Monday, October 24, 2016

WAZIRI LWENGE AHIMIZA KUKAMILIKA KWA MRADI WA VISIMA KIMBIJI NA MPERA

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, ameiagiza Kampuni ya Serengeti Limited kukamilisha mradi wa uchimbaji visima 20 vya maji vya Kimbiji na Mpera kwa muda waliokubaliana, vinginevyo itabidi ilipe gharama za ucheleweshaji kama itashindwa.

Alisema serikali haitavumilia kuona mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Jiji la Dar es Salaam unachelewa kukamilika, kwa sababu unahitajika kuhudumia wananchi kwa kuwapatia huduma ya majisafi na salama. 

Waziri Lwenge alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, baada ya kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo mkubwa uliopo Kigamboni, Dar es Salaam ulioanza kutekelezwa tangu mwezi Machi, 2013.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akipokea maelezo ya ramani ya mradi wa uchimbaji visima vya Kimbiji na Mpera kutoka kwa Mhandisi Mkazi wa mradi, Injinia Charles Kaaya.

Alisema mradi huo utagaharimu zaidi ya Sh. bilioni 18, na serikali imeshalipa kwa mkandarasi zaidi ya Sh. bilioni 13, na ulitegemewa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu, lakini utachelewa kutokana na changamoto mbalimbali alizotaja mkandarasi huyo.

“Pamoja na changamoto alizozitaja mkandarasi, hatutakubali utekelezaji wa mradi huu uendelee kuchelewa, mkandarasi inabidi aongeze kasi ili tumalize kero ya wananchi wa Kigamboni, Mkuranga na Dar es Salaam yote, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri mradi huu, hatutavumilia uchelewaji zaidi na itabidi walipie gharama endapo watashindwa”, alisema Inj. Lwenge.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Serengeti, Mehrdad Talebi (kushoto), Mhandisi Mkazi wa mradi, Charles Kaaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), Archad Mutalemwa na Mkurugenzi wa Maji Mijini, Mhandisi Dkt. Justus Rwetabula.

Alisema mradi umetekelezwa kwa asilimia 56 hadi sasa, visima nane vikiwa vimekamilika, huku vingine saba vikiwa katika hatua mbalimbali za uchimbaji na vitano vikiwa havijaanzwa kazi ya uchimbaji.

Wakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Limited, Mehrdad Talebi alikiri kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kama mkataba unavyosema, kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kazi na kuahidi ifikapo Machi, 2017 watakuwa wamekamilisha kazi hiyo.
Mashine ikiendelea na kazi ya uchimbaji kisima Kimbiji.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), Archad Mutalemwa, alisema mradi huo hautakamilika kulingana na makubaliano ya awali, lakini ana imani na kukamilika kwa kazi hiyo mara baada ya kutatua changamoto za mkandarasi, ikiwemo kupatikana kwa vifaa vya kazi.

Uchunguzi wa awali ulionyesha uwepo wa maji mengi na safi katika maeneo ya Kimbiji na Mpera. Hivyo, ikaamuliwa visima kati ya 20-40 vichimbwa kwenye maeneo hayo na vinategemwa kuchangia hadi asilimia 30 ya mahitaji ya maji ya Dar es Salaam, mji unaotarajiwa kuwa na watu wapatao milioni 7.59 ifikapo mwaka 2032.

Ili kukabiliana na tatizo la maji kati ya sasa na hadi mwaka 2032, visima 12 vitachimbwa maeneo la Kimbiji na 8 maeneo ya Mpera. Visima hivi vitakuwa na kina cha hadi mita 600 na vinategemewa kuzalisha lita za ujazo 260,000 kwa siku.
Baadhi ya mafundi wakiwa eneo la kazi Kimbiji.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akionja maji yaliyopatikana katika kisima namba K17.
Mhandisi Mkazi wa Mradi wa uchimbaji visima vya Kimbiji na Mpera, Charles Kaaya (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi na Ufundi ya Bodi ya DAWASA, Prof. Felix Mtalo (katikati) na Waziri Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge.

No comments: