Monday, December 14, 2015

NAIBU Waziri ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jaffo atoa siku 27 kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kuanza kutumia mfumo wa kielekroniki

 Naibu Waziri ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jaffo akishiriki zoezi la kuwapima uzito mmoja wa watoto waliokuwepo katika kituo cha Afya Bahi baada ya kufanya ziara ya kukagua utoaji Huduma za afya katika wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma.
 Naibu waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jaffo akizungumza na wagonjwa Mara baada ya kukagua wodi ya akina mama katika Kituo cha afya bahi.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jaffo akizungumza na watumishi na wakuu wa idara katika halmashauri ya wilaya ya bahi(hawapo pichani), kulia, ni Mkuu wa wilaya ya bahi Fransis Mwonga na kushoto ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Rachel Chuwa.
 .baadhi ya wakuu wa idara katika halmashauri ya bahi.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jaffo(mwenye tai nyekundu) akisikiliza maelezo kuhusu mradi wa maji wa mkakatika kutoka kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya bahi Rachel Chuwa. 
 
NAIBU Waziri ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jaffo ametoa siku 27 kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha wanakamilisha na kuanza kutumia mfumo wa kielekroniki wa ukusanyaji Mapato.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na wafanyakazi na wakuu wa idara wa halmashauri hiyo kufuatia ziara ya kushtukiza ya kuangalia utendaji kazi wa watumishi wilaya hiyo.

Amesema mfumo huo ulitakiwa kuwepo katika halmashauri julai mwaka huu lakini hadi sasa inamsikitisha kuona kuna halmashauri hazijatekeleza suala hilo na kufanya kuendelea kuwepo kwa upotevu wa mapato na kutaka ifikapo januari 10 mwakani kukamilisha mfumo huo kwenye halmashauri zao.

Naibu huyo alisema kwa wilaya ya Bahi ilitakiwa kuwa ya mfano kwa kuweka mfumo huo lakini kutokana na uzembe na inawezekana umecheleweshwa ili kuendelea kufanya mianya ya watu kujipatia fedha.

"Inawezekana mfumo unacheleweshwa kwa makusudi ili kufanya ile mianya ya ukusanyaji fedha kwa njia nyingine uendelee, naagiza hapa itakapofika tarehe 10 Mwezi wa kwanza nataka nipate taarifa hapa, mfumo unafanya kazi na ufungwe idara ya maliasili, afya ili mtu atakayelipa aone fedha inalipwa kwa utaratibu halali, watu wanakosa fedha kutokana na kuingia kwenye mifuko ya watu,"amesema

Amebainisha Mkurugenzi atakayeshindwa kutimiza hilo aandike barua kwa Katibu Mkuu tamisemi kwamba ameshindwa kutimiza uwepo wa mfumo huo.

"Inaonekana aigizo lilitoka lakini watu walishindwa kutimiza majukumu yao na kila Mkurugenzi atawajibika katika hili kwa kushiriki ufisadi wa kuikosesha halmashauri mapato, kila mtu ahakikishe mfumo unakamilika katika halmashauri yake na ukamilike idara zote,"amesema

Katika idara ya utumishi, Naibu huyo amesema kuna vijiji havijafanya mikutano yake tangu uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike Mwezi wa 12 mwaka jana.

Amesema mpaka sasa mwaka umeisha wananchi hawapati taarifa za mapato na matumizi katika vijiji vyao, hivyo maafisa utumishi wahakikishe wanatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha kila kijiji kinafanya mkutano.

Kuhusu malalamiko ya wafanyakazi, Jaffo alisema kumekuwepo na malalamiko ya kupanda madaraja, kulipwa posho za likizo ambapo mwisho wa siku taarifa zile matokeo yake serikali inalaumiwa wakati wanaofanya ni wenyewe kwa wenyewe.

Amesema inawezekana wakuu wa idara husika wanajifanya miungu watu hawatimizi wajibu wao na hawataki kutimiza haki za wafanyakazi wa chini na kutupa malalamiko ya wenzao.

"Sitaki kusikia malalamiko ya watumishi, kuna malalamiko mengine yanaendana na rushwa, mimi nitakapopokea maswali kutoka kwa mbunge kuhusu malalamiko ya wafanyakazi maana yake wewe Mkurugenzi na wakuu wako wa idara hamtoshi,"amesema

No comments: