, 2017

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA WATENDAJI WA MANISPAA YA WILAYA YA ILEMELA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia Watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ilemela jijini Mwanza. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe. Angelina Mabula (kulia) wakati wa mkutano wa Makamu wa Rais na Watendaji  wa Halmashauri ya wilaya ya Ilemela jijini Mwanza. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella akihutubia mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wa watendaji na Halmashauri ya wilaya ya Ilemela jijini Mwanza (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Picha ya pamoja

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameunga mkono jitihada za kupambana na dawa za kulevya nchini kama hatua ya kuliokoa na taifa janga hilo ambalo limesababisha madhara makubwa katika jamii.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Makamu wa Rais amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yatakuwa ni endelevu lengo likiwa kukomesha kabisa uuzaji,usambazaji na utumiaji wa dawa hizo kama hatua ya kuokoa kizazi cha sasa na kijacho nchini.

Amesema kamwe serikali ya wamu ya Tano hatarudi nyuma katika vita dhidi ya dawa za kulenya na ameomba wananchi waendelee kutoa taarifa za siri kwa vyombo vya dola zitakazosaidia kuwabaini watu wanajihusisha na biashara hiyo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kuhusu tatizo la uvuvi haramu, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa mikoa ya kanda ya Ziwa wakiwemo viongozi wa Mwanza na mikoa mingine nchini kuanzisha mara moja oparesheni kali ya kupambana na wavuvi haramu katika Ziwa Victoria ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika Ziwa hilo.

“Viwanda vya samaki kwa sasa havipati samaki wa kutosha hali ambayo imezorotesha shughuli za kuchakata samaki hivyo nawaagiza viongozi wote kupambana ipasavyo na wavuvi haramu na kamwe wasionewe huruma” amesisitiza Makamu wa Rais.

Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini ni muhimu yakaenda pamoja na oparesheni ya kukomesha uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini.

Amesema wavuvi haramu wamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika maziwa mbalimbali nchini kwa sababu wanatumia nyavu haramu ambazo zinaharibu mazalia ya samaki hivyo ni lazima hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao ili kukomesha kabisa tatizo hilo.

Wakati huo huo halmashauri ya wilaya ya Ilemela, imetekeleza maagizo  14 yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mwaka jana alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo likiwemo suala la watumishi wa halmashauri kukaa karibu na maeneo ya ofisi ambapo mpaka sasa wakuu wa idara 23 wanaishi ndani ya wilaya ya Ilemela ikilinganishwa na hapo awali ambapo watumishi hao walikuwa wanakaa nje ya wilaya hiyo hali ambayo inatajwa ilichangia kuzorotesha utendaji kazi kwenye halmashauri hiyo.

Kufutia hali hiyo, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mlezi wa halmashauri hiyo amepongeza viongozi wa wilaya hiyo pamoja na watendaji wa halmashauri kwa kutekeleza maagiza yake kwa haraka na kwa wakati.

Amesema yeye kama mlezi wa halmashauri hiyo atahakikisha halmashauri inafanya kazi kwa ubora wa hali ya juu katika utoaji wa huduma za uhakika kwa wananchi na kuondoa haraka changamoto mbalimbali zizowakabili wananchi hao ikiwemo uimarishaji wa miundombinu ya barabara

No comments: