Monday, October 24, 2016

UDSM YATAKIWA KUHAKIKISHA INAENDELEA KUWA CHUO KIKUU KIONGOZI



Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na washiriki wa kongamano la kuazimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho mapema hii leo Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Mhadhiri wa Heshima Prof. Tade Aina toka nchini Nigeria akielezea hali ya vyuo vikuu vya Afrika katika muktadha wa Kimataifa wakati wa kongamano la kuazimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho mapema hii leo Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa kongamano maalum la kuazimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakimsikiliza kwa makini Mhadhiri wa Heshima Prof. Tade Aina toka nchini Nigeria wakati akielezea hali ya vyuo vikuu vya Afrika katika muktadha wa Kimataifa mapema hii leo Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akifurahia jambo na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba (kushoto) wakati wa kongamano la kuazimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mapema hii leo Chuoni hapo, katikati ni Mhadhiri wa Heshima Prof. Tade Aina toka nchini Nigeria.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Wakuu wa Vitivo wa Chuo hicho wakati wa kongamano la kusherehekea kutimiza miaka 55 toka kuanzishwa kwa chuo hicho.

Picha na Eliphace Marwa – Maelezo

……………………………………………………….

Na: Frank Shija, MAELEZO.

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) takiwa kuhakikisha Chuo hicho kinaendelea kuwa kiongozi miongoni mwa Vyuo Vikuu nchini.

Ushauri huo umetolewa na Rais mstaafu wa awamu ya Nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akifungua maadhimisho ya miaka 55 ya chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.

“Hiki ndicho Chuo kiongozi kati ya Vyuo Vikuu vyote hapa nchini, mnatakiwa kuhakikisha kinaendelea kuwa kiongozi huku Vyuo vingine vikifuatia”. Alisema Dkt. Kikwete

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Lwekaza Mukandara amesema kuwa pamoja na changamoto zinazo kikabili chuo hicho wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kusaidia katika kuleta maendeleo ya chuo hicho.

Alisema kuwa baadhi ya changamoto zimetatuliwa kwa pamoja kati ya Serikali na wahisani ambapo alisema kuwa ujenzi wa kumbi mpya za mihadhara, Maabara za Kisasa na jengo la malazi,pamoja na ujenzi wa hosteli za wanafunzi unaoendelea katika Kampasi ya Julius K. Nyerere ambayo itakuwa na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 4000 mara itakapo kamilika.

Akiwasilisha mada juu ya “hali ya Taaluma Barani Afrika katika Muktadha wa Kimataifa” Mhadhiri wa Heshima kutoka nchini Nigeria, Profesa Tade Aina amesema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni moja kati ya Vyuo Vikuu mahiri barani Afrika ambapo kimetoa mchango mkubwa kwa ukombozi wa nchi nyingi za bara hili.

Aliongeza kuwa yeye binafsi ni mnufaika mkubwa wa UDSM kwani amekuwa na ushirikiano mkubwa na baadhi ya wahadhiri kutoka chuo hicho katika masuala mbalimbali ya taaluma.

Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wakati wa uwasilishaji mada alisema kuwa kipindi Chuo hiki kinaanzishwa aina ya masomo yaliyokuwa yanafundishwa chuoni hapo yalikuwa na muelekeo kuandaa wafanyakazi wa Serikali kwa wakati huo.

Na kuongeza kuwa muelekeo wa aina ya masomo uliendelea kubadilika kadri ya siku zilivyokwenda kutokana na mabadiliko ya teknolojia na uhitaji wa soko la ajira.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaadhimisha miaka 55 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1961 kikiwa ni tawi la Chuo Kikuu cha London, ambapo awali kilianzia katika mtaa wa Lumumba kikiwa na wanafunzi 14 kabla ya kujengwa mahali kilipo sasa katika eneo la Mlimani.

No comments: