WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda(Pichani) amekabidhi magari mawili ya kubeba wagonjwa yenye thamani ya
sh. milioni 150 kwa uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro ili yapelekwe kwenye kituo cha
afya cha Enduleni na hospitali ya Wasso ambayo inatumika kama hospitali ya wilaya.
Waziri
Mkuu amekabidhi magari hayo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Septemba
2013 alipofanya ziara ya kikazi ya mkoa wa Arusha na kubaini adha ya usafiri
iliyokuwa ikiwapata wakazi wa kata za Wasso na Enduleni zilizoko wilayani
Ngorongoro.
Akizungumza
na watumishi wa idara ya afya na wananchi waliohudhuria makabidhiano hayo leo mchana,
(Jumanne, Septemba 8, 2015), Waziri Mkuu alisema aliyapata magari hayo kwa
wafadhili kutoka Japan na sehemu nyingine ambayo haikuitaja.
“Nikiwa
ziarani Japan, Machi mwaka huu, nilikutana na Watanzania waishio Japan nikawaomba
kama wanaweza kunisaidia gari la wagonjwa hata kama limetumika sababu najua
kule magari yaliyotumika huwa yanakuwa hayajachoka. Watanzania wale walikubali
na kuamua kunisaidia kutekeleza ahadi yangu,” alifafanua Waziri Mkuu.
Alisema
mara baada ya ziara yake, alipeleka maelekezo ya kupata magari kwa ajili ya Wasso
na Enduleni kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii lakini kutokana na upatikanaji
mgumu wa fedha za bajeti, ombi hilo halikufanikiwa ndipo akaona atafute njia
nyingine ya kuwasaidia wakazi hao.
“Ahadi
ya Serikali ya kuwapatia gari la wagonjwa wakazi wa Wasso na Enduleni bado iko
palepale lakini niliona ni vema wakati wakiendelea kusubiri fedha zipatikane, bora
tutafute njia nyingine ya kuwasaidia kupunguza tatizo la usafiri kwa wagonjwa
linalowakabili wakazi hao,” aliongeza.
Waziri
Mkuu alikabidhi funguo za magari hayo mawili kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro,
Bw. Hashim Mgandilwa pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw.
John Kurwa.
Hafla
hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Felix Ntibenda Kijiko na viongozi
wengine wa mkoa wa Arusha na waganga wakuu vituo vya Enduleni na Wasso.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE,
SEPTEMBA 8, 2015.
No comments:
Post a Comment