Thursday, November 10, 2016

RC GAMBO AONGOZA KIKAO CHA KWANZA CHA KAMATI YA AMANI





Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo akifungua Kikao cha kwanza cha Kamati ya Amani ya viongozi wa dini Mkoa kilichofanyika Ofisini.





Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Arusha Bi. Jacquline Kapila akielezea kazi za Taasisi yake kwa viongozi wa Dini kwenye kikao cha kamati ya Amani. 



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo akiongea na viongozi wa Dini wakati wa Kikao cha Kamati ya Amani.




ASKOFU Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mkoani Arusha, Solomon Masangwa akioelezea mchango wa viongozi wa Dini katika kuhamasisha amani.

Sheikh Mkuu wa Bakwata mkoa wa Arusha, Shabaan Juma akichangia kwenye Kikao cha Kamati y Amani kwa kawataka wananchi kudumisha amani na kujenga utamaduni wa kuvumiliana.

Askofu Dr. Leornard Mwizarubi wa Kanisa la SAYUNI EAG (T) akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Amani na kumshkuru RC Gambo kwa kikao hicho na kushauri Kamati hii ikutane mara kwa mara ili kushirikiana kwa karibu na Serikali kutatua kero za wananchi.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Arusha Ndg. Apili Mbaruku akijibu hoja za viongozi wa dini wakati wa Kikao cha Kamati ya Amani.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo(kushoto) katika mazungumzo na ASKOFU Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati (KKKT) Mkoani Arusha, Solomon Masangwa baada ya Kikao cha Kamati ya Amani.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo(katikati) katika Picha ya pamoja na Viongozi wa Dini waliohudhuria Kikao cha Kamati ya Amani.



Nteghenjwa Hosseah – Arusha 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Mashaka Gambo amekutana na kamati ya Amani ya Mkoa ambayo inajumuisha viongozi wa dini mbalimbali zilizoko katoka Mkoa huu kuzungumzia mustakabali wa Amani na namna viongozi hawa wa dini watashirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo kwa wananchi ambao ni waumini wao.

Akizungumza katika Kikao hicho Mhe. Gambo alisema kazi ya Ulinzi wa Amani itakua rahisi sana kupitia viongozi wa dini ambao wana karama ya kuongea na kubadilisha maisha ya watu bila kutumia nguvu ama kuwashurutisha isipokua kwa chakula cha roho ambacho hujenga misingi imara ya imani na tabia njema.

Maendeleo ya wananchi hayawezi kupatikana bila Amani kuwepo katika Mkoa wetu ni lazima tusaidiane katika hili dhamira yetu ifanikiwe kwa wepesi zaidi tuna Imani kubwa sana Na viongozi wetu wa dini na ndio maana nikaona ni vyema tukakutana ili tusikie kutoka kwenu ninyi ambao mnawakilisha kundi kubwa la wananchi na pia kufahamu kero mbalimbali zinazowakwaza wananchi katika maeneo yenu alisema Gambo.
 
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati KKKT Solomon Masangwa akichangia kuhusu masuala yanayoweza kuhatarisha amani alisema kundi ambalo linatakiwa kuangaliwa kwa jicho la Tatu na litasaidia sana katika ulinzi wa Amani ni waendesha boda boda pamoja na wanachinga ambao kwa sasa wanaonekana kutopewa kipaumbele au hatuwajali kwa kiasi kinachostahili.

Tunapaswa kuangalia namna gani watu wanaofanya shughuli hizi wanakua rasmi kwa kupatiwa maeneo maalumu pamoja na utambulisho utakaowawezesha kufanya kazi zao kwa Amani na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na si kama walivyo sasa wanafanya kazi hizo katika maeneo yasiyo rasmi na kuhama kila siku hali hii ina wafanya wajihisi kama si sehemu ya Taifa hili hivyo wanaweza kutumika kiurahisi kuhatarisha amani ya Nchi yetu alisema Masangwa.

Akichangia katika viashiria vya uvunjifu wa amani Askofu Dr. Leornard Mwizarubi wa Kanisa la SAYUNI EAG (T) alisema ni vyema Serikali ikajikita katika kutatua changamoto zinazoathiri maisha ya kila siku ya wananchi ili hata sisi viongozi wa dini tunapoongea na waumini tuwe na vielelezo dhabiti vya kuonyesha namna ambavyo Serikali kero zao zimeshughulikiwa.

Aliendelea kusema “Katika eneo ambalo ninatoa huduma ya Kiroho kwenye Kata za Unga Ltd, Sokoni 1, Daraja II, Sinoni na maeneo ya jirani wakazi wa mitaa hiyo wanapata shida sana ya huduma ya maji Taka na hata katika Kanisa langu inanilazimu kutafuta gari la kunyonya maji taka mara tatu kwa wiki ili kufanya mazingira kuwa safi, sasa kuna maeneo mengine wananchi hao hawana uwezo wa kutafuta gari hilo la kunyonya maji taka hivyo wanaishia kulalamika kwa kuishi katika mazingira machafu”.

Aidha Sheikh Mkuu wa Bakwata mkoa wa Arusha, Shabaan Juma alishkuru Sekretariet ya Mkoa kwa kikao hiki muhimu kwa ustawi wa jamii ya Arusha na kueleza kuwa katika kipindi hiki cha Mpito Nchi yetu inahitaji maombi ya bila kikomo ili kuweza kuvuka salama na tunategemea kuendelea kuona mabadiliko katika kila eneo; Tunaamini si wote wanafurahia mabadiliko haya hivyo tuna wajibu wa kuwajulisha waumini wetu kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya mifumo katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano na faida zitakazo patikana kwa Taifa.
 
Akiwasilisha changamoto katika upande wake Sheikh Shaaban alisema “Kuna ukuaji wa kasi ya makazi holela katika Jiji la Arusha, Utaratibu wa mipango miji hauzingatiwi na hii inasabisha maeneo mengi kutopitika kwa urahisi hivyo hata itakapotokea dharua sio tahisi kwa wananchi wetu kupata msaada wa haraka, tunaomba wanachi wapimiwe maeneo yao, barabara zifunguliwe ili huduma muhimu ziweze kufika katika maeneo hayo”.

Mkurugenzi wa Idara ya maji safi na maji Taka (AUWASA) Eng. Ruth Koya alisema Taasisi yake inaanza utekelezaji wa Mradi mkubwa wa maji safi na Taka ambao matatizo yote yaliyowasilishwa katika kikao hiki yanayohusiana na maji yatashughuliwa kupitia mradi huo. Aliongeza kuwa mradi huo utahusisha uboreshaji wa mioundombinu ya maji safi, Uhamishaji wa mabwawa ya maji Taka(yaliyokuwa Lemara kwa hivi sasa), ununuzi wa magari ya kunyonyea maji machafu pamoja na magari ya kusambaza na kuuza maji safi.

Mkuu wa Mkoa Mge. Gambo alitolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizowasilishwa na kuelezea namna ambavyo Changamoto ya Mipango Miji ilivyopata ufumbuzi kupitia ukamilishaji wa Mpango Mkakati wa Jiji la Arusha (Master Plan) na kuwajulisha wajumbe kuwa mpango umekamilisha na umekwishapitiwa na Halmashauri zote tatu zinazohusika, hivyo kwa hivi sasa utawasilishwa Wizarani na taratibu zote zikikamilika utekelezaji utaanza mara moja.Kuhusu suala la Machinga na waendesha boda boda boda Rc Gambo alisema Serikali imekwisha anza utaratibu wa kutafuta maeneo salama na rafiki kwa ajili ya wafanyabishara ndogondogo maarufu kama machinga na tutaongea nao ili tuwe na makubalino ya pamoja.

Aidha kuhusu bodabdoa tumeanza kuwatambua kupitia kwenye uongozi wa mitaa na vituo vyao na tutahakikisha tunaboresha mazingira yoa ya kufanyia kazi na zaidi tunawatafutia Pikipiki ambazo watapewa Vijana wanaofanya biashara ya boda boda kwa utaratibu maalumu; Itawapasa kurudisha Fedha za Pikipiki tu na kisha kupata umiliki halali ya Chombo hicho tofauti na sasa hivi ambapo wanapewa pikipiki hizo na kulipa mara mbili ya bei kwa matajiri wao ndipo wapate Umiliki alimalizia Gambo.

No comments: