Thursday, June 23, 2016

WATUMISHI WIZARA YA MAMBO YA NDANI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA TARATIBU, KANUNI NA SHERIA ZA UTUMISHI.

 Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bi. Lilian Mapfa akizungumza na watumishi wa wizara hiyo juu ya masuala mbalimbali ya kiutendaji na uboreshaji mazingira ya kazi kwa watumishi  hao katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwa ni sehemu ya  Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma.
 Mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Berious Nyasebwa  akieleza changamoto kadhaa zinazoikabili Idara ya Huduma za Sheria  kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali (Hayupo pichani) katika mkutano uliofanyika leo wizarani hapo leo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo kilele chake ni leo.
 Mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi  Bw. Shomari  akieleza changamoto kadhaa zinazoikabili Idara ya Huduma za Sheria  kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali (Hayupo pichani) katika mkutano uliofanyika leo wizarani hapo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo kilele chake ni leo.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Idara na  watumishi mbalimbali wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza Mkutano wao uliofanyika wizarani hapo katika kuadhimisha kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bi. Lilian Mapfa amewataka watumishi wote wa wizara hiyo kufanya kazi kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za utumishi wa umma ili kuleta ufanisi wa kiutendaji katika kuhudumia wananchi.  

Mkurugenzi Mapfa ameyasema hayo leo wakati akipokea changamoto mbalimbali za kiutumishi kutoka kwa watumishi wa ngazi tofauti wanaofanya kazi katika wizara hiyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo kilele chake ni leo.

Bi. Mapfa amesema kuwa ni muhimu watumishi wakafanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa ndio nguzo kubwa inayoleta ufanisi wa kiutendaji mahali pa kazi na hivyo kufanikisha majukumu ya  wizara. 
Katika kikao hicho ambacho ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa Vitengo vya wizara hiyo pia walishiriki na kupokea kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wao. 

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na malipo ya fedha za likizo, malipo ya kazi kwa muda wa ziada pamoja na vitendea kazi.
Akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na watumishi hao Bibi. Mapfa amesema kuwa ofisi yake imepokea changamoto na kero mbalimbali zilizotolewa na hivyo zitafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya Utumishi wa Umma.  

Aidha Bibi Mafpa amewataka watumishi wote kuimarisha upendo na amani miongoni mwao kwani ndio nguzo pekee inayochangia kuleta maendeleo ya kweli ya wizara na ya mtumishi mmoja mmoja.  
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali 
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

No comments: