Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar
imedhamiria kubadilisha mitaala katika Skuli za Sekondari sambamba na
kuimarisha vyuo vya amali ili somo la ujasiriamali liweze kuchukua nafasi kubwa
katika mitaala na kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari wanafaulu
vyema ujasiriamali.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Kongamano la siku mbili na
maonyesho ya Wajasiriamali linalofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la
Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kwa utaratibu huo wanafunzi watapata
eimu itakayowasaidia kujiajiri wenyewe na kutumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali, kuhakikisha kuwa inaongeza kasi katika kulishughulikia
suala hilo.
Dk. Shein aliwakumbusha vijana kuwa elimu waliyoipata katika Vyuo Vikuu na Taasisi
mbali mbali zinazotoa mafunzo ya kazi na ufundi ni mtaji muhimu katika
kuendeleza shughuli za ujasiriamali.
Hivyo, aliwataka wasijenge dhana kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara
ndogo ndogo za bidhaa zinazoonekana katika masoko lakini wajifunze kutokana na
uzoefu wa nchi mbali mbali hasa India ambapo vijana wengi waliosoma wamekuwa
wakijiajiri wenyewe baada ya kumaliza masomo yao.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa kuwaendeleza
wajasiriamali katika kuyafikia malengo ya kupambana na umasikini wa kipato na
kupunguza tatizo la ajira hasa miongoni mwa wanawake na vijana.
Alisema kuwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kipindi hiki cha pili cha
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ameamua kuyaweka makundi ya vijana na wanawake
katika wizara moja na masuala ya uwezeshaji ili shughuli za uwezeshaji kupitia
ujasiriamali ziweze kukuza kipato cha wananchi na kuondoa umasikini.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio ya Mfuko wa Uwezeshaji
ambao katika kipindi cha miaka miwili na miezi minne tangu mfuko huo ulipoanza
kazi zake ambapo jumla ya mikopo 998 yenye jumla ya Tsh. Bilioni 1.6
imeshatolewa Unguja na Pemba ambapo tayari marejesho ya asilimia 96
yameshafanyika.
Alisema kuwa jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa taarifa zinazonesha kwamba
asilimia 67 ya watu waliopewa mikopo ya Mfuko huo ni vijana wenywe umri kati ya
miaka 18 hadi 35 huku akiwataka wanasiasa kutowadanganya vijana kuhusiana suala
la ajira kwani vijana hivi sasa hawadanganyiki
Alisema kuwa lengo la viongozi hao wa kisiasa ni kutaka kuwagombanisha
vijana na Serikali yao na kuwataka viongozi hao kusema ukweli katika suala zima
la ajira.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi na wajasiriamali kuwa Serikali kupitia
Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto na Wizara ya
Biashara, Viwanda na Masoko imejipanga ili kuona kwamba wajasiriamali wanafikia
malengo waliyoyakusudia kwa kuwatafutia masoko.
Dk. Shein aliwaeleza wajasiriamali hao kuwa watu matajiri na maarufu
duniani kote ikiwemo Zanzibar ni wajasiriamali hivyo, aliwahimiza kuendelea
kukuza vipaji na elimu walizonazo wakiamini kwamba nao wanaweza kufanikiwa kama
walivyofanikiwa wao.
Pia, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea kuzitatua changamoto
zinazowakabili wakulima na wajasiriamali katika suala zima la kuongeza ubora wa
bidhaa na mazao yanayolimwa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara ya Uwezeshaji, Wazee,
Vijana, Wanawake na Watoto kwa mafanikio yaliopatikana katika kituo cha Kuleta
na Kukuza Wajasiriamali kilichopo Mbweni kwa kushirikiana na washirika wa
maendeleo na kusisitiza haja ya kuharakishwa ujenzi wa kituo kama hicho huko
Pemba.
Mapema Dk. Shein aliangalia maonyesho ya Wajasiriamali ambapo alipata fursa
ya kukagua bidhaa zao mbali mbali wanazozizalisha. Pia katika hafla hiyo alitoa
vyeti maalum kwa wachangiaji wa kongamano hilo.
Nae Waziri wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto
Maudline Castico alisema kuwa kongamano hilo ni la kwanza la aina yake
kufanyika hapa nchini na kueleza kuwa mchango wa Sekta binafsi kupitia
wajasiriamali wakubwa na wadogo ni muhimu sana ili kufikia lengo la Zanzibar
kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati ifikapo 2020.
Alisema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuhamasisha kuwaelimisha
wajasiriamali ili kuendeleza shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Wajasiriamali katika risala yao iliyosomwa na Aziza Saleh, walieleza kuwa wanafahamu
kwamba wakati huu wa mabadiliko ya uchumi duniani kote ni wajasiriamali
watakaosaidia kuzalisha ajira kupitia ujasiriamali, ili kusaidia Serikali
kukuza uchumi wake.
Walieleza kuwa wajasiriamali wabunifu na wavumbuzi wanauwezo wa kuanzisha
mambo tofauti kulingana na mahitaji ya soko yaliopo ili kuweza kuchangia pato
la Taifa na ukuaji wa uchumi hapa nchini iwapo tu wataelekezwa na kupatiwa
utaalamu unaohitajika.
Nao Wawakilishi wa Shirika la kujitolea la Kimataifa (VSO), pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia
Tanzania (COSTECH) kwa nyakati tofauti waliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia wajasiriamali ili
kufikia lengo lililokusudiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akizindua Kongamano la Wajasiriamali katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akizindua Kongamano la Wajasiriamali katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi zawadi Meneja wa Tawi la DTB hapa Zanzibar Mbarouk Ramadhan Mbarouk katika hafla ya uzinduzi wa Kongamano la Wajasiriamali Zanzibar katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi zawadi Ofisa wa Taasisi ya 'Mchele Z'bar Foundation' hapa Zanzibar Eshe Haji Ramadhan katika hafla ya uzinduzi wa Kongamano la Wajasiriamali Zanzibar katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo
Mratibu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Dkt.Afwa Mohamed akitoa hutuba fupi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia katika hafla ya uzinduzi wa Kongamano la Wajasiriamali Zanzibar katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo,ambalo lilizinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
Baadhi ya Wajasiriamali wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akizindua Kongamano la Wajasiriamali hao lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo
Sehemu ya Wajasiriamali wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akizindua Kongamano la Wajasiriamali hao lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mnazi Mmoja Mjini Unguja leo
No comments:
Post a Comment