Tuesday, September 8, 2015

MABWAWA YA MAJI TAKA ENEO LA VINGUNGUTI KUANZA KUZALISHA GESI.

 Mratibu wa Mradi wa kuzalisha gesi ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa 4 katika fani ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi John Rutahirwa Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu moja ya mtambo wa kukusanyia maji taka kutoka majumbani eneo la mradi wa kuzalisha gesi Vingunguti.Gesi hiyo itaanza kutumika mwezi Desemba mwaka huu.
 Meneja Uhusiano wa DAWASCO Bi.Neli Msuya (kulia) akiwa na Mtaalam anayehusika na ujenzi, mafunzo na usimamizi wa mfumo wa mradi wa kuzalisha Gesi Vingunguti ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange wakionyesha moja ya kifungashio cha Gesi itakayotumika majumbani Kutokana na maji taka yanayokusanywa eneo la Vingunguti.Mradi huo unalenga kuwapunguzia  wananchi gharama za uhifadhi wa maji taka na kuwapatia nishati ya gesi kwa gharama nafuu itakayowasaidia kuondokana na matumizi ya mkaa.
 Jumanne Saidi Fundi ujenzi wa vyoo na msimamizi wa mradi wa majaribio wa Biogasi Vingunguti akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu kazi ya ufungaji wa miundombinu ya kuzalisha gesi katika eneo la Vingunguti.
 Mtaalam anayehusika na ujenzi, mafunzo na usimamizi wa mfumo wa mradi wa kuzalisha Gesi Vingunguti ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu maji taka yanayokusanywa eneo la Vingunguti ambayo yatazalisha nishati ya Gesi na kuwahudumia wanaoishi kuzunguka mabwawa ya Maji Taka Vingunguti.
 Mtambo wa kuzalisha Gesi katika katika eneo la Mradi wa Majaribio eneo la Vingunguti unaokusanya maji taka moja kwa moja kutoka katika makazi ya wananchi.Mtambo huo kwa mujibu wa maelezo ya watalaam wa mradi huo una uwezo wa kukaa ardhini kwa kipindi cha miaka 50.
 Moja ya choo cha kisasa kilichojengwa katika moja ya familia kwa ajili ya mradi wa kuzalisha Gesi katika eneo la Vingunguti.
Eneo la  Mtaa wa mji mpya Vingunguti ambako mabomba ya kupitishia maji taka kutoka kwenye vyoo vya wananchi ambayo huenda moja kwa moja kwenye mtambo wa kuzalishia Gesi.
Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.
 
Na.Aron Msigwa - MAELEZO.
WAKAZI wa mtaa wa mji mpya, kata ya Vingunguti, Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam wako mbioni kuanza kunufaika na mradi wa uzalishaji wa Gesi inayotokana na maji taka ya vyoo vyao na yale ya yaliyo katika mabwawa makubwa ya kuhifadhia maji taka yaliyo katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo unapojengwa mradi wa majaribio wa kuzalisha Gesi, Mratibu wa Mradi huo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa 4 katika fani ya Uhandisi wa Mazingira, Chuo Kikuu cha Ardhi John Rutahirwa amesema kuwa wananchi wataanza kutumia gesi itakayozalishwa kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.

Amesema kazi ya kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya mradi huo inaendelea chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji Taka (DAWASA) kwa kushirikiana na Wanafunzi wa fani ya Uhandisi wa Chuo Chuo Kikuu cha Ardhi na Taasisi isiyo ya kiserikali ya wanafunzi wanaosomea fani ya uhandisi wa Mazingira (CDI) ya Chuo kikuu cha Cambridge, Uingereza.

Amesema wanafunzi wanaosomea fani ya Uhandisi wa Mazingira wa Chuo Kikuu cha Cambridge,Uingereza kwa kushirikiana na baadhi ya wanafunzi wanaosomea Uhandisi wa Mazingira wa Chuo Kikuu cha Ardhi nchini Tanzania walikuja na wazo na kubuni mradi huo wenye lengo la kuboresha maisha kupitia maji taka.

Amesema chini ya uratibu wa DAWASA yenye jukumu la kusimamia miundombinu ya maji taka na Taasisi ya mikopo la Bridge for change  ya Tanzania inayotoa mikopo midogo midogo kwa wananchi walianza kufanya mapitio kwa  kila nyumba ili kuona namna wanavyoweza kutumia changamoto ya maji taka katika eneo hilo kwa kuigeuza kuwa fursa.

Amefafanua kuwa wakihusisha wataalm wa mradi na viongozi wa mtaa wa vingnguti mji mpya, walianza  kuzungumza na kujadiliana na wakazi wa eneo hilo ili kuwezesha kazi ya  kuunganisha vyoo vyao katika mtandao wa mabomba ya kusafirisha maji taka kuelekea kwenye mtambo wa kuzalisha gesi.

Amefafanua kuwa  chini ya mradi huo maji taka yote kutoka kutoka katika  nyumba zilizounganishwa kupitia mabomba yanakusanywa  na kusafirishwa moja kwa moja  kwenye  mtambo wa kuzalisha gesi.

Kwa upande wake Mtaalam anayehusika na ujenzi, mafunzo na usimamizi wa mfumo wa mradi huo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya Uhandisi wa Mazingira Chuo Kikuu cha Ardhi Rukia Yange amesema mradi huo ambao uko kwenye majaribio unalenga kuwapunguzia  wananchi gharama za uhifadhi wa maji taka kwa kuwapatia nishati ya gesi kwa gharama nafuu itakayowasaidia kuondokana na matumizi ya mkaa.

Amesema kwa kuanzia utawanufaisha  watu 150 wa eneo hilo na kuongeza kuwa kuanzia Desemba mwaka huu wataanza kuiweka gesi hiyo katika vifungashio maalum vitakavyoanza kusambazwa majumbani mwao tayari kwa matumizi.

Amesema gesi hiyo itamwezesha mwananchi kuitumia kwa kipindi cha mwezi mmoja na kupunguza  matumizi makubwa ya mkaa na uharibifu wa mazingira.

Aidha, amesema gharama za mwananchi kuunganishwa katika mfumo huo inaanzia shilingi 150,000/ kwa wale walio na vyoo vinavyoruhusu mfumo huo na  shilingi 700,000/= kwa mwananchi anayetaka kujengewa choo kipya katika eneo lake la makazi gharama ambazo hulipwa kidogo kidogo kupitia utaratibu wa mikopo nafuu ulioanzishwa.

Naye Meneja Uhusiano wa DAWASA  Bi. Neli Msuya akifafanua kuhusu mradi huo amesema suala la ujenzi wa miundombinu ya kuchukualia maji taka na matumizi ya gesi itakayozalishwa litakwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi hao juu ya matumizi na uhifadhi wa gesi hiyo.

Amefafanua kuwa DAWASA inaendelea kuendesha mafunzo ya uzingatiaji wa usalama katika matumizi ya gesi hiyo pamoja na suala la usafi, utunzaji na ulinzi  wa miundombinu ya kusafirishia maji taka iliyojengwa katika eneo hilo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu.

Ameeleza kuwa mbali na mradi wa kuzalisha gesi DAWASCO kwa kushirikiana na wadau wa matumizi ya Nishati endelevu na uhifadhi wa mazingira inatarajia kuanzisha mradi wa kuzalisha mbolea itakayotokana na maji taka yaliyohifadhiwa katika eneo hilo.

"DAWASA tukishirikiana na wadau mbalimbali tuna mpango wa kuyatumia maji taka haya yaliyohifadhiwa kuzalisha mbolea itakayotumiwa na wakulima katika shughuli za kilimo,tunalenga kuibadilisha changamoto hii ya maji taka kuwa fursa itakayowanufaisha wananchi badala ya kuwa kero kwao" Amesisitiza.

Wakiuzungumzia mradi huo baadhi ya wakazi wa mtaa wa mji mpya ambao vyoo vyao vimeunganishwa kwenye mfumo wa kusafirishia maji Taka wamesema mradi huo ni ukombozi katika maisha yao kwa kuwa umewapatia vyoo bora na kuwaondolea adha na gharama ya uhifadhi wa maji taka    waliyokuwa wakiipata hapo awali kutokana na ujenzi holela wa makazi yao.

Wameongeza kuwa mradi huo umewasaidia katika uhifadhi wa mazingira na kuondoa tatizo la utiririshaji wa muda mrefu wa maji taka uliosababishwa na uwepo wa mifumo mibovu ya vyoo vyao.

Wamesema kuwa kutokana na uimarishaji wa mifumo ya kusafirisha maji uliofanywa na DAWASA kwa kushirikiana na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Cambrige (CDI) na Taasisi ya utoaji wa mikopo ya Bridge for Change  wameondoa hofu waliyokuwa nayo ya kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu na kutoas wito kwa wananchi  katika maeneo mengine kujiunga na mradi huo.

No comments: