Na Lilian Lundo – Maelezo
ASKOFU wa Good News for All Ministry Dkt. Charles Gadi kwa niaba ya dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini wamempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Kamishna wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Dkt. Gadi ametoa pongezi hizo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO).
“Tunamshukuru Mungu kwa kumuinua Rais ambaye ameonyesha nia na kuwa mstari wa mbele kupigana na biashara hiyo haramu, ni ukweli usiopingika kwamba tatizo la dawa ya kulevya ni kubwa na lenye madhara makubwa sana kwa watanzania wengi haswa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” alifafanua Dkt. Gadi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, Vijana wengi wamepoteza maisha , kuharibika akili, kupata magonjwa ya kuambukiza, kupoteza malengo ya kimaisha kwa sababu ya dawa hizo. Vile vile dawa hizo zimeleta fedheha kwa Taifa kutokana na Vijana wengi wa Kitanzania kuwepo katika magereza mbalimbali Duniani huku wengine wakisubiri adhabu ya kunyongwa.
Aidha amempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kuimarisha Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kumteua Kamishna ambaye atasimamia Mamlaka hiyo na anaamini kwamba kwa neema ya Mungu ataweza kumsaidia kikamilifu Rais Magufuli katika kutimiza azma yake ya kukomesha biashara hiyo.
Wakati huo huo, Dkt. Gadi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuianzisha vita hiyo dhidi ya matumizi ya dawa kulevya katika mkoa wa Dar es Salaam. Vile vile amewapongeza waandishi wa habari na vyombo mbalimbali vya habari kwa kutoa habari zinazosaidia katika upambanaji wa biashara hiyo.
Dkt. Gadi amewataka viongozi wa Dini kuungana bega kwa bega na Rais Magufuli kwa kuendelea kutoa maadili kwa vijana ili kuepukana na uovu wa dawa za kulevya nchini.
Askofu wa Good News for All Ministry, Dkt. Charles Gadi akizungumza na waandishi wa habari wakati madhehebu mbalimbali hapa nchini walipomuombea Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nchi, pamoja na kumpongeza kwa kumteua Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dar es Salaam leo. Kushoto ni Askofu Hezron Mwamsemba wa Kanisa la Baptist jijini na katikati ni Askofu Ernest Sumisumi wa kanisa hilo.(Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Baadhi ya waandishi wa habari, wakimsikiliza Askofu wa Good News for All Ministry, Dkt. Charles Gadi wakati alipokuwa akizungumza.
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo, wakiongozwa na Askofu wa Good News for All Ministry, Dkt. Charles Gadi (katikati), wakiimba wimbo wa amani wakati wa kumuombea Rais Dk. Magufuli na Taifa.
Askofu Filbert Mbepera (wa pili kuli) wa Kanisa la EAGT, akiombea amani nchi.
Askofu Ernest Sumisumi (wa pili kushoto) wa Kanisa la Baptist akiiombea ramani ya Tanzania pamoja na picha ya Rais Dk. John Magufuli.
Askofu wa Good News for All Ministry, Dkt. Charles Gadi na Askofu Filbert Mbepera (kuli), wakiyabariki mafuta ya kupaka picha ya Rais, Dk. Magufuli.
Askofu Hezron Mwamsemba wa Kanisa la Baptist akiipaka mafuta picha ya Rais Dk. John Magufuli.
Maaskofu wa madhehebu mbalimbali wa dini ya Kikristo, wakiinyanyua juu picha ya Rais Magufuli, baada ya kuipaka mafuta na kuiombea.
Askofu John Sambuki (wa pili kulia) wa Victory Gospel Assemble a.k.a Furahini Katika Bwana, akiiombea bendera, wakati wa hafla hiyo.
Maaskofu na baadhi ya watumishi wa madhehebu hayo ya dini ya Kikristo wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa maombi hayo.
No comments:
Post a Comment