Sunday, June 5, 2016

MKUTANO WA ACT WAZALENDO VIWANJA VYA ZAKIEM MBAGALA JUMAPILI LEO

Kiongozi mkuu wa chama cha  upinzani nchini Tanzania ACT WAZALENDO ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho jimbo la Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe akiwahutubia mamia ya wakazi wa jiji la Dar es salaam katika mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Viwanja Vya Zakiem Mbagala,mkutano ambao ulikuwa na lengo la Kuwaeleza watanzania hali halisi ya kile ambacho kimetokea katika bunge la Tanzania na kufanya Mbunge huyo na wenzake saba wa vyama vya upinzani kusimamishwa kuingia bungeni kwa vipindi tofauti.

Akizungumza katika mkutano huo ambao umetumika kama uzinduzi wa harakati za kuzunguka nchi nzima kudai Democrasia ambayo ameeleza kuwa imeanza kuminywa na serikali ya awamu ya Tano Mbunge huyo amesema kuwa Chama cha ACT WAZALENDO kimesema wazi kuwa kitamuunga mkono Rais wa Tanzania Dk JOHN MAGUFULI katika harakati zake za kupambana na Rushwa lakini kitampinga kwa nguvu zote katika harakati zake za kuiminya Deocrasia ya nchi.
Amesema kuwa Hatua ya wabunge saba wa Bunge la Tanzania kusimamishwa kuingia bungeni kwa kisingizio kuwa walifanya fujo wakati wakidai haki ya watanzania kuliona bunge live ni kitendo ambacho kinaonyesha udhaifu mkubwa kwa serikali ambayo inajinasibu kuwa inapambana na wala Rushwa na mafisadi huku ikiogopa kuweka wazi mambo yake likiwemo Bunge kuonekana na wananchi wote kama ilivyokuwa awali na ndio maana chama chake kimeamua kuzuunguka nchi nzima kwa kusirikiana na vyama vingine vya upinzani na watanzania wote kupinga hali hiyo ya ukandamizwaji wa democrasia.


PICHA NA STORY NA EXAUD MTEI MSAKA HABARI

Mh ZITTO KABWE akiwasili katika viwanja vya ZAKIEM MBAGALA jioni ya leo jumapili kwa ajili ya mkutano huo mkubwa uliomalizika jioni Hii
Katikati ni mwenyekiti wa chama cha ACT WAZALENDO Mama ANNA ELISHA MGWIRA akiwa pamoja na katibu mkuu wa chama hicho Mh Juma Saanani pamoja na Kiongozi mkuu wa chama hicho Mh ZITTO KABWE wakifwatilia kwa ukaribu mkutano huo leo
Mwenyekiti wa chama cha ACT WAZALENDO Mama ANNA ELISHA MGWIRA akiwahutubia mamia ya wakazi wa mkoa wa Dar es salaam katika viwanja vya mbagala Jijini Dar es salaam ambapo katika hotuba yake mwenyekiti huyo amelaani vikali kauli aliyoitoa Rais wa Jamhuri ya muungano waTanzania Dk magufuli Ya kuwaita wanafunzi waliokuwa wanasoma UDOM kuwa ni vilaza kauli ambayo amesema kama mama ambaye anaongoza kwa kujali UTU ,UADILIFU na UZALENDO kauli hiyo haifai kwa ustawi wa jamii yake na badala yake Rais awaombe Radhi wanafunzi hao na wazazi wao kwa kauli hiyo
Pamoja na kualikwa kwa vyama vingine vya upinzani vikiwemo CHADEMA,CUF na NCCR.ni chama kimoja tu kilichoweza kushiriki katika mkutano huo ambapo pichani ni kiongozi wa makamishna wa chama cha NCCR-MAGEUZI ndugu Peterson Mushengera ambaye amekiwakilisha chama chake katika mkutano huo wa hadhara.
 Hotuba Zote zilizotolewa katika mkutano huo zipo chini



HOTUBA YA KIONGOZI WA CHAMA CHA ACT-Wazalendo NDUGU ZITTO KABWE, MBUNGE WA KIGOMA MJINI LEO JUNI 5/2016 KATIKA VIWANJA VYA MBAGALA ZAKHIEM JIJINI DAR EsSALAAM 

Ndugu Wananchi,

 Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwenu kuitikia wito wetu wa kuja kutusikiliza. Tumewaita hapa ili kuwaeleza kinachoendelea katika nchi yetu hivi sasa na madhara makubwa yanayoweza kutokea iwapo hatutosimama kidete dhidi ya mbinu zozote za kufifiza demokrasia na misingi ya uwajibikaji katika nchi yetu.
Mwaka 2015 tulikwenda kwenye uchaguzi kuchagua madiwani, wabunge na Rais. Baada ya Uchaguzi kumalizika Serikali mpya iliundwa na Serikali za mitaa kuundwa. Nawapongeza wananchi wote kwa kuendesha zoezi la uchaguzi kwa amani na kuweka heshima ya nchi yetu mbele.
Baada ya uchaguzi tumeona viongozi wapya wakichukua hatua mbalimbali nzuri na mbaya, zenye kujenga na kubomoa, zenye kuimarisha demokrasia na zinazobomoa demokrasia. Tumeshuhudia maamuzi mengine ambayo yanatia hofu kwamba ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza demokrasia ya nchi yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu. 

 Mkutano wetu wa leo utagusia baadhi ya maeneo ambayo tunadhani ni vihatarishi vya ustawi wa wananchi wetu na ambavyo lazima tuanze kuvipinga mapema sana kabla havijaota mizizi.

Ndugu Wananchi,

 Baadhi ya maeneo tutakayozungumza leo ni pamoja na

·      Wabunge kusimamishwa kazi za Bunge
·      Maamuzi ya Serikali kuhusu Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
·      Hali ya Zanzibar
·      Mwelekeo wa Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli
·      Tishio la Nchi kuelekea kwenye Utawala wa Imla wa MTU mmoja

Wabunge kusimamishwa Kazi

Ndugu Wananchi, mnamo tarehe 30 Mei 2016 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Naibu Spika lilipitisha Azimio la Bunge la kuwasimamisha kazi wabunge 7 kwa vipindi mbalimbali. Wabunge 2 ndugu Esther Bulaya na ndugu Tundu Lissu walisimamishwa Mikutano miwili ya Bunge, Wabunge 4, ndugu Halima Mdee, Ndugu Pauline Gekul, Ndugu Godbless Lema na mimi ninayezungumza nanyi walisimamishwa mkutano mmoja huu unaoendelea wa Bajeti na mbunge mmoja ndg John Heche Suguta amesimamishwa vikao 10 vya mkutano huu wa tatu unaoendelea.

 Sababu iliyoelezwa na Bunge ni kwamba wabunge hawa walifanya fujo siku ya tarehe 27 Januari 2016 kufuatia hoja niliyoitoa Bungeni ya kutaka mjadala kuhusu sababu za hovyo za uongo zilizotolewa na Serikali kuhusu uamuzi wa kuzuia Shirika la Utangazaji la Taifa ( TBC ) na televisheni binafsi nyengine kuonyesha moja kwa moja mikutano ya Bunge.

Ndugu Wananchi,

 Mimi binafsi pamoja na wabunge wengine 6 hatukufanya fujo yeyote ndani ya Bunge. Kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji maamuzi ya Serikali ambayo kwa maoni yetu hayana msingi wowote. Serikali inasema ninyi Wananchi hamfanyi kazi kwa sababu Bunge linaonyeshwa wakati wa kazi. Hata hivyo Serikali hiyo hiyo inatwambia kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita uchumi wa Tanzania ulikua kutoka tshs 16 trilioni mwaka 2005 mpaka tshs 99 trilioni mwaka 2015.

Kipindi chote hiki Bunge lilikuwa linaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa na televisheni ya StarTV. Kama mngekuwa hamfanyi kazi Uchumi usingekua kwa kiwango hicho cha asilimia 600 ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Utawala wa Rais John Magufuli unataka kutuaminisha kuwa ukiwa na Bunge ‘live’ watu hawafanyi kazi lakini uongozi uliopita umedhihirisha kwa ushahidi kuwa ukipanua demokrasia na kuwaonyesha wananchi kila kinachoendelea Bungeni uwezo wa kazi unaongezeka na uwezo wa wananchi kuwajibisha viongozi wao unaongezeka.

 Hivyo Serikali kuamua kuficha Bunge ni mbinu za kuendesha Serikali kwenye giza ili kufanya maamuzi ambayo baadaye ionekane Serikali tu au Rais tu ndiye mfanya kazi. Ndio maana mikutano yote ya Rais anapohutubia huonyeshwa moja kwa moja lakini sio Bunge.

Ndugu Wananchi,

 Wabunge wamesimamishwa kwa sababu ya kukataa Bunge kuendeshwa kwenye giza. Wabunge waliosimamishwa walisimama kidete kuhoji sababu za Serikali kufikia maamuzi hayo. Walitaka kujua kwanini Serikali imekuwa kigeugeu kwa kubadilisha badilisha sababu zake za kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Wakati mmoja Serikali ilisema sababu ni gharama, kama ni hivyo ni kwanini walizuia StarTV na AzamTV kuonyesha moja kwa moja? Ni dhahiri wananchi Serikali inataka kuendesha mambo yake kwa uficho kwa sababu kuna maamuzi inataka kufanya na haitaki wananchi mjue mapema maamuzi hayo. Serikali inaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele.

Wananchi, wabunge waliosimamishwa ni wabunge wenye uwezo wa kujenga hoja. Kuna wengine wamebaki Bungeni wenye uwezo mkubwa tu wa kujenga hoja, lakini hawa saba waliosimishwa ni wabunge walijidhihirisha kwa muda mfupi kwa baadhi yao kama ndugu Heche, kwamba wanaweza kusimamia hoja zao bila woga. Swali la kujiuliza ni, tukio ambalo limetokea mwezi Januari ni kwanini lifanyiwe mwezi Juni tena wiki moja tu kabla ya Waziri wa Fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali? Katika waliosimamishwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Fedha ndg. Halima Mdee na Waziri Kivuli wa zamani wa Fedha ambaye anazungumza nanyi leo.

 Kuna nini katika hili? Nitawaeleza katika hoja ya Bajeti. Kimsingi Utawala wa Rais Magufuli umepanga kupandisha kodi za wananchi masikini na uliona uwepo wetu bungeni utatibua mipango yao. Rais na wenzake ndani ya CCM hawapendi kusikia hoja zinazowapinga, hawana uvumilivu wa kukosolewa na hivyo walipanga kuhakikisha kuwa baadhi yetu hatutakuwepo kwenye mjadala wa Bajeti ili kufanikisha malengo yao ya kufanya maamuzi yatakayowandamiza wananchi. Nitaeleza vizuri hili baada ya muda kidogo.

 Hivyo nataka Watanzania wajue kuwa kusimamishwa kwetu ni ajenda maalumu ya Serikali ya Rais Magufuli kufunika mjadala wa Bajeti kwa sababu anajua kuwa tunajua wanachotaka kufanya dhidi ya mafukara wa nchi yetu. Sisi hatutakaa kimya, tutatumia wenzetu waliopo Bungeni kuyasema haya na pia tutazungumza na wananchi kuwaeleza pia. Tutatumia mikutano yetu mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyetu kuhakikisha kuwa Wananchi wanajua kila kinachoendelea na kuwataka kuunganisha nguvu kukataa udikteta unaonyemelea nchi yetu.

Wanafunzi 7800 kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma

Ndugu Wananchi, mmesikia sakata la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliokuwa wanasomea programu maalumu ya ualimu wa Sayansi. Hawa ni watoto wa Watanzania masikini waliokubali kuacha kwenda A levels na kukubali kusomea diploma ya Ualimu ili wakawafundishe watoto wa masikini wenzao.

 Wanafunzi hawa hawakuanzisha wao program hii, ilianzishwa na Serikali na kupitishwa na Baraza la Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe na alishiriki kikao hicho kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri. Rais Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama wenzao walivyofanya na kuanza kutekelezwa. Lengo na program hii ni kuondoa tatizo la walimu wa masomo ya Sayansi. Tanzania ina uhaba wa walimu wa Sayansi 26,000 na tukienda kwa utaratibu wa kawaida tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.

Program hii ilianzishwa ili kuziba pengo hili kwa muda mfupi na vijana waliitikia wito huu wa kizalendo kuhakikisha wadogo zao hawakosi walimu siku za usoni. Serikali ya awamu ya Tano imewafukuza vijana hawa 7800 kutoka chuoni ndani ya masaa 24 kwa makosa ambayo sio yao.
Wananchi, hatusemi kuwa program haikuwa na kosoro. Zilikuwepo ikiwemo kudahili wanafunzi wengi zaidi ya ilivyotarajiwa na kudahili wanafunzi 133 hivi hivi kati ya 7800 ambao walikuwa na daraja la nne katika masomo yao. Lakini aliyedahili sio watoto hawa bali ni Serikali yenyewe, kwanini waadhibiwe watoto?


Bunge lilipotaka kujadili hoja hii au hata kuipeleka kwenye kamati ya Bunge kuifanyia uchunguzi na kutoa mapendekezo Naibu Spika alizuia hoja ya mbunge Joshua Nasari bila sababu za msingi.

Wabunge wote bila kujali vyama vyao walitaka hoja ijadiliwe ni kuweza kupata majawabu. Mbona wakati wa Uongozi wa awamu ya 4 tulijadili hoja ya mgomo wa madaktari na kisha kupelekwa kwenye kamati ya husika ya bunge kupata suluhisho la kudumu? Kwanini Utawala wa Rais Magufuli hautaki Bunge lifanye kazi yake? Mbona yeye Rais kaenda kujadili jambo hilo huko Chuo Kikuu mlimani?

Ndugu wananchi

 Rais Magufuli anafikia kuita watoto wetu vilaza? Rais huyu anayesema yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini vilaza. Vijana hawa Wazalendo waliojitoa muhanga kuacha kwenda kidato cha Tano ili wasome kuwa Walimu na kulea kizazi kijacho Rais wao anawaita vilaza.

 Rais sifa zimempanda kichwani. Rais Magufuli hana budi kuwaomba radhi vijana hawa na wazazi wao, Rais ni Mwalimu, anajua madhara ya kisaikolojia kufuatia maneno aliyoyasema. Ni sawa na Jenerali wa Jeshi anayetukana askari wake waliomstari wa mbele.

Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani. Rais Magufuli anaongea mno, sio sawa kwa Kiongozi. Rais ajue kuweka akiba ya maneno. Yeye ni Kiongozi wa wote, wenye akili na vilaza. Yeye anapaswa kuwa wa mwisho kuongea ili watu waweze kukataa rufaa kwake. Yeye akishaongea wananchi ‘aggrieved’ waende kwa nani? Waende kwa mungu?
Tunamtaka Rais awarudishe wanafunzi Chuoni mara moja na wale wanafunzi ambao itaonekana hawakuingia kwenye program kihalali waondolewe badala ya kuadhibu watoto wote kwa makosa ya wachache ambao asilimia 5 tu ya wote. Makosa madogo ni mambo ya kawaida katika Jamii. Yeye Rais ni mfano mzuri wa hili kwani naye mbona aliteua Waziri mlevi na kurekebisha kwa kumfukuza peke yake, mbona hakufukuza Baraza zima la mawaziri kwa ulevi wa Waziri mmoja?

Zanzibar

Ndugu Wananchi mnajua mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kufutwa chama chetu kiliweka msimamo wa wazi kwamba kinatambua ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad kama Rais aliyechaguliwa na Wazanzibari na anayepaswa kula kiapo na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tuliandika pia masuala 10 muhimu kwa Rais kuyafanyia kazi na moja ya jambo tulilomtaka Rais Magufuli kufanyia kazi ni suala la demokrasia ya Zanzibar.

 Rais hakusikia wito wetu na aliruhusu ufutwaji usio halali kisiasa wala kisheria wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015. Tunarudia kusisitiza kuwa Chama chetu cha ACT Wazalendo hakiutambui uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliofanyika mwezi Machi mwaka 2016 na matokeo yake yote yaliyofanyika.

 Kwa maana hiyo hatutambui Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Rais wa Zanzibar.

Ndugu Wananchi,

Hivi karibuni kumekuwa na kuongezeka kwa sintofahamu huko Zanzibar kufuatia Mgombea Urais aliyeshinda na kunyanganywa ushindi wake kwenda kwa wananchi kuzungumza nao. Hali hii imepelekea jeshi la polisi kumhoji Maalim Seif na siku mbili baadaye Dkt. Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu hana vifaru na mizinga.

 Tunalaani kauli hii ya Dkt. Shein ya kutisha kwa vifaru na mizinga. Kamwe huwezi kuzima haki za Wananchi kwa vifaru na mizinga. Dkt Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa Dola kubwa kama Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.

 Dkt Shein akumbuke kuwa nchi kadhaa duniani zilikuwa na madikteta wenye vifaru na mizinga lakini waliondoka. Dkt Shein afute kauli yake hii na kuacha vitisho badala yake aanze mchakato wa kupata maridhiano ya jamii ya Zanzibar. Hatutaki kurithi damu, tunataka kurithi nchi yenye amani, haki na demokrasia.

NduguWananchi

 Sisi ACT Wazalendo, tunajua hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar na mkwamo uliopo hivi sasa. Hata hivyo ni lazima tupate jawabu kupitia sanduku la kura. Tunapendekeza kuwa Vyama vikuu vya siasa Zanzibar vikubali ‘kufa kidogo’ yaani ‘to die a little’ kwa vyote kukubali kuwa Uchaguzi wa Mwaka 2015 na ule wa mwaka 2016 zilikuwa batili, zifutwe na Uchaguzi Mkuu mpya uitishwe.

Uchaguzi huo utanguliwe na Serikali ya Mpito itakayohusisha vyama vyote vya siasa na baadhi ya wanajamii wanaoheshimika na Wazanzibari wote ili kujenga kuaminiana. Tuandhani hii itatupa nusra kwa Zanzibar.

Tunawaomba Wazanzibari watumie mwezi mtukufu wa Ramadhani kutafakari maoni haya na wote kwa pamoja baada ya Ramadhani kuja na jawabu ya hali ya kisiasa. Tunatamani Zanzibari irudi kwenye hali ya kawaida na ishamiri. Zanzibar ikiingia kwenye mtafuruku Tanzania nzima itakuwa kwenye mtafaruku.

Ndugu Wananchi

Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kutoa uongozi kwenye suala hili na hivyo ni wajibu wa Wazanzibari wenyewe kukaa na kupata mwafaka wa kijamii na kusonga mbele.

Bajeti ya 2016/17

Wananchi, kuanzia tarehe 8 mwezi Juni 2016 Bunge litakuwa kwenye mjadala wa Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli. Rais ameleta mapendekezo ya Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni. Katika makadirio haya vyanzo vya ndani ni shilingi 18.5 trilioni na misaada ni shilingi 3.6 trilioni. Serikali inatarajiwa kukopa jumla ya shilingi 7.4 trilioni. Mwaka 2015/16 Serikali ilitarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 13.8 trilioni, hivyo ndani ya mwaka mmoja wa fedha Utawala wa Rais Magufuli unataka kukusanya shilingi 4.7 trilioni zaidi sawa na ongezeko la asilimia 25. Kwa ufupi ni kwamba Serikali haina budi kuongeza kodi kwa kiwango cha asilimia 25 ili kuweza kutimiza malengo yake ya makusanyo.

Ndugu Wananchi

Mtakumbuka kuwa mara baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani tulikuwa tunaelezwa kodi iliyokusanywa kila mwezi na tuliona wafanyabiashara wakikabwa koo kwa kukwepa kodi. Hata hivyo ongezeko la Makusanyo lilikuwa kwa miezi 2 tu ya Novemba na Disemba kwani kuanzia mwezi Janauri makusanyo yalianza kuendana na hali halisi ya uchumi wa nchi yetu na ndio maana mbwembwe za makusanyo hazisikiki tena hapa nchini. Ukweli ni kwamba Rais alikuwa anakusanya ‘arrears’ na hapakuwa na hapajakuwa na mbinu mpya za kukusanya mapato ya Serikali.

 Maeneo muhimu yanayopoteza mapato kama vile makampuni ya nje kutumia mbinu za kihasibu kukwepa kodi hayajatazamwa kabisa na Rais na wasaidizi wake. Hivyo, Serikali imeamua kurudi kwa wanyonge kuwaminya na kodi ikianzia kuchukua kodi zote majengo kutoka kwenye Halmashauri zetu.

Kodi za majengo ndio chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri zetu za Miji. Manispaa na Majiji. Uamuzi wa Serikali kuchukua chanzo hiki cha mapato utapelekea Halmashauri zetu kushindwa kuzoa taka na hata kutoa huduma kwa wananchi.

 Hata hivyo wananchi uamuzi huu ni kwa sababu Halmashauri nyingi za Miji zinaongozwa na vyama vya Upinzani kama vile Manispaa ya Kigoma Ujiji, Manispaa ya Iringa, Arusha jiji, Ilala, Kinondoni, Mbeya Jiji nk. Utawala wa Rais Magufuli unataka kuhakikisha kuwa Manispaa zinaoongozwa na vyama vya upinzani zinashindwa kutoa huduma. Duniani kote kodi za majengo hukusanywa na Serikali za Mitaa. Katika Bajeti ya mwaka huu kodi hizi zitaongezwa maradufu.

Wananchi, Serikali inatarajia kupandisha ushuru kwenye soda, vilevi na sigara pia kwa mujibu wa vitabu vya Bajeti vilivyogawiwa kwa wabunge. Hata kodi kwenye gharama za kupiga simu zitaongezwa kwa zaidi ya asilimia 10. Eneo la ushuru peke yake Serikali inataka kukusanya shilingi 1.2 trilioni kutoka shilingi bilioni 900 za mwaka uliopita. Hii ni  nyongeza ya shilingi 300 bilioni zaidi kutoka Bajeti ya mwaka 2015/16.

 Maeneo haya mawili peke yake ( kodi za majengo na ushuru wa bidhaa ) yataongezewa kodi kiwango cha kuumiza sana wananchi wa kawaida. Hii ndio sababu Serikali imefukuza baadhi ya wabunge mahiri bungeni ili kulainisha upitishwaji wao wa viwango hivi vya kodi. Hata hivyo tutatumia wabunge waliobakia Bungeni kuhakikisha kuwa kodi kwa wananchi masikini haziongezwi kiholela.

Wananchi, sisi tunaamini kuwa Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni ya Utawala wa Magufuli sio bajeti halisi kwani makadirio yao hayazingatii ukuaji wa uchumi na yana lengo la kuchukua fedha kutoka kwa wananchi kupeleka Serikali jambo ambalo litadidimiza uchumi wa nchi yetu.

Tishio la Demokrasia
Wananchi jambo la mwisho ambalo ninataka kuwaeleza ni tishio lililopo mbele yetu dhidi ya demokrasia ya vyama vingi. Hatua mbalimbali ambazo Utawala wa Magufuli unachukua ni ishara ya kutengeneza utawala wa imla. Rais ndiye anayejua kila kitu na ndiye anayeamua kila kitu. Hii ni hatari sana kwa nchi yetu na ni lazima kuchukua hatua mahususi kumkatalia Rais mwanzoni kabisa ili asizoee.

 Tunarudia kuwa tulimwunga mkono toka mwanzo katika vita dhidi ya ufisadi kwani ni vita muhimu na lazima ipiganwe bila kujali itikadi za vyama. Hakuna namna unaweza kumlaumu Rais anapochukua hatua za kusafisha uvundo katika nchi. Tutaendelea kumwunga mkono katika eneo hilo.

Wananchi, hata hivyo Rais anatia hofu mno katika ujenzi wa mfumo wa uwajibikaji. Tanzania ina vyombo vya kuimarisha uwajibikaji ikiwemo Bunge la Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa. Rais anataka kupigana dhidi ya ufisadi nje ya mfumo jambo ambalo ni la hatari sana kwa nchi kwani akitoka yeye tutaanza upya. Inawezekanaje Kiongozi anayepambana na rushwa akavunja nguvu ofisi ya ukaguzi ya Taifa kwa kumnyima Bajeti CAG?

Ndugu Wananchi

 Rais amediriki hata kuvunja Katiba na sheria ya ukaguzi kwani Bajeti ya CAG haipangwi na Serikali bali hupangwa na Kamati ya Bunge. Hata hivyo Rais ameenda kinyume na sheria na badala yake kapanga mwenyewe Bajeti ya CAG? Toka lini mkaguliwa akapanga bajeti ya anayemkagua? Kamati ya Bunge ilipanga Bajeti ya tshs 69 bilioni kwa CAG lakini Serikali ( mkaguliwa ) imeipiga panga mpaka tshs 32 bilioni. Hii ni moja ya mfano dhahiri kabisa wa Serikali kuanza kuvunja vunja vyombo vya uwajibikaji.

Wananchi, hivi sasa kuna ukosefu wa Sukari nchini. Rais alisimama kwenye viringe vya siasa akatoa matamko makali kwamba kuna wafanyabiashara wameficha sukari na tukaonyeshwa sukari hiyo. Hata hivyo baada ya siku chache vyombo kama PCCB na TRA vikasema sukari ile ni halali. Inakuwaje Rais alitamka maneno yale bila ya kushauriana na vyombo? Ni dhahiri Rais anaongea tu na kutaka kujenga utawala wa imla. Leo bado kuna shida ya sukari na sukari ambayo serikali inasema iliagiza haionekani. Ipo wapi?

Wananchi Rais alikwenda Benki Kuu na kusema nusu ya wafanyakazi pale ni hewa. Mpaka leo hatujaona hao wafanyakazi hewa wa BoT wakielezwa. Rais alikwenda tu kwa kupata maneno ya kuokoteza barabarani na kutoa matamko ambayo yanashusha hadhi ya Benki lakini Rais anashindwa kutoka mbele kusema alikosea. Tunajenga mfumo mbaya sana wa uongozi wan chi.
Leo tunataka kumwambia Rais kuwa aongoze, asitawale. Rais awe na Utu na wananchi wake. Rais awe anasikiliza kwanza na kuchambua mambo kabla ya kusema chochote mbele ya hadhara. Rais awe wa mwisho kusema ili kama kuna rufaa watoe waseme kwake. Vinginevyo Rais anataka kujenga utawala wa imla na tutamkatalia wazi wazi.

Wananchi, nimalizie kwa kusema yafuatayo. Rais John Magufuli amesema kuwa yeye amejitoa muhanga kupambana na ufisadi. Sisi tunalazimika kujitoa muhanga kulinda demokrasia.
Ni imani yetu kuwa ufisadi utapigwa vita kikamilifu sio kwa kutegemea nia ya mtu mmoja bali kwa kuboresha na kutumia misingi ya demokrasia kwa kujenga taasisi madhubuti zitakazomaliza janga la ufisadi bila ya kutegemea nia ya Rais.

Sisi tunaamini kuwa ni jukumu letu kusimama kujitoa mhanga kuzuia maafa ya kitaifa yatakayoweza kutokana na makosa ya kukandamiza demokrasia na uhuru wa mawazo kwa kuhoji, kukosoa na kurekebisha makosa hayo sasa bila kuchelewa.
Tunamwunga mkono Rais kutokomeza ufisadi lakini TUNAMPINGA Rais kutokemeza demokrasia. Demokrasia yenye misingi madhubuti ya Uwajibikaji ndio jawabu sahihi dhidi ya ufisadi na unyonyaji nchini kwetu.

Nawashukuru sana.

Zitto Kabwe
Dar es Salaam. Juni 5, 2015



Hotuba ya Mwenyekiti wa ACT – WAZALENDO katika mkutano wa Mbagala:  Juni 5, 2016

Ndugu zangu Watu wa Temeke,

Mwaka jana tulikuja kwenu kulieleza taifa juu ya uwepo wetu kama chama na baadae tukaja wakati wa kampeni. Katika nyakati zote hizo  mlitupokea na kutusikiliza kama mlivyowasikiliza vyama vingine. Leo tumerudi tena kwenu kutumia uwanja huu kuwapa maoni yetu juu ya mambo yanayoendelea nchini na kutoa mapendekezo yetu juu ya suluhu ya baadhi ya mambo.

Sisi raia wa nchi hii kupitia uongozi wa Chama cha Mapinduzi, (CCM) viongozi waliopo na waliopita ndio tumeifikisha nchi yetu hapa ilipo: tangu uhuru hadi leo. Sifa kubwa ya nchi yetu sasa ni umasikini unaosababishwa na sisi wenyewe chini ya mwavuli wa CCM: nchi ya kitu kidogo donge kubwa, nchi ya rushwa, ufisadi, wizi, ujanjaujanja, ulaghai, ubaguzi na upendeleo wa matakwa yetu na hasa rushwa ya kupata viongozi.

Kwa sababu sisi raia na viongozi wetu tumekubali kuachana na misingi ya utu, uadilifu na uzalendo, tumekuwa wasaliti wa maendeleo yetu wenyewe. Tumekataa haki, tumekataa kuwajibika na leo tunafurahia kutumbuana kama wanyama porini. Badala ya kutumbua mafanikio yetu tunatumbua ubaya wetu na tunafurahia kufanya hivyo.

Siku zote nchi yetu itakuwa na viongozi. Kadiri tutakavyojitahidi kuilinda amani ya nchi yetu, tutakuwa na chaguzi za kila wakati, lakini kadiri tutakavyoendesha chaguzi za rushwa, na chaguzi za matumizi makubwa yasiyolingana na maisha ya watu wetu, aibu yetu itafuata vivuli vyetu mpaka kaburini. Hatutaweza kujenga demokrasia kwa kuingiza viongozi kwa njia za rushwa.

Rushwa ina tabia moja mbaya ambayo watumiaji wake hushindwa kujipambanua na wasioitumia. Rushwa ina majigambo. Rushwa ina ubabe wa ushindi. Rushwa ina kiburi. Rushwa inapofusha inakupa kufikiri uko juu ya wengine kwa sababu ulifanikiwa kuwashinda kwa bei ya rushwa na si kwa ubora. Rushwa ni mwana mahadaa ana masihara. Rushwa hutendeka gizani na kujidhihirisha mwangani. Rushwa inaaibisha, inaataabisha inazuga, inadanganya. Rushwa ni hatari kwa uhai wa maendeleo ya watu.  Weka mbali na wote wenye uhai.!

Serikali ya awamu ya tano imejipambanua kupigana na adui huyu rushwa, tunaiomba ipigane vita hii kwa weledi na ujuzi mkubwa na maarifa, na kidemokrasia kwa kushirikisha wadau wengine wengi kadiri iwezekanavyo na kwa kuonyesha uongozi wa watu katika eneo hili la utawala. Rushwa na ubadhirifu umelifukarisha taifa. Matumizi mabaya ya mamlaka, ikiwa ni pamoja na urasimu umechelewesha haki za watu kwa ubaguzi na upendeleo.

Mambo haya tumeyazungumza kwa muda mrefu, na tumeona hatua zinazochukuliwa na serikali, na sisi raia tuweke mkono wetu, sauti zetu na nia yetu kuongeza nguvu ya kuchukua hatua madhubuti za kuyadhibiti. Napenda kuwapongeza watanzania wote kwa staha na uvumilivu mkubwa ambao tunautoa kwa serikali wakati inajipanga kututumikia kwa weledi, werevu, uadilifu, utu na uzalendo.

Tumekuja hapa kuwashirikisha mambo kadhaa, pamoja na utangulizi huu.  Kwanza kuwashukuru watanzania wote kwa kukitambua, kukikubali na kukipokea chama chetu. Kwa kauli hii nitamke wazi kuwa chama chetu kimefanikiwa kupata mbnge mmoja na na madiwani 40 kutoka majimbo mbalimbali nchini, baadhi ya majimbo yakiwa yale ambayo hatukupata nafasi ya kuyafikia kabisa. Wakati wa kuomba kura hatukufanikiwa kuwafikia wapiga kura wa majimbo yote licha ya kujitahidi kufika mikoa yote nchini. Lakini mmetupa madiwani.

Hii ni imani kubwa sana. Tunawashukuru na tunawaahidi kuwa tutaendelea kulitetea taifa katika uendeshaji wa siasa na hasa katika eneo la kuandaa viongozi makini wa kulitumikia taifa katika maeneo mbalimbali.

Hili ni lengo pana la chama na ni ahadi yangu kama mama Mwenyekiti wa Chama hiki ngazi ya taifa: Jukumu langu kubwa sasa ni kukijenga chama kama chombo cha kupika fikra, kushiriki michakato ya kutafuta muafaka wa kitaifa na kuandaa viongozi:  kuelekeza vijana wa kike na wa kiume kujitambua, kujikubali, na kujua kuwa hatima ya taifa hili ipo mikononi mwao leo na kesho.

ACT wazalendo kupitia mpango mkakati wetu wa miaka mitano 2016- 2020, tumeweka mikakati ya kuwajengea uwezo vijana wa kike na wa kiume kuhakikisha kuwa wanajifunza uongozi wa umma kiutu, ki-uadilifu, kiweledi na kizalendo. Taifa hili ni mali yenu. Wajibu wetu viongozi ni kuwapa mbinu za kulitumikia. Kwa kauli hii ninawaomba vijana wote wenye mapenzi mema na nchi hii, kujiunga na chama chetu, na kuchota maarifa haya kwa faida yenu wenyewe, kwa faida ya taifa na ulimwengu kwa ujumla.

Wiki hii dunia imempoteza mmoja wa watetezi wa maendeleo ya binadamu na utu, ndugu yetu Mohamedi Ali, bondia wa dunia wa mchezo wa ngumi. Ali aliwahi kusema hivi: vita vya silaha ni vita vya kubadili ramani, lakini vita vya umaskini ni vita vya kutafuta dira na ramani ya mabadiliko. Chama chetu kimedhamiria kuwa maabara ya kutafuta ramani ya kupambana na umasikini kwa kuandaa viongozi wake kwa waume kushiriki kuitengeneza ramani hii na kuleta mabadiliko ya kweli.  Vita vyetu ni vita vya fikra, vita vya kujenga na kuimarisha uono wa jamii na kuweka mikakati ya kuifikia ramani hii. Vijana wa Tanzania karibuni ACT sasa, tushiriki mpango huu wa fikra.

Kama mama kiongozi na Mwenyekiti ninajua kuwa kina mama wenzangu wengi mitaani hawana nafasi nilizowahi kupata mimi. Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaasa wanawake waliofanikiwa kupata nafasi kuwasaidia wanawake wengine kufikia hali yao.

Miongoni mwetu kuna wanawake wanaokejeliwa kuwa wategemezi na kuitwa magolikipa, na wanyonyaji. Ninapenda kuwatia moyo wanawake wote wa nchi hii kujitambua kuwa sifa kubwa ya ushindi wa timu za michezo ni golikipa. Timu hazishindi kwa kucheza na kutupiana mpira vizuri. Timu hushinda pale kipa wao akidaka mpira na ama kuisaidia timu yake kushinda ama kuifanya timu shindani ishindwe. Wanawake ni washindi. Tuudake vizuri mpira wa maisha, mpira wa maendeleo, mpira wa uongozi.

Kupitia mpango mkakati wa chama tuna mpango maalum na ushindi wa wanawake. Mwaka jana katika upya wetu tulifanikiwa kusimamisha wanawake zaidi ya 20 kugombea ubunge, wanawake zaidi ya 100 kugombea udiwani na tulitoa mgombea urais mwanamke. Majuzi tumeshinda uongozi wa mtaa jijini Mbeya. Hakuna mtu angetegemea mafanikio makubwa ya aina hii, lakini imani ya wananchi na chama chetu ndiyo imetuletea mafanikio haya.

Hoja yetu kubwa ni kuwa na viongozi walioandaliwa. Chama chetu kupitia mpango mkakakati wake tumeweka mipango maalum ya kuimarisha uwezo wa uongozi wa wanawake na vijana. Ninawaomba wanawake wote wapenda maendeleo ya nchi hii, magolikipa wazuri wajiunge na chama chetu. Tutaimarisha umahiri wenu, tutasaidiana kufufua ndoto zenu za kuwa magolikipa mahiri zaidi kwa timu za ushindi. 2020 ninataka wanawake zaidi ya 6000 kushika nafasi za serikali za mitaa, wanawake wengine 3000 kushika udiwani, na wanawake zaidi ya 150 kushika nafasi za majimbo ya ubunge na chini ya rais mwanamke vijana wetu na kina baba watacheza kwa bidii wakiwa na uhakika wa ushindi.

Kwa sababu hii ninawakaribisha wakina mama wapenda maendeleo ya nchi yetu kuungana na chama chetu kuvuna mafao ya kuwa magolikipa mahiri watakaozipa familia zetu na jamii yetu kwa ujumla ushindi dhidi ya umasikini, ushindi wa familia imara zinazoongozwa na kina mama wanaojitambua na kujikubali, na wanaojua kuwa kila goli wanalodaka ni kwa mustakabali wa taifa letu.

Siku ya leo ninawashukuru pia ndugu zetu wa vyama vingine vya siasa ambao wamekubali kushirikiana nasi, kusimamia hoja tunayofikiri ilipigiwa kelele na raia wengi juu ya kuruhusu bunge kuendeshwa na matangazo yake kurushwa wazi, kama haki ya msingi ya kupata taarifa sahihi; na watu ama waangalie ama wasikilize popote walipo.

Hoja hii imepata vikwazo vingi bungeni na kijamii, wengine wakiunga mkono na wengine kupinga. Pengine tatizo hasa limekuwa si kuunga ama kukataa lakini jinsi hoja zisizoshibisha akili ya kawaida zinavyotolewa. Kwa kuwa nyuma mambo haya yaliwekwa wazi, kunapotokea mabadiliko ni lazima sababu makini zitolewe, lakini pia kwa sababu ya hali ya kutoaminiana katika mihimili ya uongozi, jambo hili lilihitaji umahiri wa uongozi zaidi kuliko amri na nguvu ya kulazimisha imani.

Imani hujengwa. Kazi kubwa ya uongozi ni kutuaminisha kuwa mnaweza si kutulazimisha kuamini mnaweza. Kwa mfano tumeamini kuwa Rais Magufuli ana dhamira kubwa ya kupambana na matumizi makubwa ya uendeshaji serikali. Tunampa asilimia 100 katika vita hii. Na tunaongeza kusema kuwa vita hii ikiendshwa kidemokrasia, kwa uwazi na uwajibikaji, kusikilizana na kuheshimiana inaweza kuleta tija kubwa na kuliokolea taifa mabilioni na matrilioni ya fedha lakini zaidi matrilioni ya imani kwa Rais na ofisi yake. Waingereza wakishukuru kwa furaha husema kimahaba kabisa “ thanks a million!.” Na mimi leo nasema thanks a million Mr president for fighting graft in our public coffers. Asante sana, wajefya ino! Songela zigizigi, waveja, takso mike ndugu Rais. Kwa hatua hii nawe umeingia kundi la wanawake wadakaji wa mipira ya maendeleo. Tunakupa mapenzi yetu yote.

Ugolikipa wa rais katika vita ya rushwa umefanana na wa kina mama. Lakini ukilaza wa wanafunzi hapana, hapana, hapana. Kama mama ninawaomba radhi sana watoto wangu walioingizwa UDOM kwa mpango maalum, wakatolewa kwa mpango maalum tofauti. Hili mheshimiwa Rais hapana! Hili Mheshimiwa Kikwete hapana. Hili waziri Ndalichako, hapana. Mmepotoka, mlipotoka. Mjisahihishe. Mtusaidie na sisi kujisahihisha. Tujifunze utu, uadilifu na uzalendo katika uongozi wa umma.

Aidha ninawakaribisha nyote wawili kujiunga na chama chetu kuimarisha misingi ya uongozi wa umma. CCM inaonekana kuchoka katika eneo hili na ninyi viongozi wema mnapata vikwazo vya kitendaji kwa kukosa washauri wazuri katika maeneo haya. Mpango mkakati wetu una wigo mpana wa kujengea uwezo viongozi wa umma kufikia lengo hili. Aidha mama Ndalichako, karibu sana ACT kupata vionjo hivi kuondokana na kauli za kujikinza kila wakati.

Kwa hili niseme kuwa kukinzana kwa kauli zenu juu ya jambo hili imelifedhehesha taifa. Imeshusha hadhi ya ofisi hizi na kushusha imani kubwa ambayo taifa lilianza kujijenga kwenu. Aidha makosa yote ya awamu ya nne yalitakiwa kurekebishwa wakati wa kukabidhiana kazi. Mlikuwa na muda wa kutosha kufanya haya. Kuanikana mbele ya umma kila wakati na kuanza kudhuru raia kama wanafunzi ni kinyume na misingi iliyoasisi taifa letu.

Mjisahihishe. Mheshimiwa Kiwete weka wazi mambo yote uliyoharibu wakati wa kipindi chako ujiweke huru. Mafugufuli fanya kazi ya Urais. Waachie wengine majukumu yao, ili sauti yako iwe ya mwisho. Wewe kiwango chako ni cha Sterling yaani muhusika mkuu. Wewe ni size ya super star, be at the top! Remain there.

Serikali ilipe uzito sana suala la wanafunzi wa UDOM. Tunaomba wanafunzi hawa wasikejeliwe, wasibezwe na haki zao zilindwe. Zisikiukwe. Ujenzi wa demokraisa ya vyama vingi Tanzania itujengee dira ya uongozi wetu.  Tujisahihishe.

Katika hili niongeze tena kuwa ujenzi wa demokraisa na vita vya ufisadi vitawezekana tukikamilisha pamoja na mambo mengine mchakato wa katiba mpya. Mheshimiwa ndugu Rais, Maliza kazi hii. Itakusaidia katika mambo mengi  mema unayokusudia kwa nchi yetu. Katiba itaimarisha pia utawala wa sheria na Maadili ya viongozi.

Tunahitaji dira ya taifa kwa ujumla. Tunahitaji dira ya taifa ya elimu. Dira hii itokane na maoni ya raia wote kupitia wawakilishi wa makndi yote ya jamii bila kuwasahau wanafunzi, waalimu, wazazi, wanasiasa, wafanyabiashara na mahitaji ya soko la ajira, vyuo nk. Tupate dira ambayo hakuna waziri wala rais ataikiuka.

Tunalikosea taifa, tunawakosea watoto / wanafunzi na waalimu wanaojitoa kwa ajili ya kuelekeza akili zinazokua. Tunatakiwa tujisahihishe jinsi tunavyoendesha nchi, tunavyotoa na kusimamia maamuzi. Yaliyotokea UDOM, na Chuo cha  Mtakatifu Joseph ni viashiria vya kukosekana uratibu makini na uongozi katika elimu. Tujisahihishe, tutafute suluhu. Tuanze upya, tuendelee.

Program maalum ni jambo la kawaida katika taasisi za elimu duniani, zisiwe kigezo cha migogoro na zisidhalilishe wanafunzi na waalimu na uongozi wa umma kwa kiasi hiki…tujiahihishe!

Kuanzishwa kwa shule za kata ilionesha wazi lengo la kutugawa kati ya watoto wa wenye mali na wavuja jasho wa nchi hii…hatutakuwa na maana kukusanya mapato kulipia wenye nacho….na nchi isiyotunza yatima wake ina maana gani huku duniani? Tujisahihishe!

Mauaji ya Kiraia:

Kwa nini mauaji na uchinjaji wa kiraia? Wizara ya mambo ya ndani kulikoni? Kwa nini mnatupa tu taarifa za matukio bila sababu zake na uwezekano wa kupambana na hali hii. Hatujamsikia waziri mwenye dhamana akilipa taifa taarifa sahihi juu ya jambo hili. Nini kinaendelea?

Umma haujasahau mauaji yanayofikirika kuwa ya kisiasa ya ALPHONSE Mawazo, taarifa yake iko wapi, imethibitisha chanzo cha kifo chake? Na tufanye nini kujikinga na aina hiyo ya mauaji? Hatuwezi kuendelea kuishi  kwa hofu ya kutokujua vyanzo vya mambo. Hatua gani zimechukuliwa kwa wahusika wa ukatili huu.

Mauaji ya GEITA, ya watu kuchinjwa na miili yao kutenganishwa na vichwa kutokana na imani za kishirikina. Mauaji ya kikatili ya Msikitini mkoani Mwanza na kusababisha waumini watatu kuuawa. Mauaji ya TANGA katika Kitongoji cha Kibatini yameleta hofu kubwa na hadi sasa hali si shwari  maeneo hayo. Wanakijiji wameanza kuhama maeneo hayo kutokana na hofu, kutoweka amani, na wananchi wamekosa utu.

Uadilifu na weledi wa jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama unawekewa mashaka hapa, kusababisha wananchi kutojali sheria zilizopo na kujichukulia maamuzi mikononi bila hofu.

Chama cha ACT wazalendo kinalaani mauaji haya na kuzitaka mamlaka zote za serikali kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hii inayoaendelea kuitafuna nchi yetu.



Mwisho.  Mambo yote mazito yapewe uzito wake. Suala la sukari, elimu bure, na gharama halisi za elimu hata kwa shule binafsi. Mipango ya maendeleo vijijini, ukuzaji wa viwanda, kutengeneza na kuongeza ajira na kuimarisha biashara baada ya kero za bandari na TRA kupunguzwa. Maoni ya wananchi tangu serikali ishughulikie ubadhirifu na rushwa TRA na bandari ni kuwa rushwa imeongezeka na kupata thamani tangu juhudi za awamu hii kushughulikia utendaji wa bandari na TRA.

Ushuru wa kuingiza bidhaa bado ni juu kulingana na bei halisi za bidhaa. Kwa mfano raia aliyeingiza bidhaa yenye thamani ya dolla 100 anapotozwa ushuru wa dola 150, ataingia kutaka kutoa rushwa kupunguziwa bei, lakini suala lamsingi halitashughulikiwa na bei halisi za bidhaa zitaendelea kupanda. Heshima kwa TRA nayo itaendelea kushuka, kuwa chombo cha umma cha kukusanya mapato halali. Nyongeza za ushuru hazina risiti na hazitambuliki. Ndio maana tunasema rushwa imepata thamani.

Serikali iangalie kwa upya jambo hili. Bado kuna malalamiko ya urasimu na utoaji haki mahakamani. Kesi bado zinachukua muda mrefu kukamilishwa. Ucheleweshaji wa kesi hushawishi mazingira ya rushwa na ama kunyim haki za wasiotoa rushwa. Kasi ya mahakama hailingani na kasi na mahitaji ya maendeleo ya sasa.

Maisha yanazidi kuwa magumu wakati serikali haionekani kuja na suluhu ya mambo. Tunaunga mkono mapambano dhidi ya rushwa. Tunapinga dalili za kubinya demokrasia na kuingilia utendaji kazi wa mihimili mingine. Katika mazingira ambayo nchi imejaa rushwa, imani kwa vyombo vya umma inapungua kila kukicha, tunahitaji mbinu mbadala za kupambana na rushwa kwa kuimarisha imani na vyombo vya umma.






No comments: