Saturday, December 17, 2016

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KUHUSIANA NA HALI YA UHALIFU KWA KIPINDI CHA JANUARI – DESEMBA, 2016.

DCP DHAHIRI A. KIDAVASHARI, KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Aidha kwa kipindi cha mwaka 2016 Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukabiliana na kupunguza matukio ya uhalifu katika mkoa wetu.

MAFANIKIO YA MISAKO, OPERESHENI NA DORIA. 
Kwa ujumla katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2016 hali ya uhalifu mkoa wa mbeya kwa makosa yote ya jinai makubwa na madogo umepungua kwa asilimia 1.4, matukio ya ajali yamepungua kwa asilimia 19.

Baadhi ya mafanikio ambayo Jeshi la Polisi mkoa wa mbeya kwa kushirikiana na wananchi yamepatikana ni pamoja na:-

v Bhangi uzito wa kilo 435 na gram 794 na mashamba makubwa 3 ukubwa wa ekari 2 ½   ilikamatwa.
v Dawa za kulevya aina ya heroine gram 80 zilikamatwa.
v Mirungi yenye uzito wa kilo 2 na gram 100 ilikamatwa.
v Pombe ya moshi [gongo] ujazo wa lita 792 na mitambo 22 imekamatwa.
v Nyara za serikali zenye thamani ya Tshs 197,520,000/= na Dola za Kimarekani 450,400 zimekamatwa.
v Wahamiaji haramu 142 walikamatwa, kati yao Somali 14, Ethiopia 76, Burundi 12, Malawi 34, Pakistan 4, Zambia 1 na Zimbabwe 1.
v Silaha   19  kati ya hizo smg 2shortgun 6, riffle 1,  gobole 9   na  bastola 1 na risasi 65, risasi  53 za smg, risasi 6 za shortgun na risasi 6 za bastola  zilikamatwa.
v Noti bandia 66 @ Tshs 10,000/= sawa na Tshs 660,000/= na noti 2 @ Tshs 5,000/= sawa na Tshs 10,000/= zilikamatwa.
v Majambazi 2 kati ya 5 waliuawa Wilaya ya Chunya kwenye mapambano ya kurushiana risasi na polisi wakati wakijaribu kufanya uhalifu. Silaha 2 shortgun 22555 Double barriel  na shortgun iliyotengenezwa kienyeji na  risasi  6,  panga 1 na maganda  4  ya  shortgun zilikamatwa. Pia pikipiki 2 zilikamatwa T.520 CDC T-Better na T.481 CTA Kinglion. Majambazi 3 walifanikiwa kukimbia. Hakuna mali iliyoporwa.
v Majambazi 2 kati ya 4 waliuawa Wilaya ya Rungwe kwenye mapambano ya kurushiana risasi na polisi wakati wakijaribu kufanya uhalifu. Silaha 2 Bastola B-15859 na gobole 1 risasi 2 za shortgun zilikamatwa. Majambazi 2 waliojeruhiwa walifanikiwa kukimbia. Hakuna mali iliyoporwa.
v Tumepunguza  mlundikano wa mahabusu magerezani kwa kiasi kikubwa.
v Maduhuli [tozo] kwa makosa ya usalama barabarani Tshs 1,775,970,000/= yamekusanywa kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani. 

USALAMA BARABARANI 
Kwa upande wa makosa ya  usalama barabarani, jumla ya  makosa  yote ya  ajali pamoja na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2016  yalikuwa 60,778, wakati kipindi kama hicho  mwaka 2015 makosa 56,798 yaliripotiwa.

Matukio ya ajali kwa mwaka 2016 yalikuwa 352, wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 yalikuwa 434. Ajali zilizosababisha vifo mwaka 2016 zilikuwa 157 wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 ziliripotiwa ajali 172. Watu waliokufa kutokana na ajali kwa mwaka 2016 walikuwa 182, wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 walikufa watu 231.

Ajali za majeruhi mwaka 2016 zilikuwa 195 wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 ziliripotiwa ajali 262. Watu waliojeruhiwa katika ajali mbalimbali mwaka 2016 walikuwa 467 wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 walikuwa watu 458.

Pesa zilizokusanywa kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani [notification] mwaka 2016 zilikuwa Tshs 1,775,970,000/= wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 zilikusanywa pesa Tshs 1,142,870,000/=. 

Aidha baadhi ya  sababu za kuongezeka kwa matukio ya ajali ni kuongezeka kwa vyombo vya usafiri mkoani mbeya hasa magari na pikipiki, baadhi ya  madereva kutokuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na mwendo kasi hasa usiku na ulevi  licha ya  jitihada za Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na baadhi ya  wadau kutoa elimu hiyo mara kwa mara. Hali ya hewa hususani ukungu na utelezi katika baadhi ya maeneo ya barabara ya mbeya, rungwe na kyela.

MATUKIO MAKUBWA YA JINAI 
Kwa ujumla makosa yote ya jinai yaliyoripotiwa katika kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa ni 22,079 ikilinganishwa na makosa 24,833 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2015. Kati ya  makosa hayo yote,  makosa makubwa yalikuwa 1,977  wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 makosa makubwa yalikuwa 2,083.

Makosa madogo yaliyoripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba – 2016 yalikuwa 20,102 wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 yalilipotiwa matukio 22,750.

Makosa yatokanayo na jitihada za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine kupitia misako/doria kwa mwaka 2016 yalikuwa 620, wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 yalikuwa 605.

WITO WA KAMANDA.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI  A. KIDAVASHARI anatoa pongezi kwa  wananchi wote wa mkoa wa mbeya kwa ushirikiano wao wa dhati kwa jeshi la polisi katika mapambano dhidi ya  uhalifu na wahalifu kupitia dhana ya  ulinzi shirikishi na polisi jamii katika kipindi chote cha mwaka 2016. Aidha anatoa rai kwa jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kipindi chote ili kuhakikisha mkoa wetu wa mbeya unakuwa salama.

Aidha anatoa wito kwa wazazi/walezi kuzingatia utoaji wa malezi bora kwa watoto/vijana ili wakue katika misingi mizuri ya maadili mema kijamii na kujiepusha na matukio ya kiuhalifu na kukataa uhalifu wangali wadogo ikiwa ni pamoja na kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya, kucheza kamari, ulevi uliopitiliza. 
Kwa kutambua kuwa suala la ulinzi na usalama unaanzia ngazi ya familia, mtaa, kijiji, kitongoji, kata, tarafa, wilaya hadi ngazi ya mkoa, ni vyema kila mmoja wetu kutambua na kuamini usalama wa mali na maisha yetu unaanza na mimi, wewe na sisi sote. Kwa kuimarisha ulinzi na usalama wetu na mali zetu inatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika mkoa wetu, wananchi kujiajiri na kuajiriwa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii bila kuathiri amani na utulivu. 

Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismas na mwaka mpya ikiwa kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika maeneo yao. Pia kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuheshimu sheria za barabarani, watembea kwa miguu kuzingatia alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Pia anatoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini kwa watoto wao wanapotoka kuelekea Kanisani na Kumbi za Starehe kwa kuhakikisha wanakuwa na waangalizi. 
Pia kamati za ulinzi na usalama katika Nyumba za Ibada kuhakikisha ulinzi wa ndani na nje unaimarishwa kwa kushirikiana na askari watakaopangwa maeneo hayo. Wamiliki wa kumbi za starehe kuweka ulinzi maeneo yote, kuepuka kuingiza watu kupita kiasi pamoja na kuzingatia muda wa kufungua na kufunga kumbi zao. Aidha kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa nafasi yake itasaidia kuzuia uhalifu na makosa ya barabarani ambayo yanaweza kusababisha madhara kwa jamii. 

                                                Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP].
 KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments: