Thursday, October 6, 2016

BENKI YA DUNIA KUIPIGAJEKI TANZANIA RUZUKU NA MKOPO WENYE MASHARTI NAFUU DOLA BLN 1 NUKTA 6

ben1
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philiph Mpango akifurahia jambo na Bi. Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi Mkazi anayeiwakilisha Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia wakati wakisubiri kuingia kwenye mkutano Jijini Washington DC.(Picha zote na Wizara ya Fedha na Mipango)
ben2
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James akisalimiana na Bi. Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anaewakilisha benki hiyo katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia akiwa pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Jijini Washington DC.
ben3
Bi. Bella Bird, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anaewakilisha Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia akifafanuliwa masuala mbalimbali ya Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Dotto James (kulia) pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango(katikati) Jijini Washington DC.
ben4
Kaimu Kamishna wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati na Petroli Bw. James Andilile akimweleza Kaimu Kamishma wa Sera Bw. Agustine Ollal (kushoto) na Kamishna wa Bajeti Bw. John Cheyo (kulia) kuhusu Tanesco inavyopiga hatua katika uimarishaji wa nishati kwa wananchi, wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na IMF unaoendelea Jijini Washington DC, Marekani.
ben5
Wajumbe kutoka Tanzania waliohudhuria Mkutano wa Benki ya Dunia wakiwa kwenye Mkutano wa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Jijini Washigton DC.
ben6
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akieleza ni jinsi gani Benki ya Dunia inafurahia utendaji kazi wa nchi ya Tanzania hasa katika kukuza uchumi, kulia kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dkt. Natu Mwamba anaemfuatia ni Bw. Johson Nyela Mkurugenzi wa Sera Uchumi na Utafiti na Bw. Dickson Lema Meneja Masuala ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania Jijini Washgton DC, Marekani.
ben7
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Makhtar Diop akifafanua masuala mbalimbali namna Benki hiyo ilivyojipanga kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi yake mbalimbali ya kipaumbele wakati wa mazungumzo kati ya Benki hiyo na Ujumbe kutoka Tanzania unaohudhuria mkutano wa mwaka wa Benki hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa-IFM, unaofanyika Washington DC nchini Marekani
ben8
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndullu akimweleza jambo Mkurugenzi Msaidizi wa Benki ya Dunia ya Afrika Bw. Makhtar Diop (Hayupo pichani) juu ya miradi mbalimbali ambayo Benki ya Dunia inaweza Kusaidia Tanzania katika Sekta mbalimbali kwani kwa sasa uchumi wa Tanzania umekuwa kwa kiasi cha kuridhisha kulia kwake ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango akifuatiwa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed, Jijini Washington DC, Marekani
ben9
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndullu akimwonesha kitabu waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango walipokuwa kwenye mkutano na Mkurugenzi Msaidizi wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Jijini Washigton DC, Marekani.
ben10
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akifurahia jambo na Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bw. Albert Zeufack alipotoka kwenye mkutano, Jijini Washigton DC, Marekani.
ben11
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akifurahia jambo na Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bw. Albert Zeufack alipotoka kwenye mkutano, Jijini Washigton DC, Marekani.
........................................................
Benny Mwaipaja, MoFP-Washington DC
BENKI ya Dunia inakusudia kuipatia Tanzania ruzuku na mkopo wenye masharti nafuu wa dola Bilioni 1 nukta 6 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 3 nukta 5 kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo nishati ya umeme, kilimo biashara na ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu amesema Jijini Washington DC, Marekani ambako Ujumbe wa wataalamu wa masuala ya uchumi na Fedha kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kwamba mazungumzo kuhusu mkopo huo yako katika hatua za mwisho.

Prof. Ndulu amesema kuwa upatikanaji wa mkopo huo utaisaidia serikali kuboresha miundombinu yake mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya sekta ya viwanda kwa kuimarisha pia mazingira ya sekta binafsi kufanyabiashara na kuwekeza mitaji na teknolojia.

“Mbali na mkopo huo ambao ni muhimu kwa taifa, tunajadili pia namna ukuaji wa uchumi unavyotakiwa kuakisi maisha ya kawaida ya wananchi wetu kwa kupiga hatua kimaisha na kuondokana na umasikini” alisema Gavana Prof. Ndulu.

Aidha, amesema kuwa Benki ya Dunia imesifu hatua zilizofikiwa na serikali ya Tanzania katika kukuza na kusimamia uchumi wake ambao licha ya uchumi wa dunia kushuka viwango vyake vya ukuaji uliotarajiwa wa asilimia 3.3 na kukua kwa asilimia 1.5 tu, Uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia 7.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zinazoendelea ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na unatarajia kukua zaidi kutokana na kuvumbuliwa kwa gesi na kushuka kwa mfumuko wa bei” Alisisitiza Prof Ndulu
Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa mkopo utakao tolewa ni pamoja na dola milioni mia 2 kwaajili ya kulijengea uwezo shirika la ugavi wa umeme nchini Tanzania-Tanesco ili liondokane na nakisi inayosababishwa na madeni makubwa yanayolikabili shirika hilo
Dkt. Mpango Amefafanua kuwa mkopo huo pia utaiwezesha serikali kulipa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kufanyika kwa uhakiki wa kina wa madeni hayo ili kuiwezesha mifuko hiyo itoe huduma inayostahili kwa wananchama wake.

Amesema kuwa kiasi kingine cha fedha hizo kitatumika kuijengea uwezo sekta binafsi iweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Taifa pamoja na kuimarisha kilimo kwa kuwawezesha wakulima kulima kilimo cha kibiashara na kuondoa kodi zenye kuleta kero katika sekta ya kilimo.

“Wakati tunatekeleza mpango huo tutaangalia pia namna ya kupitia upya kodi zinazolalamikiwa katika sekta ya utalii” amefafanua Dkt. Mpango
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Mohamed, ameishukuru Benki ya dunia kwa kuisaidia nchi hiyo kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa visiwani humo ikiwemo uboreshaji wa rasilimali watu, miundombinu ya barabara, kiwanja cha ndege na kuboresha mazingira yatakayochangia kukua kwa sekta ya utalii visiwani humo.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Makhtar Diop, amesema kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania ili iweze kufanikiwa kiuchumi na kijamii.

Amesifu juhudi na hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha nidhamu ya kazi na kupambana na vitendo vya ufisadi hatua ambayo inaungwa mkono na benki yake ili kuharakisha maendeleo ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.

Diop amebainisha kuwa Benki yake inataka kuona Shirika la Umeme Tanzania Tanesco linaboreshwa na kuwa la kisasa kwakuwa nishati ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa viwanda na kwamba wangependa kusaidia eneo hilo namengine ya kuboresha rasilimali watu kwa kuwekeza kwenye elimu na kuwainua wananchi kimapato kupitia mradi wa TASAF na mingine itakayoanzishwa.

No comments: