Friday, July 22, 2016

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII ATAKA JAMII ZINAZOZUNGUKA MAENEO YA HIFADHI NCHINI ZISHIRIKISHWE KULINDA MALIASILI ZA TAIFA

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa kwanza kulia) akizungumza na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Massana Mwishawa (wa pili kulia) alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 21 Julai, 2016 kwa ajili ya kujionea kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto aliyesimama na Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma.
  Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Massana Mwishawa (wa pili kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa kwanza kulia) sehemu ya fukwe za hifadhi hiyo ambazo ni makazi ya Mamba na Ndege wa aina mbali mbali alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 21 Julai, 2016 kwa ajili ya kujionea kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto aliyesimama na Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa pili kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mwl. Herman Kapufi (kulia) katika fukwe ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 21 Julai, 2016 kwa ajili ya kujionea kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto anaesaini kitabu cha wageni ni Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma. 
Picha ya pamoja kati ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (katikati waliokaa), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mwl. Herman Kapufi (wa tatu kushoto waliokaa), Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma (wa tatu kulia waliokaa), Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Ibrahim Mussa (wa pili kushoto waliokaa) na baadhi ya Watumishi wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo hifadhini hapo tarehe 21 Julai, 2016
Mamba katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
 Moja ya Fukwe katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
 Huduma za malazi katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
Huduma bora ya vyumba inapatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.
Huduma za usafiri wa boti zinapatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.

NA HAMZA TEMBA - WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 

____________________________________________________________

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani ameitaka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuzishirikisha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi hapa nchini kutambua umuhimu wa kuhifadhi maeneo hayo ili kutoa ulinzi shirikishi katika kupambana na Ujangili.

Eng. Makani amesema hayo jana wakati akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka hiyo akiwa ziarani Mkoani Geita katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo.

“Wananchi waoishi jirani na maeneo haya ya hifadhi ni muhimu wakaelimishwa juu ya faida za uhifadhi kiikolojia na kiuchumi kwenye maisha yao ambapo itawapa msukumo wa kuyatunza na kuyalinda” Alisema Eng. Makani.

Aliongeza kuwa vita dhidi ya Ujangili hapa nchini haiwezi kufanikiwa kirahisi iwapo jamii inayozunguka maeneo ya Hifadhi haitatoa ushirikiano kwa Serikali katika kulinda na kuhifadhi Maliasili zilizopo.

“Pamoja na mbinu nyingine, washirikisheni wananchi watusaidie kupambana na ujangili ili fedha ambayo ingetumiwa na Serikali kwa kazi hiyo itumike kuendeleza hifadhi zetu pamoja na kutoa huduma nyingine za kijamii” Alisema Eng. Makani.

Akizungumzia faida za uhifadhi kiuchumi hapa nchini alisema kuwa, Sekta ya utalii ndio sekta pekee inayoongoza kwa kuliingizia taifa mapato mengi ya nje (foreign currency) ambayo ni asilimia 25 ya mapato yote. Sekta hiyo pia inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.2.

Eng. Makani aliongeza kuwa “Serikali ya awamu ya tano ina mpango wa kuboresha sekta ya utalii ili iweze kuiingizia zaidi mapato, katika kufanikisha hilo tumeweka mkakati wa kuboresha ofisi zetu za utalii za Kanda ili ziweze kutangaza na kukuza zaidi utalii wa ndani”.

Kwa upande wa hoteli zinazotoa huduma ya kitalii hapa nchini alisema kuwa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, Serikali itaanza rasmi zoezi la kuorodhesha hoteli zote zinazotoa huduma hiyo na kuzipanga kwenye makundi ya ubora ambapo zile zitakazoonekana hazina hadhi kabisa zitaondolewa katika mtandao wa kutoa huduma hiyo. Alisema zoezi hilo litaboresha huduma za kitalii nchini na kusaidia watalii kufikia hoteli wanazozihitaji na kupata huduma stahiki .

Katika kushirikisha sekta binafsi kwenye kukuza utalii nchini, amewaomba watoa huduma za ndege kuangalia upya viwango vya gharama zao za usafiri ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu na kunufaika na huduma hiyo.

Wakati huo huo aliwaasa watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo kufanya kazi kwa bidii, kuwa na maadili mema na uadilifu kazini. Aliwataka pia kuwa mstari wa mbele kupiga vita ujangili, kuboresha ukusanyaji wa mapato na kushirikisha wananchi kwenye uhifadhi.

Hapo awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Naibu Waziri wa Maliasili, Eng. Ramo Makani, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Massana Mwishawa alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili hifadhi hiyo ni ujangili na upatikanaji mdogo wa mapato ambao hauwiani na mahitaji ya hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Luiza Kasheku maarufu kama Msukuma, alimuomba Naibu Waziri huyo wa Maliasili kuboresha Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambayo ipo Jimboni kwake iweze kupata mapato ya kutosha na kujiendesha yenyewe. Hifadhi hiyo kwa sasa inategemea mapato kutoka kwenye hifadhi nyingine kujiendesha.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo iliyopo Mkoani Geita ni moja ya sehemu pekee na muhimu katika uzalishaji wa mazalia ya samaki katika ziwa Victoria. Sehemu nyingine ni Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane iliyopo Mkoani Mwanza. Hifadhi hizi zina umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa samaki katika Ziwa Victoria.

No comments: