Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemavu Mhe.Jenista Mhagama
Na Daudi Manongi
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe.Jenista Mhagama amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw. Majid Mwanga kuhakikisha ana tatua mgogoro wa ujenzi wa barabara ya Kiwangwa-Mabohelo yenye urefu wa kilomita 15 na kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Ameyasema hayo jana Wilayani wakati alipotembelea miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Bagamoyo kwa ufadhili wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini(MIVARF) inayosimamiwa na chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Serikali ya Awamu ya Tano ina lengo kubwa la kuwasaidia wananchi hususani wakulima ili wafikiwe na miundombinu ili kupambana na umaskini na kuboresha masuala ya masoko yao na hivyo kuwaongezea kipato”, Alisema Mhagama.
Aidha Mhe. Mhagama alisema kuwa asili ya miradi ya ufadhili wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu haina fidia hivyo anashangaa kuona ni kwanini ujenzi vipande hivyo vitatu vya barabara vinachelewa kukamilika hadi kufikia leo.
Ameongeza kuwa pesa za kumalizia mradi huo zipo na kusema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kukosekana kwa mawasiliano kati ya Halmshauri za Bagamoyo na Chalinze na kuwaagiza Viongozi wa Halmashauri hizo chini na kumaliza mgogoro huu mara moja ili wananchi wafanikishe lengo kuu la mradi huo ambao ni umwagiliaji.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe.Ridhiwani Kikwete alisema kuwa tatizo kubwa linalofanya mradi huo kutokamilika ni kutoshirikishwa kwa wananchi na kuitaka halmashauri ya Bagamoyo kukaa pamoja na wao ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw.Majid Hemed Mwanga aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la mgogoro huo ndani ya muda alioagizwa kwa kuwashirikisha madiwani wote.
No comments:
Post a Comment