Thursday, December 15, 2016

NEC YATOA SOMO KWA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA DIMANI ZANZIBAR.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damiani Lubuva akifungua kikao cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyama vya Siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi mdogo katika jimbo la Dimani Zanzibar leo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akitoa ufafanuzi kwa viongozi wa vyama vya Siasa kuhusu maadili ya kuzingatia kwa vyama vya Siasa wakati wa uchaguzi huo na maandalizi ya Uchaguzi wa jimbo la Dimani leo mjini Zanzibar. 
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damiani Lubuva (kushoto) akiwa na wajumbe wa NEC wakakifuatilia mkutano huo leo mjini Zanzibar.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa ufafanuzi kwa viongozi wa vyama vya Siasa kuhusu maadili ya kuzingatia kwa vyama vya Siasa wakati wa uchaguzi huo na maandalizi ya Uchaguzi wa jimbo la Dimani leo mjini Zanzibar. 
Viongozi wa vyama vya Siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mdogo katika jimbo la Dimani wakifuatilia mada wakati wa mkutano wao na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mjini Zanzibar leo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damiani Lubuva (kushoto) akizungumza na baadhi ya viongozi wa vyama vya Siasa mjini Zanzibar mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Tume na Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo jimbo la Dimani mjini Zanzibar.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa NEC Bw. Emmanuel Kawishe akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya kisheria leo wakati wa Mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani. PICHA/Aron Msigwa – NEC. 


Na. Aron Msigwa – NEC, Zanzibar.


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka Vyama vya Siasa na wagombea watakaoshiriki Uchaguzi mdogo katika jimbo la Dimani visiwani Zanzibar kuzingatia Sheria , Kanuni, Taratibu na Maadili ili Uchaguzi huo uwe huru na wa haki na kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Zanzibar na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damiani Lubuva wakati akizungumza na Viongozi 19 wa vyama vya Siasa waliohudhuria mkutano wa maandalizi ya kufanikisha Uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani utakaofanyika Januari 22, 2017.

Amewataka viongozi wa Vyama vya Siasa waliohudhuria mkutano huo waendelee kudumisha hali ya amani na Utulivu wakati wa kampeni za vyama vyao zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni pia kutoa ushirikiano kwa Waratibu na Wasimamizi wa Uchaguzi huo.

“Ni matarajio ya Tume kuwa, Vyama vya Siasa vitatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha uchaguzi wetu katika jimbo la Dimani unakuwa Huru na wa Haki, lengo hili litafanikiwa tu iwapo vyama na wagombea wote watazingatia na kufuata sharia na maelekezo na maadili ya Tume” Amesisitiza Jaji Lubuva.

Amevitaka vyama vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo wakati wa kampeni vijikite katika kuelezea Sera zao na si vinginevyo pia kuepuka matumizi ya lugha ambazo zinaweza kusababisha machafuko.

Ameeleza kuwa katika kufanikisha uchaguzi huo kila Chama cha Siasa kina haki ya kuteua Wakala mmoja kwa kila kituo cha kupigia kura ili kuongeza uwazi katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa mawakala hao watapangwa kwenye vituo vilivyo ndani ya Shehia wanakoishi ili waweze kuwatambua wapiga kura katika eneo husika.

“Vyama vyote lazima muhakikishe kuwa mawakala mnaowateua wanaelewa hatua zote muhimu za uchaguzi vituoni kuanzia hatua ya kwanza ya kufungua kituo hadi kutangaza matokeo” Amesisitiza.

Aidha, Mhe. Lubuva amewasisitiza viongozi wa vyama hivyo watambue kuwa watu watakaopiga kura Januari 22,2017 ni wale walioandikishwa kwenye daftari la kudumu Wapiga Kura ambao watakuwa na Kadi za kupigia kura na si vinginevyo.

“ Naomba ninyi viongozi wa vyama vya Siasa muwakumbushe wanachama wenu walio na sifa na kadi za kupigia kura wajitokeza siku ya kupiga kura, pia muendelee kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura siku hiyo” Amesema Mhe. Lubuva.

Katika hatua nyingine Mhe. Lubuva amewakumbusha viongozi hao kuwa wananchi wakishapiga kura hawapaswi kubaki katika eneo la vituo vya kwa kuwa vyama hivyo vitakuwa na Mawakala ndani ya vituo hivyo na kuongeza kuwa ni marufuku kwa mgombea , Chama cha Siasa au Wakala kufanya kampeni Siku ya Uchaguzi kwani mwisho wa kupiga kampeni ni siku moja kabla ya siku ya uchaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhan akizungumza na viongozi wa vyama hivyo amesema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri huku akisisitiza kuwa ni matarajio ya Tume kuwa Vyama vyote vitazingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maelekezo na taratibu zote halalali zitakazotolewa na NEC.

Amewataka viongozi wa vyama hivyo kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wapiga kura wao kuepuka kufanya vitendo vya vurugu au viashiria vyovyote vya vurugu au uvunjifu wa amani ili wananchi wote waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Ametoa wito kwa wananchi wa jimbo la Dimani walioandikishwa kupiga kura wajitokeze kwa wingi Januari 22, 2017 kwenda kupiga kura ili kufanikisha uchaguzi huo.Kuhusu kampeni za vyama hivyo amesema kuwa zitaanza Desemba 23, 2016 hadi Januari 21, 2017 na kuvitaka vyama hivyo viwasilishe ratiba zao za kampeni kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo ili viweze kukubaliana ambapo kampeni zitakua zinaanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni.

Kwa upande wao viongozi wa vyama vya Siasa waliohudhuria mkutano huo kutoka vyama 19 wakizungumza kwa nyakati tofauti wameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu na kuahidi kutoa ushirikiano kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi huo.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo mjini Zanzibar wanatoka katika vyama vya ACT WAZALENDO,ADA, ADC,AFP, CCK, CCM, CHADEMA, CUF, Demokrasia Makini, DP, NCCR –MAGEUZI, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD, UPDP na CHAUMA.

No comments: