Thursday, June 23, 2016

WATUMISHI WA UMMA WATAHADHARISHWA KUTOSAMBAZA NYARAKA ZA SERIKALI KATIKA MITANDAO YA KIJAMII.

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bw. Eliakim Maswi akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Manyara katika kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2016.
 Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Dkt. Joel Bendera akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Manyara katika kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2016.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki (Mb) akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa Watumishi wa Umma wa mkoa wa Manyara kuhusu hoja mbalimbali alizozipokea wakati wa kikao kazi cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mkoani Manyara.
 Afisa Muuguzi Msaidizi, Mkoa wa Manyara,Bi. Josephine Mosha akiwasilisha maoni kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki wakati wa kikao kazi cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mkoani Manyara.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (Mb), akikabidhiwa ripoti kuhusu kero na maoni kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Mkoa (CWT)-Manyara Bw. Qambos Michael Sulle ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2016.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewataka Watumishi wa Umma kuacha tabia ya kusambaza Nyaraka za Siri za Serikali katika Mitandao ya Kijamii.

Waziri Kairuki aliyasema hayo katika kikao kazi cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mkoani Manyara.

Waziri Kairuki alisema serikali inao utaratibu wake wa kusambaza nyaraka kwa waajiri, na taarifa kumfikia kila mhusika na sio kupitia mitandao ya kijamii.

“Nawakumbusha kuhusu Kanuni za maadili katika Utumishi wa Umma ambazo  kila mtumishi anapaswa kuzingatia na kuelewa na endapo kama huelewi uliza ueleweshwe” Waziri Kairuki alisema na kuongeza Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma lazima zifuatwe.
Aliongeza, hatua zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kusambaza nyaraka kinyume na taratibu, kupitia namba zao za simu.

Waziri Kairuki, pamoja na mengine alisisitiza waajiri kuwashirikisha Watumishi katika bajeti kupitia baraza la wafanyakazi ili wajue mambo ya msingi watakayotekeleza na kuweza kuhoji pale itakapolazimu kufanya hivyo na kwa Waajiri ambao hawajaunda mabaraza ya wafanyakazi wameelekezwa kuunda mabaraza hayo. 

Pia, Waziri Kairuki alikumbusha kuwa uhamisho usifanyike kiholela, bali kwa sababu za msingi na pale kibali cha ajira kinapotolewa utekelezaji ufanyike mapema ili huduma ziendelee kutolewa.
Aidha, watumishi wanaoteuliwa katika nafasi za madaraka wathibitishwe katika kipindi cha miezi sita.
Pamoja na kupata fursa ya kuongea, na kushauri, Watumishi wa Umma waliandika kero na maoni ambayo yalichukuliwa ili kufanyiwa kazi.

Kikao hicho kilikua na lengo la kupokea maoni na kero za watumishi wa umma ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2016 na kilihudhuriwa na watumishi wote wa mkoa wa Manyara, kupitia uwakilishi.
Wiki ya Utumishi wa Umma ni moja ya tukio muhimu katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU), ambayo huadhimishwa kutambua mchango wa watumishi wa Umma barani Afrika katika kuleta maendeleo, ikiwamo kutatua changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu. Wiki hii huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa wakati mmoja. 

No comments: