Tuesday, October 20, 2015

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AWAFARIJI BAADHI YA MAJERUHI

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwafariji baadhi ya majeruhi wa ajali mbali mbali zilizotokea katika ziara za mikutano ya Kampezi mbali mbali za vyama vya Siasa hapa Nchini.
 Balozi Seif akiwapa pole vijana waliojeruhiwa katika ajali ya gari iliyokuwa ikielekea kwenye Mkutano wa Kampeni wa CUF Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja Hapo Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
 Mkuu wa Kitengo cha kupokea Wagonjwa wa dharura katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Juma  Salum Mbwana kati kati akimueleza Balozi Seif hatua zilizochukuliwa na Madaktari katika kuwahudumia majeruhi wa ajali mbali mbali za mikutano ya Kampeni.
 Balozi Seif na Mkuu wa Kitengo cha kupokea Wagonjwa wa dharura katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Juma  Salum Mbwana wakibadilishana mawazo kwenye Wodi ya akina Mama ambao baadhi yao walipata ajali ya gari katika Mikutano ya Kampen za Uchaguzi.

MAJERUHI 10  wanaendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kufuatia ajali tofauti walizopata  wakati wakielekea kwenye mikutano ya Kampeni  za uchaguzi inayoendelea katika sehemu mbali mbali hapa Nchini.

Ajali hizo takriban zote zimehusisha zaidi vijana  waliokuwa wamepanda vyombo ambavyo vyengine vikiendeshwa kwa mwendo wa kasi  na baadhi  vilijaa idadi ya abiria  kupindukia mpaka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata wasaa wa kufika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuwakagua majeruhi hao waliopata athari mbali mbali zikiwemo za kuvunjika viungo na michubuko.

Akiwafariji majeruhi hao  kutoka Vyama vya Siasa vya  CCM katika  Mkutano wao wa  Makunduchi na CUF katika  Mkutano wao wa Nungwi Balozi Seif  aliwatakia Vijana hao kupoa haraka na kurejea katika familia zao waendelee na harakati zao za Kimaisha.

Balozi Seif katika nasaha zake aliwaasa Vijana hao kuwa na tahadhari wakati wanapoendesha vyombo vya usafiri wa Bara barani kama gari na vespa kwani ni vyema wakaelewa kuwa mwendo wa kasi mbali ya kusababisha vifo lakini pia unachangia kuacha vilema vya maisha.

Naye Mkuu wa Kitengo cha kupokea wagonjwa wa dharura katika Hospitali Kuu ya Mnamo Mmoja Dr. Juma Salum Mbwana { Mambi } alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hali za wagonjwa hao zinaendelea vyema.

Dr  Mambi alisema majeruhi waliotokana na ajali hizo wwengi kati yao tayari wamesharuhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa huduma za Matibabu katika Hospitali hiyo.

Kampeni za uchaguzi zilizokuwa zikiendelea katika maeneo mbali mbali Nchini Tanzania zinatarajiwa kufikia kilele chake ifikapo Tarehe 24 Mwezi huu na uchaguzi Mkuu utafanyika Tarehe 25 zikiwa zimebakia siku tano.
Othman  Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/10/2015.

No comments: