Thursday, June 23, 2016

AZAM KUANZA KUJIFUA JULAI MOSI.

Kikosi cha timu ya Azam.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
BAADA ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja kwa kumalizika msimu uliopita, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imebakiza siku nane tu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa 2016-17. Wachezaji wote wa Azam FC wanatarajia kurejea klabuni  Juni 29 mwaka huu kuanza maandalizi hayo na wataanza rasmi mazoezi Julai Mosi mwaka huu katika makao makuu ya klabu Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Makocha wapya wa Azam FC kutoka nchini Hispania, nao watatua nchini wiki ijayo wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Kocha wa Viungo Jonas Garcia, watakaokuja na wataalamu wengine wa ufundi watatu, Kocha Msaidizi atayekuwa sambamba na Msaidizi wa sasa Dennis Kitambi, wa Makipa na Daktari wa timu.

Kazi ya kwanza ya makocha hao mara baada ya kuwasili itakuwa ni kushughulikia zoezi la usajili linaloendelea hivi sasa, ambapo watatoa hatima y wachezaji wanaobakia ndani ya timu na watakaoachwa pamoja na kuongeza nguvu mpya kwa ajili ya kukipa makali kikosi hicho msimu ujao.

Mabingwa hao wataanza msimu kwa kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) wakiwa kama mabingwa watetezi baada ya mwaka jana kuutwaa ubingwa huo kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa mchezo wowote wala kuruhusu bao ndani ya dakika 90. Michuano hiyo inatarajia kuanza katikati ya mwezi ujao, ambapo Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) liko kwenye hatua za mwisho za kuitangaza nchi itayoandaa baada ya Tanzania kujitoa.

Azam FC pia itakuwa ikijiandaa vilivyo kupigania mataji ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu ujao na ubingwa wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation pamoja na kutimiza adhma yake ya kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani. Ikumbukwe kuwa mbali na Azam FC kutwaa ubingwa wa Kagame Cup msimu uliopita, pia ilifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye ligi na FA Cup huku pia ikiishia hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.   

No comments: