Wednesday, December 21, 2016

Maonyesho vyuo vikuu vya nje yatia fora Jijini Arusha
Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Education Link akifafanua jambo kwenye maonyesho ya vyuo vya nje yanayoendelea katika viwanja vya kumbukumbu ya Azimio la Arusha, Jijini Arusha.
Meneja wa Global Education Link tawi la Arusha, Regina Lema (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza kwa umakini mmoja wa watu waliofika kwenye maonyesho ya vyuo vya nje yanayoendelea katika viwanja vya kumbukumbu ya Azimio la Arusha, Jijini ArushaHAKUNA Ubishi kwamba Tanzania ni nchi inayohitaji teknolojia nyingi mpya ili iweze kukua haraka kiuchumi kwa kuendana na kauli ya Serikali inayotaka kuona Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.

Mojawapo ya njia inayoweza kusaidia kukuza haraka teknolojia nchini ni kwa Watanzania kwenda nje ya nchi kusoma kisha kurudi na ujuzi kuliendeleza taifa. Hivi ndivyo ilivyofanya nchi nyingi Duniani, hatimaye leo nchi hizo zimevuka kwenye lindi la umaskini.

Kwa wale ambao wanafuatilia historia ya Tanzania watakubaliana na ukweli kwamba nchi hii ilikotoka haikuwa na teknolojia nyingi muhimu, zikiwamo zile zilizosaidia kuharakisha maendeleo.

Kwamba, mambo mengi nchini yamekuwa yakifanyika kwa staili za kijadi, kwa mfano hata kupata mchele, mtu alilazimika kutumia nguvu kubwa kutwanga mpunga au ilikuwa ni lazima kutumia kinu kutwanga mahindi ili kupata unga, lakini ni kupitia teknolojia mpya, leo kuna mashine nyingi za kufanya kazi hizo katika maeneo mbalimbali nchini.Kwa sasa kuna teknolojia nyingi nchini, nyingi zikitokea nje ya nchi. Nyingi za teknolojia hizi zililetwa na wafanyabiashara au wasomi wachache waliokwenda nje, kwani sio wengi ambao wamekuwa na ufahamu kuhusu vyuo vya nje.

Ukilinganisha na mataifa mengine kama Kenya, Nigeria na mengineyo ya Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa na idadi ndogo ya watu wanaokwenda kusoma nje, sababu kubwa pamoja na mambo mengine ni kutokuwa na ufahamu kuhusu vyuo vya nje.

Aidha wapo wengine wana imani isiyo sahihi kwamba kusoma nje inamuhitaji mtu kuwa na fedha nyingi, imani ambayo sio kweli, kuna vyuo nchini ni gharama zaidi kuliko vya nje.

Kwa mfano baadhi ya kozi nje unaweza kusoma Shahada kwa maana ya ada na gharama za malazi kwa mwaka ni kati ya dola 3100 hadi 5000, sawa na Shilingi milioni sita hadi kumi. Hapa nchini kuna shule hutoza ada ya dola 5000 (zaidi ya milioni kumi za Kitanzania) kwa mwaka kwa elimu ya msingi au sekondari.Mkakati wa kuielimisha jamii kuhusu vyuo vya nje

Ni kutokana na kuonekana kwamba Watanzania wengi wanahitaji ufahamu zaidi kuhusu vyuo vya nje, Kampuni ya Global Education Link (GEL) ilianzishwa, lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha inawasaidia Watanzania kuwapa maelezo sahihi kuhusu vyuo vya nje na mwongozo mzima kuhusiana na uchaguzi sahihi wa masomo.

“Nimesoma nje na nimekuwa nikiona tofauti iliyoko ya kwenda nje kati ya vijana wa Kitanzania na wenzetu wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki, ndipo mwaka 2006 nikalazimika kuanzisha GEL, na sasa nimekuwa nikiendesha maonyesho katika mikoa mbalimbali ili kutoa fursa ya watu kupata ufahamu zaidi kuhusu uchaguzi sahihi wa kozi za kusoma pamoja na namna gani mtu anaweza kusoma nje,” alisema Abdulmalik Mollel katika mahojiano na mwandishi wa makala hii.

Kwa mujibu Mollel, nje ya kuanzisha kampuni ambayo ina makao yake makuu Dar es Salaam, pia imefungua matawi katika mikoa ya Mbeya, Dodoma, Mwanza na Zanzibar. Lakini pia imeanzisha mkakati wa kufanya maonyesho mikoani.

“Tumekuwa na maonyesho ya vyuo vikuu vya nje katika mikoa tofauti mfululizo, tulianza na Dodoma, Mbeya na kisha jana tulianza hapa Arusha, na tunatarajia maonyesho haya yatamaliza leo,” alisema Mollel na kuongeza kuwa mwitikio umekuwa mzuri kwa Watanzania wengi kufurika kwenye maonyesho.

Maonyesho kama hayo pia yanatarajiwa kufanyika Zanzibar na Mwanza mapema mwakani, azma kubwa ikiwa ni kuwa ni kutumia maonyesho hayo kama jukwaa la kuelezana kuhusu mwongozo wa kusoma nje ya nchi, uchaguzi sahihi wa kozi za kusoma na kila kitu kinachohusu namna gani mtu anaweza kusoma nje.

Baadhi ya Watanzania waliofurika kwenye maonyesho hayo wameelezea kufurahishwa kwao huku wakisema kama mpango kama huo ungekuwepo miaka mingi ya nyuma, huenda sasa Tanzania ingekuwa na maendeleo makubwa kiviwanda na uchumi kwa ujumla.

“Mimi nimesoma nje, nafahamu kwa kina umuhimu wa kusoma nje ya nchi. Ukweli wenzetu wako juu sana katika teknolojia, wana vifaa vya kufundishia na wanafundisha zaidi kwa vitendo kuliko sisi, haya ni baadhi ya mambo yaliyosababisha wazazi wangu walinipeleka nje kusoma na sasa nimerudi nchini, ni kati ya maofisa katika taasisi fulani,” alisema Othman Mohammed akiwa katika viwanja vya Kumbukumbu ya Azimio la Arusha ambako maonyesho ya vyuo vya nje yanaendelea.Kuhusu Maonyesho ya Arusha

Maonyesho hayo makubwa ya vyuo vya nje yalianza jana tarehe 21 Disemba na yatamalizika jioni ya leo tarehe Disemba 22 katika uwanja wa Makumbusho ya Azimio la Arusha.

Kwa mujibu wa Meneja wa Global Education Link (GEL) tawi la Arusha, Regina P. Lema uwanja huo ambao maonyesho yatafanyika unatazamana na Mnara wa Mwenge.

“GEL ndio tunaoendesha maonyesho haya kwa kushirikiana na vyuo vya nje ambavyo baadhi yao tayari vimeshatuma wawakilisha wao. Maana yake ni kwamba watu watapata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi wa GEL au hao wawakilishi waliotoka nje ili kupata ufahamu mpana zaidi kuhusiana na suala la kusoma nje,” alisema.

Regina alifafanua kuwa baadhi ya vyuo ambavyo vimetuma wawakilishi watakaoshiriki maonyesho hayo ni Lovely Professional University, Sharda University, Chandigarh University na Maharishi Markandeshwar University vyote vya nchini India.

“Nawakaribisha watu wa Arusha na vitongoji vyake kuja kujionea masuala ya namna ya kusoma nje ya nchi, pamoja na uchaguzi wa kozi za kusoma,” aliongeza Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel na kufafanua kuwa lengo la maonyesho hayo ni kufahamishana kozi mbalimbali zinazotolewa nje ya nchi.

“Kuna kozi za kila aina zikiwamo za injinia katika masuala mengi tofauti yakiwamo ya petroli na gesi. Pia kozi za biashara, masoko, afya, udaktari, madini, uchumi na nyingine nyingi,” aliongeza na kufafanua kuwa vyuo ambavyo mtu anaweza kupatiwa maelezo katika maonyesho hayo ni vya nchi nyingi tofauti duniani vikiwamo vya China, Malaysia, India, Canada, Marekani, Australia, Uingereza, Afrika Kusini na Ukraine.Kulingana na Mollel katika maonyesho hayo wanaotaka kusoma nje wanaweza kujaza fomu hapohapo kwenye maonyesho kwa ajili ya kuanza masomo Mwaka 2017 ikiwamo mwezi Januari, Februari, Machi na kuendelea kulingana na matakwa ya mwombaji.

“Wengi wamekuwa wakitaka kusoma nje, lakini baadhi wamekuwa wakishindwa kuwa na uchaguzi sahihi za nini cha kwenda kusoma, kwa hiyo kupitia maonyesho haya tutakuwa tunatoa ufafanuzi wa kozi mbalimbali,” alisema Mollel.

Waliomaliza kidato cha nne, sita na vyuo mbalimbali ni baadhi ya wale ambao wanaweza kuunganishwa na GEL kusoma vyuo vya nje ya nchi.

GEL ni kampuni iliyosajiliwa Mwaka 2006 kwa lengo la kufanya shughuli za uwakala wa vyuo vya nje. Hadi sasa imeweza kuwaunganisha Watanzania zaidi ya 5400 na vyuo mbalimbali Duniani vikiwamo vya Marekani, Canada, Uingereza, Ukraine, China na India.

Serikali yathamini mchango wa Global Education Link, yaitunuku nishani ya uzalendo

Mchango wa Global Education Link (GEL) umekuwa ukithaminiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na Serikali.

Wiki iliyopita Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Stadi, Profesa Joyce Ndalichako ameitunuku nishani ya uzalendo kampuni ya Global Education Link (GEL) kutokana na mchango inaotoa katika maendeleo ya elimu nchini.

Nishani hiyo aliitoa wakati akizindua mkutano mkuu wa 11 wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchini (TAHOSSA) mkoani Dodoma.

Rais wa TAHOSSA, Bonus Nyimbo alisema GEL imekuwa mdau mkubwa katika kusaidia shughuli za TAHOSSA na masuala mengine muhimu katika maendeleo kwa ujumla nchini.

“Tunaipongeza sana Global Education Link, kwani wamekuwa karibu na jamii, wamekuwa karibu na sekta ya elimu na maendeleo ya nchi kwa ujumla,” alisema Katibu Mkuu wa TAHOSSA Diana Matemu.

Global Education Link ni kampuni iliyoanzishwa Mwaka 2006 kwa lengo la kuwaunganisha watu na vyuo vya nje. Tangu imeanza hadi sasa imewaunganisha Watanzania 5400 na vyuo mbalimbali vilivyoko Marekani, Canada, India, Malaysia na China.

No comments: