Monday, February 13, 2017

Darakuta kuingiza Megawati 1.3 kwenye Gridi ya Taifa

Na Greyson Mwase, Manyara.

Imeelezwa kuwa kampuni ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji (Darakuta Hydro Power Project) iliyopo Babati mkoani Manyara inatarajia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Kilowati 370 hadi Megawati 1.3 zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa na kupunguza upungufu wa umeme nchini ifikapo mwaka 2021.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Raphael Bapsl wilayani Babati mkoani Manyara wakati wa ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika wilaya hiyo, yenye lengo la kuangalia maendeleo ya miradi ya uzalishaji umeme na kubaini changamoto zake.

Akielezea historia ya mradi huo, Bapsl alisema kampuni yake ilianza kuzalisha umeme wa Kilowati 50 mwaka 1995 na kuongeza kuwa Aprili mwaka 2016 kampuni ilianza kuliuzia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) umeme unaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Alisema mbali na umeme huo kutumika kwa matumizi ya nyumbani ambao ni kidogo hususan katika shughuli za kilimo na ufugaji ili kujiongezea kipato, kampuni yake huuza umeme wa ziada kwa TANESCO ili kuongeza kiasi cha umeme katika wilaya ya Babati.

Alisisitiza kuwa ili Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kupitia uwekezaji kwenye viwanda, nishati ya umeme wa uhakika inahitajika na kuendelea kusema kuwa kwa kutambua hilo kampuni yake imeweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili kuhakikisha inachangia katika ongezeko la umeme katika Gridi ya Taifa.
Mtaalam wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Emillian Nyanda (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Maji ya Darakuta, Raphael Bapsl mara baada ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini kuwasili wilayani humo kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya umeme.
Sehemu ya kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji cha Darakuta kilichopo wilayani Babati mkoani Manyara.
Mtaalam wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Emillian Nyanda ( wa pili kutoka kulia) na Thomas Ndazi ( wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa kampuni ya Darakuta mara baada ya kumalizika kwa ziara katika kampuni hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Maji ya Darakuta, Raphael Bapsl (katikati) akionesha moja ya chanzo cha maji kinachotumika katika kuzalisha umeme.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Maji ya Darakuta, Raphael Bapsl (kushoto) akielezea mitambo ya kuzalisha umeme inavyofanya kazi katika kituo hicho kwa Mtaalam wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Emillian Nyanda (kulia).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Maji ya Darakuta, Raphael Bapsl (katikati) akionesha mfumo wa kuongozea mitambo ya kuzalisha umeme ya kituo hicho.

No comments: