Monday, October 24, 2016

WAZIRI WA FEDHA DK MPANGO AMWAKILISHA RAIS MKUTANO WA TANO WA USHIRIKIANO KATI YA NCHI ZA KIAFRIKA NA KOREA KUSINI

MKUTANO wa Tano wa Ushirikiano kati ya Nchi za Kiafrika na Korea Kusini (Korea-Africa Economic Cooperation (KOAFEC), Umefunguliwa leo Jijini Seoul, Korea Kusini, huku agenda kubwa ikiwa ni kuzungumzia namna nchi za Kiafrika zinavyoweza kutumia kilimo katika muktadha wa maendeleo ya  viwanda ili ziweze kujikwamua haraka kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, anawakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) katika mkutano huo unahusisha nchi 54 za kiafrika na nchi ya Korea Kusini.

Dkt. Mpango ameuelezea mkutano huo ulioandaliwa na Serikali ya Korea Kusini kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya EXIM ya nchini humo, kwamba utaleta mapinduzi makubwa katika nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kilimo, rasilimali watu na teknolojia ya habari na Mawasiliano-TEHAMA.

Amesema kuwa nchi ya Korea Kusini ilipata uhuru mwaka mmoja na nchi ya Ghana, Mwaka 1954 miaka michache kabla ya Tanzania Bara kupata uhuru wake, lakini imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kuwa moja kati ya nchi za  ulimwengu wa kwanza kiuchumi, lakini Ghana na Tanzania bado ni nchi masikini.“Ni jambo zuri kwamba tuimarishe ushirikiano na Korea Kusini ili njia walizotumia kupiga hatua kubwa kimaendeleo, na sisi tuweze kujifunza kwa haraka” alifafanua Dkt. Mpango

Amesema kuwa Baadhi ya Mawaziri wenzake wa Fedha aliozungumza nao wanaokuwa uongozi thabiti wa nchi na uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu na kilimo cha kisasa, vinaweza kuzikwamua nchi za Kiafrika kuondokana na umasikini.

“ Ni muhimu sana elimu na ujuzi tuyasisitize tunapoanza hatua ya kujenga Tanzania mpya kwa nguvu zaidi lakini jambo linguine ni ukweli kwamba kilimo ndio msingi ambao watu wetu wengi wako huko wanaishi kwa kutegemea kilimo kwa hiyo mkutano huu unaendana kabisa na mkakati wetu  wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa” alisema Dkt. Mpango

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utafutaji rasilimali kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sabra Issa Machamo, amesema kuwa uhusiano wa Zanzibar na Korea Kusini ni wa kuigwa ambapo nchi hiyo inafadhili mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji unaotarajiwa kujengwa visiwani humo.

Akifungua Mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Fedha wa Korea Kusini II Ho YOO (ILU Ho Yuu), amesema kuwa serikali yake imeamua kuwekeza kiasi kikubwa cha rasilimali zake kuendeleza nchi za Afrika kupitia sekta za kilimo, rasilimali watu na viwanda.

Amesema mkazo mkubwa utakuwa kuishirikisha sekta binafsi kusisimua uchumi wa nchi zinazonufaika na mpango huo ili kuharakisha maendeleo ya nchi hizo.“Hatua hii itachangia sana kupunguza umasikini uliokithiri pamoja ja kuzalisha ajira nyingi ambazo zitaleta matumaini kwa kizazi za vijana” Alisema Yoo.

Bw. Yoo amesema kuwa katika miongo miwili iliyopita, nchi za kiafrika zimapiga hatua kubwa katika nyanza za afya, elimu na mambo mengine kadha wa kadha lakini akaonya kuwa matukio ya uvunjifu wa Amani na mizozo ya kivita vinakwaza maendeleo ya nchi hizo.

Naye Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika, Akinwumi Adesina, amesema kuwa benki yake hivi sasa imeelekeza nguvu zake katika vipaumbele vitano ambavyo baadhi yake ni kuimarisha kilimo biashara kitakacholisha Afrika, kuboresha miundombinu ya sekta ya umeme, viwanda na kuiunganisha Afrika kiuchumi na kiuwekezaji, kuboresha huduma za jamii kama vile maji, chakula, usafi wa mazingira na mambo mengine kama hayo.

Mkutano wa tano wa KOAFEC mwaka huu umebeba kaulimbiu ya kuibadili Afrika kwa njia kilimo na mpango jumuifu wa watu unaolenga kuimarisha sekta ya fedha kwa njia ya mitandao ya simu” (Transforming Africa’s Agriculture through Industrialization and Inclusive Finance) 

No comments: