Thursday, February 16, 2017

PROF. MBARAWA: UWANJA WA NDEGE WA MTWARA UJENZI MWEZI JULAI

Serikali imesema  ina mpango wa kukarabati uwanja wa ndege wa  Mtwara  ifikapo mwezi Julai mwaka huu ili kuruhusu ndege kubwa kuweza kutua uwanjani hapo na hivyo kufungua fursa za kiuchumi mkoani humo.

Akizungumza mara baada ya kukagua uwanja huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa ukarabati huo utahusisha njia ya kuruka na kutua ndege, maeneo ya maegesho pamoja na barabara yenye urefu wa km 1.5 inayoingia katika uwanja huo.

"Tunategemea mwisho wa mwezi huu kutangaza zabuni ya ukarabati wa uwanja huu, matumaini yetu tutampata mkandarasi mzuri kwa ajili ya kazi hii", amesema Waziri Mbarawa.Aidha, Profesa Mbarawa amefafanua kuwa Serikali itahakikisha kuwa  inajenga uzio katika uwanja huo ili kuhakikisha usalama wa uhakika uwanjani hapo.

Sambamba na hilo, Waziri Mbarawa ametanabaisha kuwa Serikali ina mpango wa ununuzi wa rada nne  mpya kubwa na za kisasa ili kubaini taarifa za ndege  nchini tangu zinapoanza kuruka hadi kutua.
“Tukiwa na rada kubwa na za kisasa zitatusaidia kubaini ndege zote hata ndogo zinazoingia katika maeneo ya viwanja vya madini kwa lengo la kuona ndege hizi zinaingia na zinatoka na nini?”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
 Kuhusu ujio wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Bombadier Q 400, Waziri huyo amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda,  kuwa Serikali inatarajia kuanzisha safari zake kutoka Dar- Mtwara na Songea hivi karibuni.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, amemuomba Waziri huyo kuharakisha ujio wa ndege hizo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Mtwara na kuchochea fursa za kibiashara katika Mkoa huo na mikoa ya jirani.

Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania(TAA) mkoa wa Mtwara, Bi. Zitta Majinge, amesema kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa uboreshaji wa miundombinu ya viwanja hivyo inafanyika kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya wasafiri wa anga.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amekagua maendeleo ya Kivuko cha MV Kilambo kinachotoa huduma kati ya Kilambo na Namoto nchini Msumbiji na kuhakikisha kuwa kivuko hicho kinafanya kazi katika vipindi vyote vya mwaka.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mtwara ambapo ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara yake.



Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Serikalini Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akipata taarifa ya maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Mtwara kutoka kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoani humo, Bi. Zitta Majinge (kulia), mara baada ya kuwasili leo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia), akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoa wa Mtwara, Bi. Zitta Majinge (wa pili kulia), kuhusu ukarabati wa uwanja huo mara baada ya kuwasili leo mkoani hapo. Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda.
 Muonekano wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara ambalo lina uwezo wa kubeba abiria 100 kwa wakati mmoja.
 Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoa wa Mtwara, Bi. Zitta Majinge (katikati), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), mipaka ya Uwanja wa Ndege huo ambao unahitajika kuwekwa uzio ili kulinda usalama wa uwanja.
 Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara yenye urefu wa mita 2258 na upana wa mita 30.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akifafanua jambo kwa Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) mkoa wa Mtwara Emmanuel Wanje, wakati alipokagua Uwanja wa Ndege wa Mtwara leo.

No comments: