Thursday, December 15, 2016

TAASISI YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMU – NIMR YAELEZEA MAFANIKIO YAKE KWA MWAKA 2016 NA MATARAJIO YAKE KWA MWAKA 2017

 Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ,Dk. Mwele Malecela akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es salaam leo akielezea mafanikio ya Taasisi katika Mwaka 2016,katika nyanja mbalimbali ikiwmo Rasilimali na uimarishaji wa utawala Bora,Usimamizi wa utafiti za Afya,Tafiti za Afya ikinda sambamba na Matarajio yake kwa mwaka 2017
Baadhi ya Wadau na wataalamu mbalimbali pamoja na wanahabari wakimsikiliza  Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ,Dkt. Mwele Malecela alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyohusu mafanikio ya Taasisi hiyo katika Mwaka wa 2016 pamoja na Matarajio yake kwa mwaka 2017.Picha na Michuzi Jr.TAASISI YA TAIFA YA UTAFITI WA MAGONJWA YA BINADAMUTAARIFA KWA UMMA YA MAFANIKIO YA TAASISI KATIKA MWAKA 2016

Desemba 15, 2016


1.       RASILIMALI NA UIMARISHAJI WA UTAWALA BORA

Rasilimali fedha
Taasisi imeanzisha na kuanza kutumia mfumo wa fedha wa kielektroniki. Mfumo huu unaendeshwa kwa pamoja na mfumo wa serikali wa rasilimali watu. Ili kupanua matumizi ya mfumo huu mafunzo yametolewa kwa wahisbu wote wa Makao Makuu na Vituo Vikuu vya Utafiti. Lengo ni kuunganisha vituo vyote katika mfumo huo ili kurahisisha usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za Taasisi.

Rasilimali watu.

Taasisi imeendelea kuwapa uwezo watumishi wake katika ngazi mbalimbali za mafunzo. Watafiti 3 wameweza kuhitimu shahada za uzamivu, 6 shahada za uzamili and 4 shahada ya kwanza katika kipindi hiki. 

Taasisi imeshiriki katika utoaji mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi. Watafiti wa Taasisi wameshiriki kutoa mihadhara katika vyuo mbalimbali nchini – kama vile Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Cha Afya na Sayansi Shirikishi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela. Wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbali mbali ikiwemo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dodoma na taasisi nyingine wamepata mafunzo katika maabara zetu. Pia taasisi imeendelea kuwasaidia wafanyakazi wake kupata elimu ya juu katika ngazi za astashahada, shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na uzamivu. Watafiti watatu wametunukiwa shahada za uzamivu katika mwaka 2016.

Mwongozo wa Matumizi ya Tehama
Taasisi imeandaa Mwongozo wa Matumizi ya Tehama kwa ajili ya watumishi na wadau wake. Mwongozo huo unapatikana katika tovuti ya taasisi (http://www.nimr.or.tz)

Uandaaji wa Takwimu-msingi ya machapisho ya Taasisi
Katika kipindi cha 2016, Taasisi imeanza kuorodhesha machapisho yote ya kitaaluma iliyochapisha katika kipindi cha uhai wake (1980-2016). Takwimu-msingi hiyo itakuwa na machapisho ya majarida, vitabu na taarifa nyingine za kisayansi. Takwimu-msingi itakapokamilika, watafiti watakuwa na fursa ya kuongeza machapisho yao wenyewe kupitia tovuti ya taasisi. Hadi sana, machapisho 1,249 yamehifadhiwa kwenye takwimu-msingi.

Matumizi ya Mifumo ya Taarifa za Kijiografia 
Taasisi imeendelea kujenga uwezo wa watumishi wa afya kwa ngazi za mkoa na wilaya katika matumizi ya mifumo ya taarifa za kijiografia. Jumal ya watumishi 230 kutoka mikoa 16 na wilaya 107 wamepata mafunzo hayo. Kati ya hao, 214 wametoka katika Wilaya na 16 kutoka mikoani 

Huduma za Maabara inayotembea.

Taasisi imeendelea kutumia Maabara Inayotembea kutoa huduma za mafuzo katika Mkoa wa Mbeya. Lengo ni kufikisha huduma za afya karibu na wananchi. Mafunzo yalitolewa kwa njia mbalimbali, hususan kwa kutumia sinema. Magonjwa yaliyolengwa ni UKIMWI na Kifua kikuu. Katika kipindi cha Oktoba 2015 hadi Oktoba 2016, Maabara imeweza kuwafikia wateja 8,000; na asilimia 45% ya wagonjwa wa UKIMWI wameweza kuunganishwa na huduma hiyo. Huduma nyingine zinazotolewa na maabara hiyo ni kupima VVU, kupima chembechembe za damu za CD4, kupima Kifua Kikuu na saratani ya shingo ya uzazi. Huduma ya uchunguzi wa usugu wa dawa za kurefusha maisha (ARV) nayo imeongezwa katika huduma za maabara hiyo.

2. USIMAMIZI WA TAFITI ZA AFYA

Matumizi ya mtandao wa TEHAMA katika kuwasilisha na kupitia rasimu za tafiti.

Taasisi imeanzisha mfumo wa kielekitroniki wa kuwasilisha na kupitia ubora wa rasimu za kitafiti zinazohitaji kibali cha Kamati ya Maadili ya Utafiti wa Afya. Kwa mfumo huo, mtafiti anaweza kufuatilia hatua kwa hatua rasimu yake ilipo. Tayari mfumo huu mpya umeanza kutumika. Inatarajiwa kuwa ifikapo Januari 2017, rasimu zote zitawasilishwa kwa kutumia mfumo huu. 

3.TAFITI ZA AFYA KATIKA 2016

Tafiti za VVU/UKIMWI

UKIMWI katika kundi la waendesha bodaboda
 Utafiti wenye lengo la kutathmini viashiria vya maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI ulifanyika mwezi Agost 2016 katika Mkoa wa Dar es Salama na kuwahusisha vijana wanaondesha pikipiki za abiria (Bodaboda). Utafiti huo umeonesha kuwa kiwango cha maabukizi ya VVU kwa waendesha boda boda ni kidogo (2.5%). Hata hivyo, vijana wengi wanaoendesha boda boda wameonekana kuwa na tabia hatarishi zinazoweza kuwafanya wapate maabukizi ya VVU. Tabia hizo ni kama vile kuwa na wapenzi wengi, baadhi kutotumia kondomu na kutofuatilia ili kupata huduma ya ushauri nasaha na vipimo vya VVU. Taasisi inapendekeza kufanyika kwa utafiti kama huu katika maeneo mengine ya nchi na pia kujumuisha makundi mengine ambayo yako hatarini kuambukizwa VVU kama vile wasichana wanaofanya kazi za ndani.

Chanjo ya UKIMWI
Taasisi imeanza majaribio ya chanjo chini ya mkakati mpya kupitia mradi unaoitwa P5. Majaribio haya yanafanyika pia katika nchi za Botwana, Zimbabwe, Msumbiji, Zambia, Malawi, na Kenya.  Chini ya mpango huu, washiriki wenye umri kati ya miaka 15-50, wasio na maambukizi ya VVU na magonjwa sugu wanashiriki katika awamu mbalimbali za utafiti. Tanzania inashiriki majaribio haya kwa kushirikiana na washirika wake, Mpango wa Utafiti wa Jeshi la Marekani na Mtandao wa Tafiti za Ukimwi Duniani. Mpaka sasa taasisi imesajiri washiriki 17 kati ya 28 wanaotegemea kusajiriwa kwenye mojawapo ya tafiti hizi za chanjo. 

Saveilensi ya usugu wa dawa za UKIMWI
Pamoja na majaribio hayo, NIMR imeanza utafiti wa kufuatilia usugu katika dawa za kurefusha maisha (ARV) kwa watu wanaotumia dawa hizo. Utafiti huu unahusisha watu wanaotumia dawa za kurefusha maisha na unafanyika kwa miaka 15 kwa kushirikiana na hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Utafiti huu unafuatilia washiriki 500 wanaohudhuria matibabu katika kituo cha hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya.

Maambukizi ya VVU kwa Watoto
Taasisi imeendelea kufanya tafiti za virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI ikiwa ni pamoja na kutathmini utekelezaji wa mpango wa kupima VVU kwa watoto wachanga. Matokeo yameonesha kuwa mpango wa kupima VVU kwa watoto wachanga bado unakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo kuchelewesha majibu ya vipimo. Hata hivyo, imeonekana kuwa kuna uwezekano wa kuongeza vituo vya kupima sampuli za watoto wachanga katika hospitali za mikoa na baadhi ya hospital hapa nchini. Kwa hiyo, Wizara ya Afya imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kutumia maabara nyingine zenye uwezo wa kupima sampuli za watoto wachanga wanaodhaniwa kuambukizwa VVU. 

Tiba na mkakati wa Tiba-Kinga dhidi ya fangasi wanaosababisha maradhi ya uti wa mgongo kwa wenye maambukizi ya VVU
Kuvu au fangasi wa jamii ya Cryptococcus meningitis wanaosababisha maradhi ya uti wa mgongo huachangia kwa aslimia 25 kwenye vifo vya wagonjwa walioathirika na ukimwi. 
Taasisi imekamilisha utafiti wa kutafuta tiba ya homa ya uti wa mgongo unaosababishwa na fangasi aitwaye Cryptococcal meningitis kwa wagonjwa walioathirika na ukimwi kwa kutumia mseto wa dawa za aina mbili. Utafiti huu umehusha Tanzania, Malawi, Zambia na Cameroon. Matokeo ya awali yameonesha mafanikio mazuri katika kupunguza vifo kwa wagonjwa hawa. Matokeo ya mwisho yatatangazwa mwaka 2017 baada ya kumaliza uchambuzi wa takwimu. 

Taasisi pia, imekamilisha utafiti uliotathmini mkakati wa tiba-kinga wa kupunguza vifo kwa wagonjwa wenye maambukizi ya fangasi zinazosababisha maradhi ya uti wa mgongo kwa wagonjwa walioathirika na Ukwimi.  Utafiti huu umeonesha matokeo mazuri ya kupunguza vifo kwa asilimia 30 kwa wagonjwa walioathirika na ukimwi ambao wana maambukizi wa fangasi hawa. Matokeo ya utafiti huu yamechapishwa kweye jarida maarufu la The Lancet.  Kufuatia matokeo haya Taasisi ikishirikiana na Wizara ya Afya imeanzisha “tafiti elekezi“ ili kutekeleza mkakati huu kwenye utaratibu wa huduma za kawaida za afya hapa nchini. Hospitali 18 zitahusika kwenye mpango wa awali. 

Tafiti za Kifua Kikuu

Tathimini ya utambuzi wa maradhi Kifua Kikuu
Utambuzi wa maradhi ya kifua kikuu (KK) kwa ufanisi bado ni changamoto kubwa duniani. Taasisi ikishirikiana na wadau wengine imeendesha utafiti ambao umefanyika kutadhimini ufanisi wa vipimo vya uchunguzi wa maambukizi ya KK vya sasa (matumizi ya hadubini na uoteshaji vimelea) na uchunguzi upya (unaotumia kifaa kinachoitwa Gene Xpert) katika utambuzi wa kifua kikuu. Matokeo ya awali yanaonesha kuwa vipimo vya zamani na vipya vyote bado vina umuhimi katika utambuizi wa maambukizi ya KK kutegemeana na aina mbali mbali za ugonwa huo. 

Pamoja na uchunguzi huu, Taasisi imeanzisha utafiti wa kipimo kipya cha utambuzi wa maambukizi ya kifua kikuu katika viungo vilivyo nje ya mfumo wa kupumua (mapafu).  

Tafiti za ugonjwa wa malaria na magonjwa mengine yanayohusiana na homa
Tiba ya Malaria
Taasisi imeendelea kufanya tafiti za ugonjwa wa malaria. Tafiti zilizofanyika ni pamoja na kufuatilia ubora na usalama wa dawa mseto za kutibu malaria isiyo kali na tathmini ya chanjo ya malaria. Matokeo ya tafiti hizi yameonesha kuwa dawa mseto aina ya artemether-lumefantrine (ALU) bado inao uwezo mkubwa wa kutibu malaria isiyo kali na kiwango chake cha usalama ni kizuri. Pia matokeo ya tafiti zetu yameonesha kuwa chanjo ya malaria inaweza kutoa kinga kwa baadhi ya watoto na Shirika la Afya Duniani liko kwenye maandalizi ya kuanza matumizi ya chanjo hii katika maeneo machache yatakayochaguliwa. 

Malaria katika mifumo ya kilimo cha mpunga
Taasisi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Bugando imefanya utafiti wa uwezekano wa kutumia mbolea iliyochanganywa na viuatilifu katika mashamba ya mpunga kuua viluwiluwi vya mbu wa malaria. Utafiti huo ulifanywa kwenye mashamba ya mpunga eneo la Kilangali Wilayani Kilosa. Matokeo ya awali yanaonesha kuwa mseto wa mbolea na viuatilifu ni rahisi kutumiwa na wakulima kupunguza mazalio ya mbu katika mashamba ya mpunga.

Utafiti wa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu
Taasisi kwa kushirikiana Wizara ya Afya, imeendelea na utafiti wa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vinanyotumika kwenye vyandarua na kupuliziwa ndani ya kuta za nyumba kudhibiti malaria katila wilaya 23 Tanzania. Utafiti huu umebainisha kuna usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu. Maeneo ambayo yameonyesha usugu wa hali ya juu ni maeneo ya Arumeru, Bagamoyo, Geita, Muleba, Ruangwa na Sengerema.

Utafiti wa Homa zisizosababishwa na malaria
Taasisi imeendelea na utafiti wa maradhi yanayoambana na homa katika maeneo ya mkoa wa Mbeya- ambayo ni pamoja na Mbeya Mjini na mwambao wa Ziwa Nyasa (wilayani Rungwe na Kyela). Pamoja na malaria, utafiti huu umebainisha maambukizi makubwa ya Homa ya Matumbo katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Hususan, baadhi washiriki waligundulika kuwa na vimelea vya Homa ya Bonde la Ufa na Chikungunya,

Ufuatiliaji wa mradi wa kudhibiti mbu wa malaria kanda ya Ziwa Viktoria
Mradi huu ulionza mwaka 2007 unahusisha tathmini ya matumizi ya viuatilifu vya kupulizia majumbani katika kuangamiza mbu wa malaria kwenye Kanda ya Ziwa Viktoria. Mradi umeonesha matokeo chanya na ushiriki wa wananchi umeongezeka

Magonjwa ya Milipuko
Chanjo ya Ebola
Kufuatia mlipuko mkubwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi. Kwa kushirikiana na Kampuni ya Dawa ya Janssen & Jansen, Taasisi imefanya majaribio ya awali ya chanjo ya Ebola (Ebovac) katika maeneo ya kanda ya Ziwa Viktoria. Zoezi hili lilihusisha watu 25 na wote walimaliza dozi ya chanjo kama inavyotakia. Matokeo yameonesha kuwa chanjo hiyo (Ebovac) ni salama kwa binadamu na inauwezo wa kujenga kinga dhidi ya virusi vya Ebola. Ufuatiliaji wa wale waliopata chanjo unaendelea ili kutadhimini athari za muda mrefu za chanjo hiyo.

Maambuki ya Zika Tanzania
Taasisi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katolic Bugando kimefanya utafiti kuanisha uwepo wa maambukizi ya virusi vya Zika katika jamii ya watanzania – na kuangalia adhari ya maambukizi katika kusababisha watoto wanaozaliwa na ulemavu. Sampuli za damu kutoka watu 533 zilipimwa. Kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viuongo mbalimbali. Kati ya waliopimwa 533, 83 (15.6%) waligundulika kuwa wameambukizwa virusi vya Zika. Kati ya wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, 43.8% walikuwa wameambukizwa virusi vya Zika. Utafiti unaendelea kujua ukubwa wa tatitzo hili.

Magonjwa yasioambukiza
Matumizi ya pombe kwa vijana 
Taasisi imefanya utafiti kuhusu matumizi ya pombe kama kichocheo cha maambukizi ya UKIMWI. Matokeo ya awali yameonesha kuwa tatizo la matumizi ya pombe kwa vijana ni makubwa. Matokeo ya utafiti yamewasilishwa serikalini kwa ajili ya matumizi katika kuboresha sera. Iko haja kwa serikali kuandaa sera itakayoelekeza utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe nchini. 

Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipa umbele
Taasisi imeshirikiana na Mpango wa Taifa wa kuthibiti magonjwa yasiyopewa kiumbele kwa kufanya tafiti katika maeneo mbali mbali nchini. Tafiti hizi zimetoa mwelekeo wa maeneo ambayo baadhi ya magonjwa kama vile matende na usubi yameshatokomezwa na yale ambayo bado yanahitaji kutiliwa mkazo katika kutoa dawa na ufuatiliaji.

Tiba asilia
Taasisi imefunga mtambo wa kutengeneza dawa. Majadiliano na wadau wa ndani na nje yanaendelea ili kuweza kuingia ubia katika utengenezaji wa tiba asili. Baadhi ya dawa ziko katika mchakato wa kusajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa.

Mifumo ya Huduma za Afya
Matumizi ya TEHAMA katika kuimarisha mfumo wa saveilansi ya magonjwa katika ngazi ya jamii
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimetengeneza nyezo ya kielektroniki zinazoweza kutumika kutuma taarifa za matukio ya magonjwa katika ngazi ya jamii hadi ngazi za wilaya na taifa. Kwa kutumia mfumo huu, unaoitwa AfyaData, taarifa za matukio ya magonjwa zinatumwa na kuifikia ofisi husika katika muda ule ule. Pia, Taasisi imetengeza nyezo ya kielektronic ambayo inauwezo wa kuchanganua taarifa za magonjwa zilizotumwa na wanajamii na kuweza kuanisha aina ya ugonwa uliotokea. Hadi sasa, idadi ya wana jamii watoa taarifa 82 wamefundishwa matumizi ya AfyaData; watoa huduma wa vituo vya afya 41, maofisa mifugo 33 na maofisa wengine 14 wamepewa mafunzo hayo pia. Wilaya zilizofaidika in Temeke, Morogoro, Ngorongoro na Kibaha.


MATUMIZI YA MATOKEO YA TAFITI

Machapisho ya kitaaluma
Taasisi imeendelea kuchapisha Jarida lake Tanzania Journal of Health Research Toleo la 18 Namba 1, 2, 3, na 4 ya Januari, Aprili, Julai na Oktoba.  Pamoja, na jarida hilo, taasis imechapisha Makala 69 katika majarida ya Sayansi ya kimataifa kati ya Januari na Desemba 20116.

Tafsiri za matokeo ya tafiti
Watafiti 30 kutoka taasisi mbalimbali za utafiti Tanzania wamejengewa uwezo wa kutafsiri matokeo ya utafiti kwa ajili ya matumizi katika kuboresha sera na huduma za afya. Watafiti waliotoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Afya ya Ifakara, Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kilimanjaro, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Kanisa Katoliki-Bugando, Chuo Kikuu cha KCMC. Jumla ya Rasimu za Mapendekezo ya Sera (policy briefs) kumi ziliandaliwa, kuchapishwa na kusambazwa kwa wadau mbalimbali. Hususan, Taasisi iliandaa mkutano wa Watafiti na Watunga Sera tarehe 15 Machi 2016. Mkutano wa pili wa aina hiyo umepangwa kufanyika kesho Desemba 16, 2016 na utawashirikisha watafiti, viongozi wa juu wa Serikali (Afya, Kilimo/Mifungo, TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mashirika ya Kimataifa kama WHO, wawakilishi wa wananchi na watunga sera).

Mwongozo kuhusu chanjo ya VVU
Taasisi iliitisha mkutano wa wadau wa mapambano ya UKIMWI mwezi Septemba 2016. Washiriki walikuwa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Kamisheni ya UKIMWI Tanzania, Wizara ya Afya, Waratibu wa Mpango wa Kudhibiti UKIMWI wa Mikoa na Wilaya. Agenda ilikuwa ni kujadili matokeao ya tafiti kuhusu uwezekano wa kujumuisha chanjo ya VVU katika Mwongozo wa Utoaji ushauri nasaa na Upimaji wa UKIMWI Tanzania. Washiriki walikubaliana kwa pamoja kuwa masuala ya chanjo ni muhimu sana na kuna haja ya kuendelea na mashauriano zaidi ili kujua ni namna gani taarifa za chanjo na uelimishaji wa wafanyakazi wa afya utajumuishwa katika mwongozo wa utoaji ushauri nasaa na upimaji wa UKIMWI Tanzania. 

Kongamano la 30 la Sayansi
Taasisi iliandaa na kufanikisha kufanyika kwa kongamano lake la 30 la wanasayansi Oktoba 4-6, 2016. Lengo la Kongamano hili ni kuwakutanisha watafiti, watunga sera, wakufunzi, na wadau wa afya kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti mbalimbali za afya. Katika kongamano hili, matokeo ya tafiti mbalimbali yalitolewa na kujadiliwa
Mada kuu ilikuwa: Haja ya Uwekezaji katika tafiti zenye ubunifu ili kufikia Malengo Endelevu ya Dunia. Mada kuu ililenga kujadili haja ya kuwekeza katika tafiti za mifumo ya utoaji huduma, magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza na tabia na shughuli za binadamu zinayochangia kuwepo kwa maradhi. Mada katika kongamano zililenga maeneo yafuatayo:
1.      Mikakati ya kuboresha afya ya uzazi, ya mama, watoto wachanga na vijana
2.     Kiwango cha magonjwa sugu yasiyoambukiza na changamoto zake
3.     Kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria
4.     Maji, Usafi na Afya kuelekea maendeleo endelevu
5.     Mkakati wa Afya Moja katika kufanikisha usalama wa afya duniani
6.    Magonjwa ya Kitropiki yasiyopewa kipaumbele
7.     Upatikanaji na utoaji huduma za afya: fursa na changamoto katika kufanikisha mkakati wa afya kwa wote
8.     Maradhi na changamoto za afya katika mazingira ya mijini

Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Kongamano hilo alikuwa Mh. Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jumla ya washiriki 302 walihudhuria na mada 199 ziliwasilishwa katika siku 3 za Kongamano. Washiriki walitoka nchi za Tanzania, Kenya, Australia, Uingereza and Marekani. 

Programu za Redio
Taasisi imeendesha programu mbalimbali za redio katika mwaka 2016. Katika mkoa wa Mbeya peke yake, programu 15 ziliendeshwa kwa kupitia redio. Kati ya hizo, 10 zililenga UKIMWI na Chanjo ya UKIMWI – lengo lilikuwa kuwahamasisha wananchi washiriki katika utafiti wa chanjo ya UKIMWI. Programu tano zililenga Kifua Kikuu (KK) na tafiti za Kifua. Wananchi walipewa elimu kuhusu ugonjwa huo (unavyoambukizwa, dalili, kinga na tiba). Pia wananchi walifahamishwa kuhusu tafiti za KK zinazoendelea katika mkoa wa Mbeya.

Ushiriki katika matamasha ya Kitaifa 
Taasisi ilishiriki katika matamasha mbalimbali ya kitaifa/kimataifa. Hususan, Siku ya Kifua Kikuu duniani (Machi 24, 2016), Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei 1, 2016), Maonesho ya Nane Nane (Agosti 2016) na Siku ya UKIMWI Duniani (Desemba 1, 2016). Taasisi ilitumia fursa hizo kutoa huduma mbalimbali kama vile kupima VVU, kutoa ushauri nasaha, elimu ya afya na ugawaji wa kondomu.

Taarifa hii imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
3 Barack Obama, S.L.P. 9653, 11101 Dar es Salaam, Tanzania
Tovuti: htpp://www.nimr.or.tz
Barua pepe: dg@nimr.or.tz


MATARAJIO YA 2017

RASILIMALI NA UIMARISHAJI WA UTAWALA BORA
Kuendeleza raslimaliwatu na kushiriki katika kutoa elimu ya juu
Taasisi itaendeleza jitihada zake za kuwajengea uwezo Wataalamu wa kada mbali mbali ikiwemo wanafunzi wa elimu ya juu uwezo wa kutoa huduma ya afya na kufanya tafiti zinazokidhi viwango vya kimataifa. Mkazo utawekwa kwenye huduma na tafiti za magonjwa ambayo yako kwenye vipaumbele vya kitaifa na kimataifa. Tutatoa nafasi kwa wanafunzi na wataalamu na pia kushiriki katika kufundisha wanafunzi katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi ikiwemo, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dodoma na taasisi nyingine. Tuendelea kutekeleza programu zetu za mafunzo kwa wafanyakazi wetu wanaotarajia kuanza na wale wanaondelea na masomo ya elimu ya juu hapa nchini na nje ya nchi. 

TAFITI ZA AFYA KATIKA 2017
Tafiti za homa na ugonjwa wa malaria
Hii itahusisha tafiti katika maeneo yafuatayo:
·        Kufuatilia ubora na usalama wa dawa mseto za kutibu malaria isiyo kali 
·        Kujenga uwezo na kufanya tafiti za kufuatilia hali ya usugu wa vimelea vya malaria dhidi ya dawa zinazotumika hapa nchini kutibu malaria isiyo kali
·        Kushirikiana na wadau mbali mbali katika kuendeleza tathmini ya chanjo ya malaria ya RTS,S. 
·        Kufanya tafiti ili kubaini vyanzo na tiba ya homa ambayo haitokani na malaria
·        Kufanya utafiti kuanisha aula mbadala za kuangamiza mbu waenezao maradhi ikiwa ni pamoja na majaribio ya vivutio vya mbu kwa watu na mazalio yao.

Tafiti za VVU/UKIMWI
Tutashirikiana na wenzetu wa ndani na nje ya nchi kufanya tatifi za VVU na UKIMWI katika maeneo yafuatayo.
·        Tathmini ya hali ya maambukizi ya VVU na ugonjwa wa UKIMWI kwa makundi yaliyoko kwenye hatari ya kupata maambukizi kama vile wafanyakazi wa ndani
·        Uboreshaji wa huduma za kupima VVU kwa watoto wachanga
·        Ufuatiliaji wa usugu wa VVU dhini ya dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wenye VVU/UKIMWI

Magonjwa yasiyopewa kipaumbele 
·        Kufanya tathmini ya maambukizi ya ugonjwa wa matende/mabusha na usubi 
·        Kuimarisha uwezo wa maabara yetu ili kutoa huduma ya kupima sampuli zinachukuliwa maeneo yanayolengwa katika kutomeza ugonjwa matende na usubi 

Magonjwa yasiyoambukiza 
·        Tathimini ya madhara ya upungufu wa damu kwa mama waja wazito katika kusababisha magonjwa yasioambukiza kwa watoto wao.

3. MATUMIZI YA MATOKEO YA TAFITI

Machapisho
Taasisi itaandaa na kuchapisha machapisho ili kutoa taarifa na matokeo ya tafiti zilizofanyika huko nyuma na zile zinazoendelea kwa sasa. Lengo letu ni kutoa machapisho yasiyopungua 150 katika majarida ya kimataifa katika mwaka wa 2017.

Ushiriki katika matamasha ya Kitaifa 
Taasisi inatarajia kushiriki katika matamasha mbalimbali ya kitaifa/kimataifa. Hususan, Siku ya Malaria duniani (Aprili 25, 2017), Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei 1, 2017) na Maonesho ya Nane Nane (Agosti 2017). Taasisi itatumia fursa hizo pale itakapowezekana kutoa huduma mbalimbali kama vile kupima maambukizi ya magonjwa mbalimbali na kutoa elimu na ushauri. Pia watafiti wetu watashiriki mikutano, warsha na kongamano vitavyofanyika nje ya nchi ikiwa ni pamoja na mkutano wa Kongamano la 31 la Taasisi.

Tafsiri ya matumizi ya matokeo ya tafiti

Taasisi inatarajia kuanda Kongamano lake la Sayansi baadae mwaka ujao kwa tarehe itakayopangwa na Menejimenti. Tutaendelea kufanya mikutano na watunga sera katika kila robo mwaka ili kujadili matumizi ya matoke ya tafiti 

No comments: