Tuesday, December 13, 2016

WIZARA YA AFYA YAPOKEA VIFAA UZAZI KUTOKA ECOBANK

 UPUNGUFU wa vituo vya afya na watoa huduma wasiokuwa na ujuzi na stadi za kuokoa maisha ni miongoni mwa vyanzo vinavyochangia kasi ndogo ya kuondokana na vifo vya uzazi na watoto wa umri wa chini ya mwezi mmoja.
           
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Khamis Kigwangalla, alipokuwa akipokea msaada wa vifaa tiba vya uzazi kutoka Eco bank.
 
Vifaa hivyo vilivyotolewa kwa hospitali ya rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wakati benki hiyo ikiadhimisha siku yao ambayo mwaka huu kauli mbiu ilisema, ‘kuboresha huduma kwa wajawazito barani Afrika.’
 
“Katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la vifo vinavyotokana na uzazi, jawabu lipo katika kuongeza vituo vya afya na watoa huduma wenye ujuzi na stadi za kuokoa maisha pamoja na vifaa tiba vya kutosha,” alisema.
 
Hata hivyo, Dk Kigwangalah alisema hali si nzuri kwa upande wa vifo vya uzazi na watoto wenye umri wa mwezi mmoja kutokana na takwimu zilizopo kuonyesha kuwapo kwa kasi ndogo katika udhibiti wake katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
 
Alisema takwimu za vifo hivyo zinaonesha kuwa mwaka 1996 kulikuwa na vifo 529 vilivyopungua kufikia 432 kwa vizazi hai 100,000 katika kipindi cha mwaka 2012, ikiwa ni sawa na vifo 7,500 kwa mwaka mmoja.
 
Kwa upande mwingine, Dk Kigwangalla alisema vifo vya watoto wachanga wenye umri wa chini ya mwezi mmoja ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili afya ya uzazi kutokana na takwimu kuonesha kuwapo (vifo) 21 kwa kila vizazi hai 1,000
 
Akizungumza katika halfa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Eco Bank, Enoch Osei Safi alisema siku ya benki hiyo inaadhimishwa katika nchi 33 za Afrika na kushirikisha utoaji misaada kulingana na mahitaji na mazingira ya nchi husika.
 
“Tumeazimia kuadhimisha siku yetu kwa kuipatia hospitali hii vifaa tiba vya uzazi ikiwa ni baada ya mashauriano ya pamoja yaliyotuwezesha kuwapo upungufu katika eneo hilo,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Safi, Eco Bank iliichagua hospitali ya rufaa ya Temeke kutokana na namna inavyowahudumia watu wengi kutoka maeneo tofauti ya jijini Dar es Salaam ikilinganishwa na hospitali nyingine.
 
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dk Gwamaka Mwabulambo, alisema wajawazito kati ya 50 hadi 80 wanajifungua hospitalini hapo kila siku, 10 kati yao wakijifungua kwa njia ya upasuaji.
 
Dk Mwabulambo alisema ipo haja kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali ili kufanikisha mahitaji ya hospitali hiyo katika kuwahudumia wajawazito na watoto.

 
 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Dk Amani Malima (aliyesimama) akizungumza kwenye hafla hiyo.
  Mkurugenzi Mtendaji wa ECO Bank, Enock Osei Safi (aliyesimama) akihutubia kwenye hafla hiyo.
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Khamis Kigwangalla akihutubia kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya wajawazito walioshiriki hafla ya kukabidhi vifaa vya kujifungua vilivyotolewa na benki ya Eco Bank.


  
Mkurugenzi Mtendaji wa Eco Bank, Enock Osei Safi (kushoto) akimkabidhi msaada wa vifaa vya uzazi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Khamis Kigwangalla (wa pili kushoto),
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Dk Amani Malimana na
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dk Gwamaka Mwabulambo

No comments: