Shule ya Sekondari Loyola imeibuka mshindi wa mashindano ya
vilabu vya kodi mwaka 2016 na kujinyakulia zawadi ya Televisheni ya Inchi 40,
Kompyuta ya mezani pamoja na Printa moja baada kuonesha uwezo wa hali ya juu
katika kujibu maswali ya kodi wakati wa mashindano ya vilabu vya kodi
yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Shaaban Robert Jijini Dar es
Salaam.
Nafasi ya pili katika
mashindano hayo imeshikwa na shule ya Sekondari Kibaha ambayo ilizawadiwa
Kompyuta ya mezani na Printa wakati shule ya Sekondari ya St. Joseph imekuwa
mshindi wa tatu na kupatiwa Kompyuta ya mezani.
Zawadi ya shule iliyowasilisha
mada bora ya kodi ilinyakuliwa na shule ya Sekondari Shaaban Robert ambapo mwanafunzi
Adamson Nsimba kutoka shule ya Sekondari St. Joseph ameibuka mwanafunzi bora na
kuzawadiwa Kompyuta mpakato.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa
na kuratibiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalizishirikisha shule za
sekondari 47 kutoka katika mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani kwa lengo la kupima uelewa wa masuala ya kodi miongoni mwa
wanafunzi ikiwa ni mkakati wa kujenga uzalendo na uhiari wa kulipa kodi kupitia
shule za sekondari kwa kuwajengea uwezo wa kuwa walipakodi wa baadae.
Kati ya shule hizo zilizoshiriki,
jumla ya shule 18 zilishindana katika kuwasilisha mada mbalimbali za kodi baada ya kuibuka washindi katika mashindano
ya awali yaliyofanyika Tarehe 26 Novemba 2016 katika Chuo cha Kodi (ITA) ambayo
yalishirikisha shule 46 za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Mada ambazo ziliwasilishwa na kushindanishwa katika
shindano hilo ni pamoja na Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT), Mashine za Kielektroniki za Kodi (EFD’s) na Utunzaji
wa Kumbukumbu za Biashara; Uingizaji wa Bidhaa Nchini na Uuzaji wa Bidhaa Nje
ya nchi; Mifumo ya Ulipaji Kodi na Kodi ya Mapato Yatokanayo na Ajira (PAYE).
Mada nyingine
zilizowasiliswa katika mashindano hayo ni Uboreshaji wa Mifumo na Utawala wa
Kodi Tanzania, Kodi ya Mapato Yatokanayo na Rasilimali na Mapato yatokanayo na Biashara.
Akiongea wakati wa ufunguzi
wa mashindano hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA Bw. Richard
Kayombo alisema, mashindano hayo ya vilabu vya kodi kwa shule za Sekondari
yalianza kufanyika baada ya kuzinduliwa vilabu vya kodi katika shule za
Sekondari mwaka 2008 ili kukuza uelewa wa masuala ya kodi kwa wanafunzi na
kuongeza hamasa ya ushiriki wa mashindano hayo.
“Tayari
TRA imezindua jumla ya vilabu vya kodi katika shule za Sekondari 220 za
Tanzania Bara na Visiwani zikiwa na wananfunzi
wanachama 16,620”. Alisema Bw.
Kayombo.
Bw.
Kayombo amesema TRA itaendelea kusaidia vilabu vya kodi kadri inavyoweza kwani
kupitia vilabu vya kodi Taifa linapata vijana wenye uelewa wa kodi ambao wanakuwa
mabalozi wazuri wa masuala ya kodi na hivyo kupata taifa lenye uelewa wa
masuala ya kodi na kujijengea utamaduni wa kulipa kodi.
Kwa
upande wake Mratibu wa vilabu vya kodi Tanzania ambaye ni Meneja wa Huduma kwa
Mlipakodi TRA Bi. Honesta Ndunguru alisema pamoja na kuzindua vilabu vya kodi
katika shule za sekondari; TRA pia imepanua wigo wa vilabu hivyo kwa kuanzisha
Jumuiya za Kodi kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambao kwa pamoja na shule za Sekondari
watakuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi mashuleni, vyuoni na katika jamii
kwa ujumla.
Mwanafunzi
bora Adamson Nsimba ametoa wito kwa wanafunzi wote kujiunga na vilabu vya kodi
ili wapate uelewa wa masuala ya kodi na hivyo kujijengea utamaduni wa kulipa
kodi kwa hiari.
No comments:
Post a Comment