Tuesday, October 4, 2016

BENKI YA MKOMBOZI YAKABIDHI MSAADA WA MADAWATI SHULE YA MSINGI NGARAMA

Na Editha Karlo wa blog ya jamii,Kagera

MKOMBOZI Commercial Bank ambayo ni moja ya benki zinazokuwa kwa kasi nchini, jana imekabidhi madawati mia moja(100) kwa shule ya  Msingi Ngarama ikiwa ni katika juhudi za kuunga mkono wito wa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wa kuchangia madawati mashuleni.

Madawati hayo yalikabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bibi  Edwina A. Lupembe katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya  shule hiyo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo ambaye alipokea rasmi madawati hayo.

Akikabidhi madawati hayo Mkurugenzi  wa banki hiyo Edwina Lupembe  alisema wao kama benki wameguswa na tatizo hili la madawati na kuona ni jambo la busara kuchangia ili watoto waweze kusoma bila matatizo.

“Sisi Benki ya Biashara ya  Mkombozi tunathamini sana elimu na tunaunga mkono jitihada mbalimbali za serikali za kuboresha elimu hasa katika hili la madawati ambapo hapo nyuma tulishuhudia wanafunzi wengi wakikaa chini. Wahenga walisema; Kama mpango mkakati wako ni wa mwaka mmoja panda mpunga kama mpango wako ni  wa miaka kumi panda miti lakini kama mpango mkakati  wako ni wa miaka 100 somesha watoto. Wote tutakubaliana kuwa mpango mkakati wa selikali yetu katika elimu ni wa miaka 100.” alisema.

Alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa uongozi wa shule hiyo kuhakikisha madawati hayo yanatumiwa vizuri ili wanafunzi wengi zaidi waweze kufaidi, na kwa wanafunzi aliwataka wafanye bidii katika masomo yao kwani sasa mazingira ya kusomea yatakuwa bora zaidi na kwamba elimu ni ufunguo wa maisha bora.

Bibi  Lupembe alisema mbali na mchango katika jamii, benki yake imekuwa katika mstari wa mbele kuanzisha huduma ambazo zinalenga kuwasaidia wananchi hasa wenye kipato cha chini kama vile huduma ya mikopo ya Mfuko wa Bima ya Afya kwa wakopaji wa vikundi.

“Huduma hii ni endelevu  na napenda kutoa rai kwa wazazi na walimu waliopo hapa wajiunge katika huduma ya mikopo ya  vikundi inayotolewa na Benki ya Biashara ya Mkombozi kupitia tawi lake la hapa Bukoba ambavyo vitawasaidia kupata mikopo hii ya Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa,alisema na kuongeza kuwa hii italeta afueni kubwa kwani wanafunzi pia wataweza kulipiwa kadi zao za matibabu kupitia bima za wazazi wao ambao watakuwa wamejiunga na vikundi vya mikopo kutoka Benki ya Biashara ya  Mkombozi.

Aliwaomba wakazi wa Kagera watembelee tawi la Benki ya Biashara ya  Mkombozi lililopo Bukoba Mjini ili wapate maelezo kamili kuhusu huduma hii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Benki ya Biashara ya  Mkombozi pia inatoa huduma ya akaunti maalumu kwa ajili ya wanafunzi (student account) ambayo aliwaomba wazazi kuwafungulia watoto wao ili iweze kuwasaidia  kutunza fedha sasa na hata baadaye wanapojiunga na masomo ya ngazi za juu zaidi kwani akiba haiozi.

Akiendelea aliongeza kuwa benki hiyo inatoa pia huduma ya kuchukua na kuweka fedha katika akaunti kupitia simu yako. Huduma hiyo inamwezesha mwenye akaunti kuchukua au kuweka fedha kwenye akaunti yake kupitia M-pesa, Airtel Money na Tigo pesa kutoka mahali popote Tanzania kwa masaa 24 siku zote za juma. Benki hii pia inaendesha akaunti ya Community kwa ajili ya asasi na Taasisi ambazo hazifanyi shughuli kibiashara bali hutoa huduma kwa jamii. Asasi hizi ni pamoja na NGOs, Shule, hospitali na Asasi zote za dini. Kama mchango wa benki kwa jamii, akaunti hii haina makato ya aina yoyote. Aliishauri shule kufungua akaunti yake mara moja.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawilo   aliishukuru Benki ya Mkombozi kwa mchango huo wa madawati na kusema utasaidia kuziba pengo lililokuwepo.

“Inatupa moyo kuona kuwa wito huu wa Rais umepokelewa vyema na mashirika mbalimbali kama Benki ya Biashara ya  Mkombozi na hii ni dalili kuwa sote tuna dira moja ya kutaka watoto wetu wafanikiwe katika masomo yao bila kupitia matatizo mengi,” alisema.

Alitoa rai kwa wanafunzi na walimu kulipa fadhila kwa kuwafundisha  watoto vizuri na watoto kusoma kwa bidii kwa kuhakikisha Mkoa wa Kagera unafanya vizuri ili misaada inayotolewa isiende bure.

Mkombozi Commercial Bank Plc ilianzishwa mwaka 2009 na kanisa Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha. 

Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine kuwekeza katika benki hiyo wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza nguvu.

Benki ya Biashara ya Mkombozi inayo matawi sita na vituo vya huduma za kibenki viwili. Matawi hayo yapo Dar es Salaam matatu na kituo cha huduma za kibenki kimoja, Mwanza, Moshi, Bukoba na kituo  cha pili cha huduma za kibenki kipo Morogoro.
 Mkurugenzi wa benki ya Mkombozi, Edwina Lupembe akikabidhi msaada wa madawati 100 kwa shule ya msingi Ngarama Wilayani Karagwe kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mjini
 Viongozi wa Wilaya ya Karagwe na viongozi wa banki ya mkombozi wakiwa wamekaa kwenye moja ya dawati yaliyotolewa msaada na banki ya mkombozi kwa shule ya msingi Ngarama.
  Wanafunzi wa shule msingi Ngarama wakifurahia madawati waliyopewa msaada na banki ya mkomboz

 Wanafunzi wa shule ya msingi Ngarama wakibeba madawati yao waliyopewa msaada na banki ya mkombozi

No comments: