Thursday, November 10, 2016

UMOJA WA MATAIFA WAISHUKURU SERIKALI YA TANZANIA


Na Mwandishi Maalum, New York


Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena, umeishukuru Serikali ya Tanzania kwa kusaidia kwa hali na mali ujenzi na hatimaye kuelekea ukamilishwaji wa Majengo mapya ambayo yatatumika kwa shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) ambayo ilihitimisha majukumu yake mwaka jana.

Shukrani hizo zimetolewa siku ya jumatano na Bw.Theodor Meron, ambaye ni Rais wa Mahakama za Kimataifa za Kesi za Masalia na Utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka zote muhimu za zilizokuwa Mahakama za Kimataifa zilizoshughulikia mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda na Yugoslavia ya zamani ( IRMCT).

Bw. Theodor Meron alikuwa akiwasilisha Ripoti yake ya Nne kuhusu IRMCT mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa . Ripoti ambayo imeanisha maendeleo ya kipindi cha mpito kutoka ICTR na ICTY kwenda IRMCT kazi ambayo amesema inakwenda vizuri ingawa kumekuwapo na changamoto kadhaa.

“Wakati ninapowasilisha ripoti hii, nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa mchango mkubwa na ushirikiano ambao tumeupata kutoka serikali ya Tanzania, takribani wiki tatu zijazo majengo hayo yatazinduliwa rasmi baada ya kuwa yamekamilika”. Akasema Bw. Meroe

Baadhi ya changamoto hizo kwa upande wa iliyokuwa ICTR ni pamoja na kutokamatwa hadi sasa kwa watuhumiwa watatu ambao inaelezwa wapo mafichoni. Ni pili ni mahali pa kuwapeleka watu ambao ama wamekwisha maliza kutumikia vifungo vyao na kuachiwa huru. Watu hao wamekosa nchi ya kuwapokea na hadi sasa bado wanaendelea kuishi nchini Tanzania.

Na kwa sababu hiyo, Rais wa IRMCT ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa ushirikiano wa kuwachukua watu hao ambao hawana mahali pa kwenda na kwa wale walioko mafichoni nchi ambazo wamejificha watoe ushirikiano kwa kuwafichua na kuwakamata ili hatimaye sheria iweze kuchukua mkondo wake

Kwa upande wake, Tanzania kupitia Mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amesema Tanzania inakaribisha kuhitimishwa kwa ujenzi kwa ujenzi wa makazo mapya ya iliyokuwa ICTR katika eneo la Lakilaki ndani ya wakati na kwa bajeti iliyopangwa.

“Kwa namna ya pekee tunampongeza Msajili wa Mahakama, Bw. John Hopkins kwa uongozi wake na ushirikiano wake ambao umewezesha kukamilisha hatua hii muhimu sana”. Akasisiza Balozi.

Aidha kukamilika kwa majengo hayo na ambayo yapo katika ardhi ya Tanzania ni heshima na fahari kubwa na ya kipekee kwa Tanzania na wananchi wake kutokana na jukumu kubwa iliyobeba ya kuwa mwenyeji wa Mahakama ya Kimataifa ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda kwa niaba ya Jumuiya ya Kimataifa. 

Balozi Manongi pia amepongeza uratibu uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Mshauri wa Sheria, Ofisi ya Msajili na the Hegue ya kuhakikisha kwamba, pamekuwapo na utaratibu mzuri wa kurithishana kutoka ICTR kwenda IRMCT. Na kwamba kazi hiyo haikuwa nyepesi.

Akizungumzia kuhusu kazi za IRMCT, Balozi amesema, Tanzania ingependa kuona Taasisi za Kitaifa zinawezeshwa ili ziweze kushughulikia kwa ukamilifu, haki na usawa na kwa kuzingatia sheria za kimataifa kesi zinazopelekwa kwenye Taasisi hizo za kitaifa.Aidha akasema uzoefu ambao umepatikana kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na ICTR pamoja na ile ya ICTY ni vema ukatumika kama mfano katika Mahakama nyingine za Kimataifa.

Kwa upande wa mashahidi, Tanzania imesisita umuhimu wa mashahidi kulindwa na kuhakikishiwa usalama wao dhidi ya vitisho mara baada ya kutoa ushahidi.Kuhusu watu walioachiwa huru baada ya kukamilisha vifungo vyao na bado wapo nchini Tanzania. Tanzania imeungana na wazungumzaji wengine katika mkutano huo wa kutaka pawepo na majadiliano ya kina ya kuangalia namna gani ya kuwasaidia watu hao.

Vile Tanzania imetoa wito kwa nchi zile ambazo zinahisiwa kwamba zinawahifadhi watuhumiwa watatu ambao wapo mafichoni na wanatakiwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kutoa ushirikiano ili hatimaye haki itendeke.Watuhumiwa ambao wametajwa kuwa walihusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji ya Kimbari nchini Rwanda na wapo mafichoni hadi sasa ni Augustin Bizimana, Felicien Kabuga na Proitas Mpiranya. 

Kwa mujibu wa Ripoti iliyowasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, watuhumiwa hao watakapopatikana kesi zao zitafanyika katika Mahakama hiyo mpya nchini Tanzania.Uamuzi kwa kuwa na matawi ya IRMCT huko Arusha na the Hague, Uholanzi unatokana na maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio nambari 1966 la mwaka 2010.

Kupitia Azimio hilo Baraza la Usalama liliamua kwamba, baada ya kumalizika rasmi kwa ICTR ( 2015) na ICTY ( 2017) Tanzania ambayo ndiyo ilikuwa mwenyeji wa ICTR itapewa jukumuu la kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka zote muhimu za iliyokuwa ICTR ikiwa ni pamoja na kumalizia kesi zitakazokuwa zimebaki. Huku the Hague ikiwa na dhamana hiyo hiyo kwa kazi zilizokuwa za iliyokuwa ICTY.

Mahakama za Kimataifa za Rwanda na Yugoslavia ambazo zimefanya kazi kubwa ya kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa karibu wote waliohusika na matukio ya kutisha ya ukiukwaji wa haki za binadamu ziliazishwa mwaka 1990 na Umoja wa Mataifa.
.Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Ripoti ya utendaji kazi wa IRMCT ambapo alimshukuru kwa namna ya pekee Msajili wa IRMCT Bw. John Hopkins kwa uongozi wake na ushirikiano ambao ameonyesha katika ujenzi wa majengo mapya huko Lakilaki lakini pia katika kusimamia kipindi cha mpito na makabidhiano kutoka ICTR kwenda IRMCT.
Rais wa IRMCT, Bw. Theodor Meron akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hapo siku ya jumatano, Ripoti ya utendaji kazi wa Matawi ya Mahakama za Kimataifa za Kesi za Masalia zinachokua nafasi ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) na Mauaji ya halaiki yaliyotokea katika iliyokuwa Yugoslavia ya zamani ( ICTY. Bw. Meron alitumia pia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa hali na mali katika ujenzi wa majengo yanayochokua nafasi ya ICTR majengo hayo yamejengwa katika eneo la Lakilaki Mkoani Arusha.

No comments: