Thursday, June 23, 2016

KAMPUNI YA STAMIGOLD YAKABIDHI MSAADA WA UMEME WA JUA KWA KITUO CHA POLISI BIHARAMULO

Kampuni ya STAMIGOLD ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupitia mgodi wake wa Biharamulo uliopo wilayani Biharamulo mkoa wa Kagera umekabidhi  msaada wa  umeme wa jua kwa Kituo cha Polisi Mavota wenye thamani ya shilingi milioni 10/- za kitanzania lengo likiwa kuboresha mazingira ya  kazi katika kituo yatakayosaidia kuimarisha  ulinzi.

Msaada huo umekabidhiwa kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mavota OCS. Bwana Antony Ramwa na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Biharamulo Mhandisi Dennis Sebugwao.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika jana katika Kituo cha Polisi Mavota kilichopo katika kijiji cha Mavota takribani kilomita tano kutoka lango kuu la mgodi Mhandisi Sebugwao alisema kuwa msaada wa umeme wa jua uliokabidhiwa ni utekelezaji wa mipango iliyowekwa na kampuni ya kuwezesha uwepo wa mazingira bora katika huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, maji na miundo mbinu hasa katika jamii zilizo jirani na mgodi
Meneja Mkuu wa mgodi wa Biharamulo Mhandisi Dennis Sebugwao (mwenye sare ya mgodi) akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi msaada wa umeme wa jua kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mavota OCS Bwana Ramwa mwenye sare za Polisi (aliyeshika kifimbo).

 “Mgodi unatambua umuhimu wa kuwa na mazingira bora katika huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na uwepo wa miundo mbinu itakayowezesha  wananchi kupata huduma muhimu bila vikwazo na ndio sababu Stamigold tukaona ni vyema kuweka umeme wa jua katika Kituo cha Polisi Mavota ili wananchi waweze kunufaika na huduma zitolewazo hata nyakati za usiku ukizingatia kituo hiki ni kituo pekee cha polisi katika kata nzima ya Kaniha ambapo kinahudumia takribani vijiji vitano” Alisema Sebugwao.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Mavota OCS.  Bwana Antony Ramwa aliushukuru uongozi wa mgodi kwa kukubali ombi la kuweka umeme wa jua katika kituo cha polisi Mavota ili kuwasaidia kuondokana na adha ya kufanya kazi katika mazingira magumu ambapo awali Polisi walilazimika kusitisha huduma zao kituoni pindi giza liingiapo hivyo kusababisha kero kwa wananchi pale inapotokea kuhitaji  msaada wa polisi nyakati za usiku.
Mhandisi wa Umeme kutoka mgodi wa Biharamulo Godfrey Lweyemamu akitoa maelezo ya namna kifaa cha umeme wa jua kilivyounganishwa na uwezo wake wa kufanya kazi. Pembeni ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mavota OCS Bwana Antony Ramwa akishuhudia.

“Msaada  huu utasaidia sana kuimarisha ulinzi katika kata yetu ya Kaniha kwani kuanzia sasa Kituo kitafanya kazi ya kuhudumia wananchi usiku na mchana bila kikwazo chochote. Kuwepo kwa umeme katika kituo hiki kutasaidia askari kutumia muda mwingi katika doria kusaidia kutokomeza uhalifu uliokuwa ukifanywa hasa nyakazi za usiku katika maeneo mbalimbali hususani katika maeneo yanayozunguka mgodi.” Alieleza OCS Ramwa.

Msaada uliokabidhiwa umehusisha ufungaji wa umeme wa jua katika Kituo cha Polisi Mavota pamoja na nyumba wanayoishi Polisi wa kituo hicho ambapo kazi hiyo imefanywa na Wafanyakazi wa Kitengo cha Matengenezo katika mgodi wa Stamigold chini ya usimamizi wa Mhandisi wa Umeme Godfrey Lweyemamu.
Moja kati ya kifaa cha umeme wa jua kilichowekwa katika kituo cha polisi Mavota kwa msaada wa mgodi wa Stamigold Biharamulo.

Aidha mgodi wa Biharamulo tangu kuanzishwa kwake umekuwa ukitoa huduma mbalimbali za kijamii hususani kwa jamii zilizo jirani na mgodi zikiwemo uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu, afya, barabara za vijiji, utoaji wa ajira na masoko kwa vikundi vya wajasiriamali  ili kusaidia jamii kunufaika na uwepo wa mgodi.

Maeneo mengi hapa nchini hususani vijijini yanakabiliwa na ukosefu wa nishati ya umeme hali inayosababisha watoaji wa huduma muhimu za kijamii kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na wakati mwingine wananchi kukosa kabisa huduma hasa nyakati za usiku.

No comments: