Monday, May 16, 2016

HOTUBA YA WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO MHESHIMIWA PROF. MAKAME MBARAWA (MB), WAKATI WA UZINDUZI WA SERA YA TAIFA YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASIIANO YA MWAKA 2016 KWENYE UKUMBI WA MIKUTANO WA WIZARA, DODOMA TAREHE 16 MEI, 2016

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Inj. Edwin Ngonyani,
Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini Tanzania, Cancellor Oscar Kassy,
Katibu Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Prof. Faustin Kamuzora,
Katibu Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi), Dkt. Leonard M. Chamuliho,
Katibu Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Ujenzi), Inj. Joseph. Nyamuhanga,
Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano) Dkt. Inj. Maria Sassabo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Prof. Norman Sigala King,
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma,
Wakuu wa Idara na Vitengo wa  Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mwenyekiti wa TAMNOA, TISPA, TPSF,
Watumishi wa Ofisi ya Ubalozi wa Finland nchini Tanzania,
Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

  1. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia sote kufika na kuwepo mahali hapa, natambua wengi mmewasili kutoka nje ya Mkoa wa Dodoma, nasema karibuni sana.

  1. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imepewa dhamana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kusimamia na kuendeleza Sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili kuwe na miundombinu ya kisasa na inayochangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi na kuongeza pato la Taifa kwa lengo la kumhudumia mwananchi.
  2. Kwa kutambua hilo, Wizara ilianza mpango na utaratibu wa kupitia Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Mwaka 2003 ili kuweza kuwa na Sera mpya inayokwenda na wakati na kuhakikisha kuwa mwananchi ananufaika na kufaidika na huduma za mawasiliano katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
  1. Madhumuni ya kupitia Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 ni kuwa na dira ama mtazamo mpya wa kisera katika sekta ya mawasiliano ili kutumia kikamilifu fursa zilizotokana na utekelezaji wa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 iliyolenga katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha miundombinu ya mawasiliano. Dira ya Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 imetekelezwa kwa kiasi kikubwa ambapo ililenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha miundombinu ya TEHAMA katika ukanda wa Afrika ambayo kwa sehemu kubwa imefikiwa ikiwa ni pamoja na kufanikisha ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliounganisha mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia, kuziunganisha nchi zinazoizunguka Tanzania ikiwemo Visiwa vya Shelisheli na mikongo ya Baharini.

  1. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umefanikisha kushuka kwa gharama za jumla za mawasiliano kutoka Dola za Marekani 20,000 kwa mwezi kwa umbali wa Km zaidi ya 1,000 kwa kipimo cha 2Mbps hadi Dola za Marekani 160 kwa mwezi, sawa na punguzo la zaidi ya 99%; kushuka kwa gharama kwa watumiaji wa mwisho kutoka Sh. 147/dk (2009) hadi Sh. 62/dk (2013) na kushuka kwa gharama za intaneti kutoka sh. 36,000/Gb (2009) hadi Sh. 9,000/Gb (2013) na kushuka kwa gharama za maunganisho (interconnection fees) kutoka Sh. 115/dk (2007) hadi Sh. 34.92/dk (2013). Mafanikio mengine ni  pamoja na wananchi wengi kufikiwa na huduma za mawasiliano yaliyotokana na uanzishwaji wa taasisi za udhibiti na uendelezaji wa TEHAMA; kutambuliwa kwa watalaam wa TEHAMA na kuanzishwa kwa idara na vitengo katika taasisi za Serikali kulikotokana na  kuanzishwa kwa muundo wa kada ya TEHAMA nchini.

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
  1. Sekta ya Mawasiliano imekua kwa kasi kubwa na kuwa moja ya nguzo muhimu ya kukuza uchumi kwa Taifa letu. Ukuaji huu unathibitishwa na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano. Sekta hii huchangia katika uchumi moja kwa moja na kupitia sekta zingine zote kama nyenzo ya uwezeshaji katika kuongeza ufanisi wa utendaji kupitia jamii habari. Takwimu zinaonyesha kuwa laini za simu zinazotumika zimeongezeka kutoka 34,251,801 mwaka 2014 hadi kufikia laini 39,808,419 mwaka 2015 na idadi ya Watumiaji wa intaneti waliongezeka kutoka 14,217,311 kwa mwaka 2014 hadi kufikia  17,263,523 kwa  mwaka 2015. Pia, zaidi ya asilimia 64 ya kaya nchini zinamiliki simu za mikononi. Aidha, vituo vya kurusha matangazo ya radio vimeongezeka kutoka vituo 91 mwaka 2014 hadi kufikia vituo 116 mwaka 2015 na vituo vya kurusha matangazo ya Runinga vilipungua kutoka vituo 28  mwaka 2014 na kushuka hadi kufikia vituo 26  mwaka 2015.  Vilevile, teledensity/penetration rate ni zaidi ya asilimia 79 ambacho ni kiwango cha nchi kufikiwa na huduma za mawasiliano ikiwemo simu, intaneti na utangazaji, na watoa huduma za mawasiliano ya simu na posta pia wameongezeka na kuleta ushindani wenye tija na ufanisi nchini kwa sekta zote.

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
  1. Mafanikio hayo yamewezesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano kutoka asilimia 8.0 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 12.1 mwaka 2015 na hivyo kuwa sekta ya kwanza katika sekta za huduma na kuwa ya pili kwa sekta zote  katika ukuaji hapa nchini. Sekta hii imechangia katika Pato Ghafi la Taifa kwa asilimia 3.6 mwaka 2015. Matokeo haya ya ukuaji na mchango katika teknolojia ya habari na mawasiliano kwa sehemu kubwa kulitokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mawasiliano zikiwemo zile za muda wa maongezi kwa simu za viganjani na mezani, intaneti na utangazaji. Pia, ufanisi huu ulichangiwa na kukua kwa matumizi ya miamala ya kielektroniki ambayo ni pamoja na uuzaji na ununuzi wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa njia za kielektroniki.

  1. Vile vile utafiti kupitia tathmini ya Global Microscope umebaini kuwa Tanzania ipo nafasi ya sita kati ya nchi 55 Ulimwenguni na inaongoza katika Bara la Afrika kwa kuwa na mazingira mazuri ya huduma za kifedha kupitia simu za kiganjani. Vilevile, kwa mujibu wa ripoti ya Fiscope Survey ya mwaka 2015, huduma za kifedha zimewafikia watanzania kwa asilimia 76 kutoka asilimia 44 mwaka 2009 ikiwa imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Mawakala wa Kibenki (Agent Bankings) pamoja na huduma za kifedha kupitia makampuni ya simu kiasi cha kufikia akaunti za miamala ya kifedha (mobile money accounts) kuwa 17,639,349 hadi Desemba 2015.


9.        Tanzania inaripotiwa kuwa nchi ya kwanza duniani kwa kampuni za simu za viganjani kuwa na makubaliano ya kutengamanisha miamala ya huduma ya fedha (interoperability). Hii imewezesha kupunguza gharama za kutuma fedha kutoka mtandao mmoja kwenda mitandao mingine. Jambo hili limewezesha Tanzania kuongoza duniani katika kutumia huduma ya Mobile Money Banking kwa kiasi cha fedha zinazozunguka kwenye mtandao kwa wastani wa Shilingi trilioni 4.5 kwa mwezi. Mzunguko huu wa fedha unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa (gross domestic product) kwa kuwa unaongeza mzunguko wa fedha (money multiplier) kwa kuongeza tija kwenye shughuli za uzalishaji na huduma za kijamii.

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
10.     Pamoja na mafanikio hayo, pia kumekuwepo na changamoto katika Sekta ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa sera kuhusu masafa na rasilimali nyingine adimu za TEHAMA kunakosababisha kupungua kwa ufanisi katika matumizi ya rasilimali hizo adimu; mifumo ya umiliki wa miundombinu kutojumuisha TEHAMA na hivyo kuathiri maendeleo ya huduma za broadband; uhitaji wa mfumo wa kisera wa kukuza fursa kwa Tanzania  kutoa huduma kwa mataifa mengine kupitia TEHAMA (BPO); vifaa na huduma za TEHAMA vinavyotumika nchini kukosa maudhui ya ndani kutokana na kukosekana mwongozo mahsusi; kuongezeka kwa hujuma katika miundombinu ya TEHAMA na ukosefu wa mifumo madhubuti ya kisheria ya kulinda miundombinu ya TEHAMA; kuongezeka kwa uhalifu kupitia mtandao na uvunjifu wa maadili katika jamii; kuongezeka kwa vifaa vya kielektroniki vinavyoisha muda wake kunakosababisha athari kwa binadamu na mazingira; kukosekana kwa motisha za kukuza tafiti na ubunifu katika TEHAMA; na kukosekana kwa mfumo wa kutambua na kuendeleza wataalam na utaalam wa TEHAMA nchini.

11.   Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kutambua hilo, na kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Serikali ya Finland; sekta binafsi na taasisi za Serikali  imewezesha kuhuisha Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 na kuwa na Sera Mpya ya TEHAMA ya mwaka 2016. Sera mpya inatoa mwelekeo na dira mpya inayolenga kuiwezesha Tanzania kutumia fursa zinazotokana na uwepo wa miundombinu ya TEHAMA ili ichangie katika kufikiwa lengo la taifa la nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025; kujenga Jamii Habari itakayoiwezesha nchi yetu kufikia uchumi maarifa na hivyo kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati; na kwenda sambamba na mwelekeo wa Taifa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17- 2020/21) unaolenga kujenga uchumi wa viwanda unaowezeshwa na uwepo wa miundombinu madhubuti ya kiuchumi. Hii ni pamoja na kuunganisha sekta muhimu za uzalishaji na viwanda katika miundombinu ya TEHAMA yenye uwezo mkubwa.

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
12. Pamoja na mambo mengine, Sera mpya ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 imejikita katika kukuza matumizi ya TEHAMA katika sekta za uzalishaji ili kuongeza tija; kukuza tafiti, ubunifu ujasiriamali na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi katika TEHAMA ili kuongeza mchango wa TEHAMA katika kutengeneza ajira; kuimarisha usimamizi na kuongeza ufanisi katika utumiaji wa masafa na rasilimali nyingine adimu za TEHAMA; kuongeza huduma za kielektroniki na kujumuisha maudhui ya ndani katika vifaa na huduma za TEHAMA ikiwemo kutunza taarifa hapa nchini; kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano zenye uwezo wa kubeba huduma zote (simu, video, luninga, intaneti na redio) kwa kasi na uhakika kwa gharama nafuu kote nchini; kuendeleza rasilimali watu ili kuwa na uwezo wa kuendeleza TEHAMA nchini; kuimarisha mfumo wa kuongoza sekta ya TEHAMA; kuimarisha usalama na kujenga imani kwa watumiaji wa mifumo na huduma za TEHAMA; kuimarisha mfumo wa kisheria na udhibiti katika sekta ya TEHAMA; na kuimarisha uhawilishaji wa maarifa na kuvutia uwekezaji.

13. Ni matumaini yangu kuwa, utekelezaji wa Sera mpya ya TEHAMA ya mwaka 2016 itaongeza manufaa kwa Taifa na kuwa ya faida kwa mwananchi mmoja mmoja katika nyanja ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia, kiutamaduni, kisiasa, kimazingira na kwa makundi maalumu. Hii ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma na matumizi salama ya TEHAMA kwa jamii; kuongeza mchango wa TEHAMA katika pato ghafi la Taifa kupitia viwanda vya uzalishaji katika TEHAMA (ujasiriamali katika TEHAMA), ajira kwa wananchi na kuwezesha sekta za uzalishaji kutumia TEHAMA katika uboreshaji wa utendaji kazi; kuongeza upatikanaji na utumiaji wa teknolojia za kisasa, kwa usalama na kwa ufasaha katika maeneo mbalimbali; kutunza kumbukumbu na utamaduni (heritage) kwa kutumia TEHAMA kwa ajili ya vizazi vijavyo; kuongezeka kwa ufanisi katika mifumo ya kisiasa na uwajibikaji;  kulinda kwa mazingira dhidi ya athari hasi za TEHAMA mfano taka za TEHAMA; na kutoa fursa kwa makundi yote katika upatikanaji na matumizi ya TEHAMA.

14. Sera mpya ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ni Sera mtambuka ambayo inagusa sekta zote na Taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na mwananchi mmoja mmoja, hivyo nitoe rai kwa wadau wote kushirikiana kwa pamoja kutekeleza Sera hii kwa maendeleo ya Taifa letu. Aidha, Sera hii inazinduliwa leo ndani ya wiki ya TEHAMA duniani ikiwa ni siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho ya wiki hiyo, yaani Siku ya Mawasiliano na Jamii Habari Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 17 Mei kila mwaka duniani kote, na kwa mwaka huu ina Kauli Mbiu isemayo, “ICT entrerpreneurship for social impact.”  Serikali ya awamu ya tano ya Mhe. Dr. John P. Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kupitisha marekebisho ya  Sera hii imezingatia kauli mbiu hiyo na ndio mwelekeo wa dunia kujumuisha ujasiriamali na ubunifu katika TEHAMA katika kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii kwa kuwashirikisha vijana kuendeleza na kutumia fursa zilizopo katika TEHAMA na hatimaye kupata ajira.

Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
15.   Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuzindua rasmi Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2016.

Asanteni kwa kunisikiliza


Eng. E.A.N

NW - UUM

No comments: